Tuesday, July 10, 2012

MWENYEKITI WA MADAKTARI, DR NAMALA MKPOI KIZIMBANI

Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam leo ilifurika umati wa watu waliofika kufuatilia kesi inayomkabili Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Namala Mkopi (pichani).


Dk. Mkopi amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ambapo alisomewa mashitaka mawili.Mashitaka hayo ni kukiuka amri halali iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi iliyomtaka yeye na wanachama wake kutoshiriki au kujihusisha na mgomo wa madaktari na kuhamasisha mgomo kinyume na amri hiyo.

Dk. Mkopi alisomewa mashitaka hayo leo na Wakili wa Serikali Mwandamizi Tumaini Kweka akisaidiana na Wakili wa Serikali Ladislaus Komanya,mbele ya Hakimu Mkazi Faisal Kahamba.

Wakili Kweka akisoma mashitaka alidai kati ya Juni 26 na 28, mwaka huu, Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa Rais wa MAT hakutii amri halali ilitolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi ambayo ilimtaka atoe tangazo kwa kupitia vyombo vya habari kwa wanachama wake kutoshiriki au kujihusisha na mgomo.

Amri ambayo ilitolewa na mahakama Juni 22, mwaka huu.

Shitaka la pili, Dk. Mkopi anadaiwa Juni 27, mwaka huu, Dar es Salaam, waliwashawishi wanachama wa chama cha MAT Tanzania Bara kushiriki mgomo ikiwa ni kinyume na amri iliyotolewa na Mahakama ya Kazi, Juni 22, mwaka huu.


Dk. Mkopi alikana mashitaka hayo, ambapo upande wa mashitaka ulidai upelelezi haujakamilika.Mawakili wa Dk. Mkopi Isaya Matambo, Dk. Maurid Kikondo, Dk. Gaston Kenedy na Dk. Rugemeleza Nshala waliomba mteja wao apatiwe dhamana kwa kuwa mashitaka yanayomkabili yanadhaminika.Hakimu Kahamba alitoa masharti ya dhamana ambayo mshitakiwa awe na wadhamini wawili waajiriwa wa serikali au kutoka taasisi inayotambulika kila mmoja atatia saini dhamana ya sh. 500,000.Wakili wa Serikali aliiomba mahakama izingatie kifungu cha 148(6) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kinachoelekeza masharti ya nyongeza wakati wa kutoa dhamana ambayo ni mshitakiwa kuwasilisha polisi hati za kusafiria na kutotoka nje ya mkoa husika bila ya kibali cha mahakama.kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 6, mwaka huu, kesi itakapotajwa kutokana na kutimiza masharti hayo Dk huyo yuko nje kwa dhamana.

No comments: