Monday, July 16, 2012

UNAJUA NINI KUHUSU MILLARD AYO..... YASOME HAPA YANAYOMUHUSU


Mo Blog: Tunamsikia Millard Ayo lakini hatujui ni nani hasa.?
Millard Ayo: Milliard Ayo ni kijana wa miaka 26 aliyezaliwa tarehe 26 Januari mwaka 1986 ni kijana aliyezaliwa katika hospitali ya Mount Meru na ni mtoto wa kwanza kwenye familia ya watoto wanne.
Ninatoka katika familia ya Mzee Arael Ayo al maarufu kama ‘Chalii’ pale Tengeru mkoani Arusha.
Mo Blog: Tupe siri ya mafanikio yako pamoja na umaarufu ulionao.?
Millard Ayo: Kiukweli moja kati ya vitu vinavyonifanya mimi nipate mafanikio, namshukuru Mungu kwa sababu kwanza situmii vitu vinavyowaangusha watu wengi kwenye kazi kama hizi; kwanza kabisa mimi sinywi pombe na sijawahi kunywa tangu nizaliwe; nadhani inanisaidia pia kwa sababu wakati wote akili inakuwa ‘fresh’.
Mo Blog: Kwa kifupi tuambie ilikuaje mara ya mwisho tumekusikia Radio One ghafla Clouds FM.?
Millard Ayo: Clouds Fm walivutiwa na kazi yangu, nadhani waliona uwezo wangu kupitia show ya ‘Milazo 101’ niliokuwa nikiifanya Radio One so alinipigia simu bosi wao nakumbuka ilikuwa ni siku ya Jumatano akaniambia tuonane.
Ukizingatia mimi nilikuwa na dream sana kufanya kazi ‘Clouds’ hata wakati naingia college ya Journalism nilikuwa na ndoto za kufanya kazi Clouds.
Mo Blog: Ayo tufafanulie kote ulikopita na hatimae hapa ulipo.?

Millard Ayo: Kiukweli nimefanya kazi TVZ Zanzibar, Wapo Radio -Dar es Salaam na ITV/Radio One kwa miaka mitatu; kote nilikuwa nafanyakazi na sisemi kwa nia mbaya, lakini Clouds ni Radio ambayo nilikuwa nimei’dream’ kuifanyika kazi kwenye maisha yangu.
Mo Blog: Zungumzia filamu za ki-bongo, kwa mtazamo wako tunaelekea wapi.?
Millard Ayo: Filamu za kitanzania zamani nilikuwa siangalii, lakini sasa hivi naangalia sana kwa sababu napenda kujifunza sana, mimi sikuzote napenda mtu ambaye anakubali kurekebishwa.
Filamu za kitanzania zina soko kubwa sana kwa watanzania, kwa sababu watanzania wanapenda vitu ambavyo wanavielewa; vitu ambavyo vina’happen’ kwenye maisha yao. Pia hakuna kitu kizuri kuwaona watu ambao unawafahamu wakiigiza inaleta uzalendo zaidi.
Mimi ningependa kuona waigizaji wa Tanzania wakitumia muda mwingi zaidi kujiandaa kwa ajili ya movie na waandaaji watumie fedha nyingi kutengeneza filamu ziwe na ubora unaostaili na naamini zitauza zaidi.
Mo Blog:  Tupe siri ya sauti yako..?
Millard Ayo: Mwenyezi Mungu ndio anajua, Mwenyezi Mungu ndio muweza wa yote na Mwenyezi Mungu ndio aliyopanga kila ninachokifanya kwenye hii dunia. Amepanga niumbike au kuzaliwa niwe hivi. Najua kupitia Mwenyezi Mungu haya yote yamewezekana. Sauti yangu sijaitengeneza ni sauti ambayo nimezaliwa nayo.
Mo Blog: Sasa hivi unatisha na kipindi almaarufu cha ‘Amplifaya’ hebu tumegee kidogo wazo la kipindi hiki.
Millard Ayo: Wakati naingia Clouds hii ilikuwa ‘idea’ ya show ambayo nitaifanya, baadae tuka kaa pamoja na mkuu wangu wa vipindi ndio tukapata mawazo mengine tukayajumuisha pamoja ikaanza show.
Amplifaya imetumika kama neno la kuonesha kama tunarahisisha siku yako; yaani tuna-amplify. Kwa mfano ndani ya shoo hii ya saa mbili kuna ‘habari Kumi za Siku’ lengo ni kukuhabarisha yaliyotokea pengine ulikuwa katika mihangaiko hukupata muda wa kusikiliza vyombo vya habari.
Mo blog: Katika siku za hivi karibu kuna suala lililochukua nafasi kubwa katika midomo ya watu, suala la Freemason haswa kwa watu maarufu kama wewe. Unazungumziaje?
Millard Ayo: Mimi Freemason siijui naisikia tu kwa watu kwa hiyo siwezi nikatolea ufafanuzi zaidi kwa sababu sina elimu nayo, sijawi kushudia vitu kama hivyo kwa hiyo nawaachia wanaofahamu. Kwa kweli siwezi ku-comment’ chochote.
Mo blog: MO BLOG ingependa uzungumzie maisha yako ya kimapenzi maana tumesikia mengi.!
Millard Ayo: Wakati mwingine unapokuwa ni mtu wa kufahamika vinaweza vikazushwa vitu vingi sana, na kuna taarifa nyingi sana kuhusiana na maisha yangu ya kimapenzi ambazo sio za kweli.
Kiufupi ni kwamba mimi nina ‘girlfriend’ niko nae huu ni mwaka wa tatu sasa na ni huyo peke yake.
Mo Blog: Kumezuka utamaduni wa watu mbali mbali kufungua ‘Blogs’ hebu zizungumzie kama unavyozijua.
Millard Ayo: Kiukweli mimi napenda sana, kwanza watu wanaojituma kwa nguvu zao wenyewe . kufunguliwa kwa blogs nyingi kila siku sioni kama ni kitu kibaya ni kitu kizuri sana, kwa sababu kila mtu ana ubunifu wake, kila mtu ana nguvu yake. Cha msingi ni kufanya kitu ambacho kinaendana na lengo la kufunguliwa kwa blog. Napenda sana kuona blogs mbalimbali.
Mo Blog: Umekuwa mtangazaji muda mrefu sasa nini hutokisahau radioni?
Millard Ayo: Katika maisha yangu mimi sababu ya utangazaji nimewahi kufanya vitu vingi kwenye radio lakini kuna shows tatu ambazo siwezi kuzisahau ambazo niliweka nguvu nyingi sana. ‘Vipaji Halisi’-Wapo Radio, ‘Milazo 101’-Radio One na ‘Amplifaya’-Clouds FM.
Amplifaya ndio ninayofanya sasa hivi na nimeahidi moyoni nitazidi kuweka nguvu kuifanya vizuri zaidi kuanzia mwanzo hadi mwisho moto utakuwa uleule. Hii show sio kwamba naifanya kwa kuwa ni kazi hapana na-enjoy kufanya na nafurahi kuwa Clouds FM. Namuomba Mungu anipe nguvu.
Mo Blog: Changamoto gani unakutana nazo katika kazi wewe kama Millard Ayo..?
Millard Ayo: Kuna changamoto nyingi sana lakini labda kubwa ni pale ambapo ninataka niwe wa kwanza kutoa habari yaani nitoe ‘exclusive’. Hii ndio changamoto inayonifanya nichelewe kulala, ndio maana ukifungua web site yangu unaweza kuona nimeweka stori ya tukio lililotokea labda saa nane usiku. Ina maana nilikuwa eneo latukio. Napenda sana kuwa wa kwanza kutoa habari ‘always’.
Mo Blog: Kama Millard lipi tukio la kukumbuka sana duniani.?
Millard Ayo: Tukio la kukumbuka sana kwangu ni siku nipotolewa katika chumba cha mtihani wa kumaliza katika Chuo cha Uandishi wa Habari. Nilitolewa kwa sababu sikuwa nimemalizia kulipa. Baba yangu kipindi hicho gari yake ilikuwa imevamiwa na majambazi akipeleka watu mnadani. Lilipigwa risasi kwa hiyo likawa liko gereji. Ile hela ya akiba akawa ameitumia yote ikaisha na bado gari halikupona.
Halafu mama yangu ni mwalimu akawa amewalipia ada wadogo zangu waliokuwa wasoma katika hizi shule za Medium akawa hana pesa kabisa, yaani kwenda shuleni nilikuwa natembea wakati nauli ni shilingi 150/- au 200/-. Natoka Ngarenaro mpaka Stadium kila siku asubuhi na jioni kurudi nyumbani hata hela ya kula mchana inakosekana.
Baada kushindikana kabisa kupatikana ada, mama yangu akajaribu kwenda kuongea na wale masekretari ili wamkubalie nifanye mtihani kwa sababu alikuwa akijuana nao kinamna, lakini ikashindikana kwa sababu walikuwa wameachiwa maagizo kuwa siwezi kufanya mtihani mpaka nimalize ada na ilikuwa imebaki 300,000/-.  Nikiamini mama atamaliza nao nikaingia katika chumba cha mtihani nikaanza kufanya baada ya kama dakika 10 au 12 hivi nikaja kutolewa tena nakumbuka ulikuwa ni mtihani wa ‘Video Shooting’.
Yaani nilipotolewa nikawa niko na mama analia mimi nalia nakumbuka nililia sana maana mtihani huo ulikuwa ndio-final, inamaana nisipofanya inabidi nisubiri tena mwakani.  Mama akaniambia anakwenda asipopajua popote Mungu atakapo muongoza akatafute hiyo ada, basi nikamsubiri pale chuo chini kuna-kimgahawa nikalia sana mpaka dada mmoja aliyekuja kunihudumia chai akaniuliza unalia nini?
Akanibembeleza sana lakini nikawa nalia tu nashindwa hata kuongea akaniambia hata hiyo chai kunywa tu bure usilipe sema unataka nini kingine mi nikawa nalia tu.
Baada ya kama dakika 35 au 45 hivi nikamuona mama anakuja ‘speed’ anakimbia akitokwa machozi akaniambia nimepata hela mwanangu twende. Tukapanda tena mpaka ofisi ya chuo akalipa mimi nikaambiwa niende kwenye chumba cha mtihani.
Nashukuru kwamba somo lenyewe nilifaulu nilipata 93 kwa sababu nilikuwa nalipenda. Yaani jambo hili ndugu zangu wana Mo Blog sitakisahau.
CHANZOMO BLOG

No comments: