Monday, July 9, 2012

MAWASILIANO IKULU: MGOMO WAMADAKTARI UMEISHA, HAKUNA CHA KUJADILI


Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salvatory Rweyemamu kujibu swali aliloulizwa na gazeti la HABARI LEO kuhusu ombi hilo la viongozi wa dini, alisema mambo ya msingi kwa sasa ni manne.

“Kwamba mgomo wa madaktari umeisha na walioamua kuendelea na kazi hii muhimu sana ya kutibu binadamu wamerudi kazini. Hili ni jambo jema sana. Sasa siyo wakati wa kulumbana tena bali ni wakati wa kusonga mbele badala ya kurudi nyuma kwa sababu hakuna mgomo tena wa kujadiliwa.

“Kwamba tokea madaktari walipoanza kudai maslahi zaidi, Serikali ilifanya jitihada kubwa za kukutana na madaktari hao.
Mbali na Kamati ya Majadiliano ya Serikali, Madaktari pia wamekutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda. Kamwe, Serikali haijapata kukataa kukutana na viongozi wa madaktari,” alieleza Mkurugenzi huyo.

Alieleza kuwa mara ya mwisho madaktari hao walipoitwa kukutana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Hussein Mwinyi walikataa wakidai kuwa Waziri hakuwa na jambo jipya la kuwaambia.

“Huu ni ushahidi mwingine kuwa kamwe Serikali haijapata kukataa kukutana na kuzungumza na madaktari,” alieleza. 

“Kwamba mara zote walipoomba kukutana na viongozi wa Serikali, akiwemo Rais, hawakupitia kwa mtu yeyote isipokuwa waliomba moja kwa moja na wakakubaliwa. Hivyo, hawana sababu ya kupitia kwa watu wengine kuomba kukutana na viongozi wa Serikali,” Mkurugenzi huyo aliutaja msingi mwingine.

Moja ya hoja za madaktari hao waliogoma ni kutaka kulipwa mshahara zaidi na Serikali na katika mapendekezo yao walitaka kulipwa Sh. milioni 3.5 kwa mwezi kwa daktari anayeanza kazi; kiwango ambacho ukijumuisha na madai mengine ya posho kinafikia Sh. milioni 7.7.

Rais Kikwete katika hotuba yake ya mwisho ya mwezi Juni, aliwaeleza madaktari hao kwamba Serikali haina uwezo wa kulipa kiwango hicho, na kwamba wako huru kutafuta mwajiri mwingine anayeweza kuwalipa, na hivyo hawana sababu ya kugoma.

“Kama daktari anaona kuwa hawezi kufanya kazi Serikalini bila ya kulipwa mshahara huo (Sh. milioni 7.7) awe huru kuacha kazi na kwenda kwa mwajiri anayeweza kumlipa kiasi hicho,” alisema Rais Kikwete.

ENDELEA KUSOMA ZAIDI HAPA...GAZETI LA Habari Leo

No comments: