Sunday, July 8, 2012

MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR AMSHANGAA TUNDU LISU

MWANASHERIA Mkuu wa Zanzibar Othman Masoud Othman ameshangazwa na mwanasheria mwenzake Tundu Lisu kwa kutofahamu madhumuni na malengo ya mabadiliko ya katiba ya Zanzibar yaliozaa serikali ya umoja wa kitaifa. 

Kauli ya Mwanasheria huyo aliitoa katika baraza la wawakilishi wakati akifafanua baadhi ya mambo ya kisheria baada ya wajumbe wa baraza hilo kumtaka afanye hivyo kufuatia kauli ya ya Tundu Lisu aliyoitoa bungeni wiki hii.




“Sasa kuja kwa haya yametuonesha kwamba kuna wenzetu kumbe wana fikra kwamba Zanzibar iliwahi kutawaliwa. Maana mtu anaposema marekebisho ya 10 ya Zanzibar yamjitangazia uhuru maana yake ana fikra na huyu ni mwanasheria mtu kafika mpaka kuwa mbunge anayeaminika na chama chake lakini anasema kwa kufanya hivyo Zanzibar imejitangazia kuwa huru kwani tuliwahi kutawaliwa?,” alihoji Othman.


Akijadili bajeti ya wizara ya makamu wa rais wa jamhuri ya muungano, huko Dodoma Mbunge wa Singida Mashariki wa Chama Cha (CHADEMA) Tundu Lisu alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa Zanzibar imefanya katiba kwa kujitangazia kuwa ni nchi.


Othman alisema marekebisho ya katika ya Zanzibar yalikuja baada ya hoja nyingi ambazo hazikuwa na majibu katika muungano ambayo ilikuwa ikisema ni Zanzibar ni sehemu ya muungano, lakini kama nini mkoa? Shehia? Kata? au kijiji?, haya hayakuwa na jibu katika katiba ya muungano.



Kufuatia maridhiano Zanzibar ndipo wazanzibari wakamaua kufanya kukufikia marekebisho ya 10 ya katiba yao ambayo ilifafanua kuwa zanzibar ni nchi na ndivyo ilivyo kwa sababu haikuwahi kutawaliwa kama ambavyo baadhi ya wanasiasa wanavyofikiria.



“Marekebisho ya 10 ilichofanya ni kusema kwamba ikiwa mtu hatambui, maana ilikuwa imeshaonesha dalili kwamba kuna wengine hawatambui hilo tena wakubwa. Sasa marekebisho ya 10 yalipokuja ni kufafanua tu, kama kuna mtu hatambui sisi wenyewe tunajitambua” alisema mwanasheria huyo huku akiungwa mkono na wajumbe kwa kupigiwa makofi.



Huku akishangiriwa na wajumbe wa baraza hilo mwanasheria mkuu alisema hakuna mtu ambaye atawazuwia kusema “Aaah katiba yenu isiwe namna gani au isiwe hivi na ndio maana unakuta katiba za muungano zipo nyingi lakini kila mmoja ina muundo wake kwa mujibu mlivyokubaliana nyinyi wenyewe.”



Mwanasheria mkuu alisifu muungano wa miaka mingi wa Uswizi ambao unatambulika na kuigwa duniani kutokana na kufuata misingi imara iliyowekwa na wananchi wenyewe.



Alisema muungano ambao umedumu na unasifiwa ni Swiss Federation kwa sababu umeanza tokea mwaka 1292 na umekwenda kwa mafahamiano hadi mwaka 1874 wakatunga katiba ambayo wameifanyia mapitio upya mwaka 1999 na nchi hiyo ina serikali 26, lugha nne rasmi na ndio muungano amabo umedumu na nchi ambayo ni imetulia duniani.



Mwanasheria huyo alisema mashirika yoye ya kimataifa yapo Uswizi kwa sababu ya muungano huo uliotumilia na kwa sababu umekuwa na misingi imara ya kuhakikisha muungano ule unaweza kuhimili mabadiliko yoyote yatakayokuja ya kisiasa.

No comments: