Friday, July 13, 2012

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA ARDHI NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI MHE. HALIMA JAMES MDEE (MB) KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2011/12 MA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI MWAKA WA FEDHA 2012/13.


UTANGULIZI
Mheshimiwa  Spika, napenda kuchukua  nafasi hii  kumshukuru Mwenyezi Mungu  kwa kuniwezesha kuwepo hapa leo  kuwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani  kuhusu Wizara  ya Ardhi, Nyumba  Na Maendeleo ya Makazi .
Mheshimiwa Spika, pia nikushukuru wewe  kwa kuniruhusu  kutoa maoni  ya Kambi ya Upinzani  kuhusu Wizara hii  kwa mujibu wa  Kanuni  ya 99 kanuni ndogo  ya (7) , ya Kanuni  za Bunge  Toleo la Mwaka  2007.
Mheshimiwa Spika, pili ningependa  kutoa shukrani zangu za dhati  kwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo  (CHADEMA) na wananchi wa Jimbo la Kawe ( wapiga kura wangu) kwa imani  yao kwangu, makamanda wote (vijana, wazee na akina mama wa vyama vyote)  kwa kuendelea kuniunga mkono katika kuhakikisha Jimbo letu linapata huduma  zote za msingi zinapatikana katika viwango stahili. Ahadi yangu kwenu ni kuwatumikia kwa uwezo wangu wote kwa kadiri Mwenyezi Mungu atakavyoniwezesha!
Mheshimiwa Spika, napenda pia kutoa shukrani za dhati kwa CHADEMA kikiwa chini ya Mtendaji wake mkuu (KATIBU MKUU-TAIFA), Mhe. Wilbroad Peter Slaa. Hakika  kila Mtanzania anaona kazi unayoifanya ya kuhakikisha chama chetu kina kuwa juu na Watanzania wote wanatuunga mkono. Mungu akupe uhai, naamini ipo siku tutaifikia Nchi ya Ahadi!
Mheshimiwa Spika,  sina budi kumshukuru  Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Mhe. Freeman Aikaeli Mbowe, kwa kuniamini  na kuniteua tena kuwa Msemaji Mkuu wa  Kambi ya Upinzani  katika Wizara hii. Shukrani pia ziende kwa  wasaidizi wa Kiongozi wa Kambi, Kabwe Zitto (Naibu Kiongozi wa Kambi) na Tundu Lissu (Mnadhimu wa Kambi) kwa kutuongoza vyema katika shughuli hii ngumu ya kuwatetea wanyonge. Shukrani pia ziwafikie wabunge  wenzangu  wote wa Kambi kwa ushirikiano wao kwangu.

Mheshimiwa Spika, kipekee niishukuru sana familia yangu yote, wazazi wangu Prof. James Salehe Mdee na Theresia Kisenga Ngowi kwa upendo wao na kwa upekee nimshukuru kaka yangu Joseph James Mdee,kwa msaada na ushauri mkubwa katika kuhakikisha natimiza majukumu yangu ya kibunge ndani na nje ya Bunge. Asanteni sana!!!

 HOJA ZA KAMBI YA UPINZANI 2011/12

Mheshimiwa Spika, kufuatia hotuba ya Kambi ya Upinzani Bungeni ya mwaka 2011/12 Kambi ya upinzani inatambua hatua zilizochukuliwa na serikali  katika hoja kadhaa ambazo ziliwasilishwa kwake hususan suala la  ada ya ukodishwaji wa mashamba na vitalu ambapo serikali ilikuwa inatoza shilingi 220 tu kwa eka. Kauli ya serikali kupitia Naibu Waziri wa ardhi wakati akichangia hotuba ya mapitio  na mwelekeo  wa kazi za serikali  na makadirio  ya matumizi ya fedha  ya Ofisi ya Waziri Mkuu 2012/2013 imeonyesha nia ya serikali kuongeza ada husika ili kuiongezea serikali mapato.

Kambi ya Upinzani inatambua pia hatua ambazo serikali imeahidi kuzichukua katika mwaka huu wa fedha 2012/13 kwa kutenga fedha za fidia kwa wananchi wa Kurasini Mabwawani. Serikali imeeleza kwamba fidia zitalipwa kwa viwango vipya kuendana na thamani ya soko!

Halikadhalika, Kambi ya Upinzani inatambua hatua zitakazochukuliwa na serikali kuhusiana na mwekezaji Agrisol , ili  kuiepusha nchi kuingia kwenye mkataba mbovu usiozingatia maslahi na sheria za nchi. Kambi ya upinzani imefarijika na Kauli ya Waziri Mkuu wakati akihitimisha hotuba yake ya bajeti ambapo, pamoja na mambo mengine alitamka kwamba mchakato wa Agrisol haujaanza, hawajaingia makubaliano/mkataba  ”wowote” na kwamba mchakato ukianza ndipo wataingia kwenye mambo ya msingi waone  wanapangiana vipi, uwiano utakuwaje na kwamba halmashauri imiliki kiasi gani cha hisa!

Mheshimiwa Spika, rai ya Kambi ya Upinzani ni kwa serikali  kusitisha mpango wake wa kuligawa eneo la Mishamo na Katumba  lenye ukubwa  wa zaidi ya hekta 325,000 au ekari 760,728 kwa AGRISOL. Kuna taarifa kwamba tayari serikali ilishaligawa eneo la  Lugufu lenye ukubwa wa hekta 10,000 kwa AGRISOL (kwa kuwa mikataba  inaendeshwa kwa usiri mkubwa.) Ni imani yangu  Serikali itatupa jibu juu ya mustakabali wa Lugufu.

Mheshimiwa Spika, wakati serikali ikitafakari, ni muhimu Bunge hili tukufu likaelewa kwamba aliyekuwa mshirika muhimu wa Agrisol IOWA State University College of Agriculture aliyekuwa mhimili muhimu wa mwekezaji huyu hasa katika kuwasaidia wakulima wadogo wadogo kama ilivyoainishwa katika kipengele cha  4.7 cha MoU  baina Halmashauri ya  wilaya ya Mpanda  na AGRISOL ENERGY TANZANIA LIMITED alijitoa baada ya kugundua kwamba mwekezaji huyu hana dhamira ya kuisaidia nchi na wakulima wadogo zaidi ya kujinufaisha kibiashara.

Mheshimiwa Spika, kwa maelezo ya IOWA State University College of Agriculture, ilijitoa baada ya kugundua ilitumiwa na mmiliki wa AGRISOL  bwana Bruce Rastetter ili  aweze kupata uhalali wa kukubalika kirahisi kama mwekezaji mahiri! Ukweli ni kwamba nia ya mwekezaji huyu haikuwa kuisaidia nchi bali kuendeleza mashamba makubwa ya zao mojamoja,.. matumizi ya viwango vikubwa vya kemikali na pia kuomba mabadiliko katika kanuni za kitaifa za usalama wa kibiolojia ili mazao yenye viinitete yaweze kupandwa. 

Mheshimiwa Spika, madhara ya GMO ni makubwa sana, moja kubwa ni kufifisha kabisa matumizi ya mbegu za asili.  Mwekezaji akizitumia kwenye eneo lake, madhara yanasambaa pia kwa mashamba ya jirani, inajenga utegemezi wa wakulima kununua mbegu kutoka kwa wakulima wakubwa. Mbali na utegemezi wa mbegu, GMO zina madhara makubwa sana kiafya. Tafiti zimeonyesha kwamba nchi zilizoendelea ziko katika vita kali sana za kuzuia matumizi ya GMO lakini sisi tunayapokea makampuni makubwa kwa misamaha lukuki ya kodi, tukiamini tunaalika wawekezaji waje kuijenga nchi, kumbe wanakuja kutengeneza taifa la utegemezi na lenye maradhi lukuki.

Mheshimiwa Spika, ni muhimu ikaeleweka kwamba katika wilaya ya Mpanda ardhi ambayo iko wazi kwa matumizi ya binadamu (arable land) ni 19% tu ya eneo lote! Nyingine iliyobaki ni hifadhi za taifa:
i)                   18% hifadhi ya wanyama,
ii)                  59% hifadhi ya misitu
iii)                4% hifadhi ya maji.

Mheshimiwa Spika,badala ya kila kitu kuwategemea mabeberu, inawezekana kabisa  serikali ikawekeza katika eneo husika. Taarifa zinaonyesha kwamba AGRISOL walitarajia kuwekeza $100 milioni (shilingi bilioni 150) katika kipindi cha miaka 10, kwa matarajio ya kupata faida ya $272 milioni (shilingi bilioni 408) ndani ya mwaka mmoja baada ya uwekezaji huo kwa kulima hekta 200,000 tu za mahindi, kiasi ambacho  kinalingana kama sio kuzidi bajeti ya Wizara ya Kilimo!

Mheshimiwa Spika, kama Agrisol wangepata/watapata hadhi  ya mwekezaji wa kimkakati,(stratergic investor). Wangepata/watapata pia msamaha wa kodi ya shirika (corporate tax)  ambayo ni 30% ya shilingi bilioni 408 (ambayo ni bilioni 122)! Hivi kweli serikali makini, mbali ya kuwa na vivutio vya utalii  vilivyosheheni, na hivyo kuwa nchi ya nne ya uzalishaji wa dhahabu Afrika, nchi pekee yenye madini tofauti tofauti zaidi ya 15 na kwa upekee ni madini ya Tanzanite, tuna urani ya kutosha,  hivi karibuni tumegundua gesi yenye thamani ya  tsh trilioni 626.7, tuna tani milioni 86 za makaa ya mawe, tuna kila dalili ya kupata mafuta n.k inashindwa kuwekeza kwa faida ya nchi na wananchi wake? Tunawezaje kuokoa kizazi cha vijana waliogeuka wazururaji kwa sababu serikali yao haijawapa fursa?

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2011/2012, Kambi ya Upinzani ilielezea kwa kina matatizo sugu ya migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali  nchini ambayo imekithiri kufikia hatua ya uvunjifu wa amani kunakopelekea umwagaji damu  na wakati mwingine vifo kutokea. Mwaka mmoja umepita bado  hakuna hatua dhahiri zilizochukuliwa na serikali hususan kuhusu:-

i)                   Mgogoro wa ardhi unaowahusisha  wakulima wa kijiji cha Nzasa, ambapo  Wizara ya Maliasili na Utalii wanataka kuwaondoa  wananchi katika ardhi yao halali kwa madai kwamba wanaishi ndani ya hifadhi ya Msitu wa Kazimzumbwi.

ii)                 Mustakabali wa maeneo ya yaliyokuwa mashamba ya Ngano, Hanang  (Hanang Wheat Complex  (HWC) na Dakawa Ranch.

iii)               Tatizo la ukodishwaji wa mashamba unaofanywa na wawekezaji dhidi ya  wananchi wenyeji. Hususan shamba la mpunga la Mbarali na Kapunga, yote yakiwa wilaya ya Mbarali na  mwekezaji RAI group anayemiliki mashamba ya  Setchet, Murjala na Gidagamowd ambaye alikuwa anawakodisha  wananchi $10  kwa ekari.

Kambi ya Upinzani ina taarifa za kuendelea kwa ukodishaji wa mashamba unaofanywa na wawekezaji. Shamba la hekta 1 hukodishwa kwa shilingi laki moja mpaka laki moja na nusu  katika mashamba ya Kapunga na Mbarali.

Hoja ya Kambi ya Upinzani imethibitishwa pia na timu ya wataalam wa  Consolidated Holding Corporation (CHC) katika taarifa yao ya ufuatiliaji  wa mashamba  na viwanda vilivyobinafsishwa[1] ambayo inabainisha kwamba katika shamba la Mbarali Rice Farm mwekezaji analima sehemu ya shamba  na sehemu nyingine ya shamba   anakodisha kwa wananchi kwa utaratibu maalum.

iv)             Kambi ya Upinzani inataka kujua mustakabali wa kijiji cha Kapunga, kilichopo wilaya ya Mbarali ambacho kiliuzwa  kwa mwekezaji!  Mkataba wa mauzo  na Hati miliki ya shamba (certificate of title) zinaonyesha kuwa shamba  lina ukubwa  wa hekta 7,370. Wanakijiji wanadai  kuwa shamba linatakiwa  kuwa na ukubwa wa hekta 5,500 kulingana na barua ya maombi ya ardhi kutoka kwa NAFCO na muhtasari  wa mkutano wa kijiji ulioidhinisha  utoaji wa eneo husika.

v)                           Mashamba  ya Gawal na Warret yaliyopo Hanang yalitakiwa  kurejeshwa kwa wananchi lakini hayajarejeshwa.

vi)             Mgogoro wa ardhi baina ya Jeshi la Wananchi (JWTZ)  na wananchi wa Bukanga  na Buhare (Mgaranjab) Musoma Mjini.

vii)           Mgogoro unaohusu shamba namba 299 (iliyokuwa NARCO  Ranches) lenye ukubwa wa hekta 49,981. Halmashauri ya wilaya ya Mvomero. Mgogoro huu uliwahusisha vigogo wakubwa wastaafu wa Chama cha siasa na serikali.

viii)         Mgogoro  baina ya Simba Motors na wanakijiji  wa  Mapinga, kitongoji cha Undindivu, wilaya ya  Bagamoyo.

ix)              Mgogoro baina ya wakulima na wafugaji  wa jamii ya Wamasai katika  eneo la vijiji  vya Izava   (Chamwino) na Chitengo (Kongwa).

x)                Uvamizi wa  maeneo ya wazi Mkoa wa Dar es salaam; viwanja vingapi vimerejeshwa kwa matumizi ya umma?  Na  viwanja vingapi bado vipo  mikononi mwa wavamizi?


MATATIZO YA TATHMINI NA MALIPO YA FIDIA

Mheshimiwa Spika, imekuwa ni jambo la kawaida sana kwa zoezi la fidia kuendeshwa kihenyeji na pasipo kuzingatia sheria na taratibu tulizojiwekea! Na hata wananchi wakilalamika serikali inaendelea na miradi! Kambi ya Upinzani inataka majibu ya hoja zifuatazo ambazo licha ya kuzungumzwa katika bajeti ya 2011/12 bado serikali haijazipatia majibu:
a)  Hatma ya wanakijiji wa kijiji cha Mabwepande ambao  miaka mitano iliyopita serikali ilifanya tathmini na kuwaagiza wasifanye  maendeleo yoyote ili kupisha ujenzi wa chuo cha IFM. Pia baada ya mafuriko makubwa yaliyolikumbwa jiji la Dar es salaam maeneo yao yalichukuliwa na serikali kwa ajili ya kugawa viwanja kwa waathirika! Mpaka sasa hakuna fidia yoyote iliyolipwa!
b)  Hatma ya Wananchi wa Kigamboni.
c)   Hatma ya wananchi 1600 wa wilaya ya Mbarali waliotakiwa kuondoka kupisha upanuzi wa  mbuga ya Taifa ya Ruaha.

UTEKELEZAJI WA BAJETI 2011/12

Mheshimiwa Spika, mpango wa Taifa[2] umeainisha wazi kwamba, pamoja na mambo mengine  kufanikiwa kwake kunategemeana sana na mipango bora ya matumizi ya ardhi. Na chombo pekee cha kuweza kufanikisha hili ni  Wizara ya Ardhi kupitia taasisi yake ya Tume ya Taifa ya Mipango. Kati ya majukumu ya Tume ni:-
i)                   Kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji.
ii)                 Utekelezaji  wa Mpango wa Taifa  wa Matumizi ya Ardhi  kwa kutekeleza programu  za kilimo, mifugo na maji  kwa kushirikiana na  Wizara ya Mifugo, Maji na Kilimo.
iii)               Kusaidia  kupatikana kwa  ardhi kwa ajili ya utekelezaji wa KILIMO KWANZA.
iv)             Kufanya utafiti katika  masuala yanayohusiana na ardhi hasa katika maeneo yenye migogoro, uhamiaji mijini kutoka vijijini, ushirikishwaji  wananchi katika kuendeleza ardhi mijini, viwango vya matumizi ardhi mijini na vijijini.
v)               Kufuatilia  na kutathmini  mipango ya matumizi ya ardhi iliyokwisha andaliwa  na katika maeneo yenye  migogoro  sugu.

Mheshimiwa Spika, ni wazi kwamba majukumu yao yangekuwa yanachukuliwa kwa uzito unaostahili, leo tungekuwa hatuzungumzii hoja za migogoro ya ardhi ambayo kwa sasa ni tishio la amani ya nchi, bali mafanikio ya matumizi endelevu ya rasilimali kubwa ya ardhi tuliyobarikiwa na mwenyezi Mungu!

KUPUUZWA KWA MIRADI YA MAENDELEO
Mheshimiwa Spika, licha ya umuhimu na ukubwa wa majukumu yake, Wizara ya Ardhi ni kati ya wizara ambazo zinapewa fedha ndogo sana za kutekeleza miradi ya maendeleo! Na mbaya zaidi, licha ya ufinyu wa fedha, fedha zimekuwa hazipelekwi zote!
Mwaka wa fedha 2010/11 Wizara iliidhinishiwa  jumla ya shilingi 22,265,078,000/-  kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Hadi mwaka unaisha, wizara ilipokea jumla ya shilingi 4,673,383,000/- tu! Ambapo  fedha zilizotumika kutekeleza miradi ya maendeleo ni  shilingi 3,931,581,086/-  zilitumika kutekeleza miradi ya maendeleo! [3]
Hali kadhalika, katika mwaka wa fedha  2011/12, wizara  iliidhinishiwa jumla ya shilingi 22,010,437,000/ kwa ajili ya miradi ya maendeleo . Hadi Mei 2012, Wizara ilipokea shilingi 3,663,685,463.96/- tu kwa jili ya miradi ya maendeleo!

Mheshimiwa spika, uzembe wa aina hii hauwezi kuvumilika! Kambi ya Upinzani inaitaka serikali ilieleze Bunge lako tukufu, ni kwa nini kwa miaka miwili mfululizo fedha za maendeleo  zimekuwa hazitolewi kama zilivyopangwa! Sambamba na hilo, ni miradi mingapi imekwama kutokana na upungufu huo?

KUPUUZWA KWA MAELEKEZO YA WAZIRI MKUU
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia changamoto za kimapato zinazoikabili  Wizara ya Ardhi, serikali kupitia kauli ya Waziri Mkuu iliridhia kuipatia wizara  kibali cha kubakia na makusanyo yao asilimia 100. Naomba kumnukuu:
’Mheshimiwa  Naibu Spika,lakini nasema hivi, jana tukiwa kwenye Cabinet tumemuidhinishia huyu mama kwamba wewe mama ile fedha yote  ambayo utakuwa unakusanya kutokana na shughuli zako za ardhi  baki nayo yote, chukua yote ili ikusaidie  wewe katika uendeshaji wa wizara hiyo.Kwa hiyo tunatambua  changamoto alizonazo  na naamini tutamsaidia vizuri sana na najua ataweza’  Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, hadi Mei  2012 , Wizara ilikusanya  jumla ya shilingi bilioni 16. Kinyume na maelekezo ya Waziri Mkuu,  wizara ilipokea  kiasi cha bilioni 9.4 tu, sawa  na asilimia 59 ya kilichokusanywa! Kutokana na  upungufu huo wizara ilishindwa kuongeza gawio la fedha za retention  kwa Halmashauri  mpaka kufikia 30%  badala ya gawio la sasa la 20%! Kambi ya Upinzani inaitaka serikali itoe maelezo juu ya mustakabali wa kiasi cha retention ambacho bado hakijapelekwa Wizarani!

MATUMIZI YANAYOHITAJI MAELEZO

MISHAHARA

Mheshimiwa Spika, imekuwa ni utaratibu  wa Bunge lako tukufu kupitisha mafungu mbali  mbali kama yalivyoombwa na wizara na idara mbalimbali za serikali. Tafsiri ikiwa kila wizara au idara ya serikali ina ufahamu wa makadirio ya fedha ambazo ina tarajia kutumia katika fungu husika.  Kwa miaka miwili mfululizo wizara ya ardhi imekuwa ikitumia fungu la mshahara kuliko kiasi kilichoidhinishwa na Bunge.

Katika mwaka wa fedha 2010/11,  wizara iliidhinishiwa  jumla ya shilingi 6,423,295,000/- kwa ajili ya  mishahara. Lakini  katika kipindi  cha Julai 2010 hadi Mei 2011 kiasi cha shilingi 8,499,539,334/-  zilitumika kulipa mishahara. Hali kadhalika  katika mwaka wa fedha 2011/12  wizara iliidhinishiwa  shilingi 7,531,409,000/- kwa ajili ya matumizi ya mishahara. Hadi Mei 2012  kiasi cha shilingi 9,765,774,300/- zilitumika kulipa mishahara! Kambi ya Upinzani inaitaka serikali itoe maelezo, hiyo tofauti  (ya zaidi ya shilingi bilioni mbili) ya kiasi kilichoidhinishwa na Bunge  na kiasi kilichotumiwa na wizara kwa miaka miwili mfululizo  imetokana na nini!

MIPAKA YA KIMATAIFA
Mheshimiwa Spika, Serikali ilikuwa katika mchakato wa kuandaa  andiko la kuomba eneo la nyongeza nje ya ukanda wa kiuchumi baharini . Andiko hili liliwasilishwa Umoja wa Mataifa  tarehe 18 Januari 2012. Kwa mwaka wa fedha 2010/11 na 2011/12   kiasi cha shilingi 431,572,872/- na 171,920,854.59/-  zilitumika kuandaa andiko husika! Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kutoa mchanganuo wa matumizi husika na kuainisha ni kwa namna gani ANDIKO limeweza kuigharimu serikali zaidi ya shilingi milioni mia sita!      

MASHAMBA YALIYOBINAFSISHWA AMBAYO HAYAJAENDELEZWA
Mheshimiwa Spika,  wakati akihitimisha bajeti ya ardhi mwaka jana, Waziri wa ardhi aliliahidi bunge lako tukufu kwamba baada ya bunge la bajeti  wizara ingekwenda kufanya ukaguzi huru wa nani ametelekeza mashamba. Alisisitiza kwamba wawekezaji wote waliotelekeza mashamba the honeymoon is over.[4]
Mheshimiwa  Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka kupata idadi ya mashamba  yaliyokaguliwa na wizara na mahali yalipo toka ahadi husika ilipotolewa  na ni hatua  gani ambazo zimeshachukuliwa na serikali dhidi ya wawekezaji husika.

Mheshimiwa Spika, wakati Kambi ya Upinzani ikisubiri taarifa toka kwa waziri wa ardhi juu ya ukaguzi huru iliyofanywa na wizara kuweza kuwabaini waliotelekeza mashamba, kambi ya upinzani inataka serikali itoe msimamo juu ya taarifa ya ufuatiliaji wa mashamba na viwanda   vya bidhaa na kilimo iliyofanyiwa kazi na CHC kufuatia maelekezo waliyopewa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC).

Taarifa husika imebainisha kwamba mashamba 13 yenye ukubwa  wa hekta 71,184  yalikuwa yameendelezwa kwa kiasi, wakati mashamba 14 yenye ukubwa wa hekta 44,764 yalikuwa hayajaendeleza kabisa/yametelekezwa! Mengi ya mashamba yakiwa ni mashamba ya Mkonge! Mashamba hayo ni:-

1)  Ndungu Sisal Estate, shamba hili lenye ukubwa wa hekta 1,230. 9 liliuzwa  kwa  L.M investiment  ya Tanga  mwaka 1997 kwa bei ya shilingi milioni 278 . Mpaka  sasa 2012,  miaka 15 baada ya kukabidhiwa shamba, mwekezaji  ameendeleza 52% tu ya shamba lote!
2)  Mkumbara Sisal Estate , shamba hili lenye ukubwa  wa hekta  1,734  liliuzwa mwaka  1997  kwa M/S D.D Ruhinda  & Company  LTD  kwa bei ya shilingi 100 milioni. Mpaka sasa  (miaka 15 baada ya kukabidhiwa shamba) mwekezaji  ameendeleza  52% tu ya shamba lote.

3)  Toronto Sisal Estate, shamba lenye ukubwa wa hekta 6,023 lililobinafsishwa kwa Highland Estate Limited kwa bei ya shilingi milioni 265.4 mwaka 1998. Mpaka Septemba 2011, ni 50% tu ya shamba lilikuwa limeendelezwa! Taarifa zilizopo ni kwamba mwekezaji husika hana hati miliki ya shamba kutokana na kudaiwa riba  hivyo kushindwa  kupata mkopo wa kuliendeleza shamba.

4)   Magunga Sisal Estate, shamba lipo wilaya ya Korogwe, lina ukubwa  wa hekta 6,520. Katika shamba hili ambalo linamilikiwa  kwa ubia na kuendeshwa  kwa kilimo cha mkataba  kati ya wakulima  wadogo  wa mkonge na Katani Limited limeendelezwa kwa  19% tu .

5)  Mgombezi Sisal Estate , shamba liko wilaya ya Korogwe  na lina ukubwa  wa hekta 6,480 ambapo hekta 3881 zimegawiwa kwa wakulima. Shamba linaendeshwa kwa kilimo cha mkataba  kati ya wakulima wakubwa na wa kati. Eneo lililopandwa mkonge ni hekta  1301.6 tu!

6)   Hale Mruazi Sisal Estate, shamba lina ukubwa wa hekta 4,180, ambapo hekta 1,136 tu  ndizo  zilizopandwa Mkonge.

7)   Manzabay Sisal Estate, shamba liliuzwa kwa Chavda Group mwaka 1998.  Mwekezaji alitumia hati miliki kupata mkopo ambapo hakutumia mkopo husika kuendeleza shamba, shamba husika lilishikiliwa na CRDB mpaka mwaka 2001 alipoiuzia Mbegu Technologies ambaye naye amelikodisha kwa Omari Mduduma. Shamba halijaendelezwa!

8)   Kwashemshi Sisal Estate, shamba lina ukubwa wa hetka  1498.5,shamba liliuzwa kwa Chavda Group mwaka 1998, mwekezaji alitumia hati miliki  ya shamba kupata mkopo, ambao hakuutumia  kuendeleza shamba. Shamba hilo lilishikiliwa na NBC mpaka 2003 lilipouzwa kwa Mathew Upanga Mnkande. Shamba limeendelezwa kwa 35% tu!

9)   Ubena Sisal Estate, shamba lenye ukubwa wa hekta  4,227 ambalo lipo wilaya ya Bagamoyo, mkoa wa Pwani   liliuzwa kwa Highlands  Estates Ltd  mwaka 2007 kwa kiasi cha shilingi  278 milioni. Jumla ya hekta 499 ambayo ni sawa na 12% tu imepandwa mkonge.

10)                      Kingolwila /Pangawe Sisal estate, shamba lenye ukubwa wa hekta 3703 liko wilaya ya Morogoro, mkoani morogoro, liliuzwa kwa Highland Estates limited kwa bei ya shilingi milioni 210.2 kupitia PSRC mwaka 2007. Jumla ya hekta 800 kati ya hekta 3703 ambazo ni sawa na 22% ya eneo lote ndio limepandwa mkonge!

11)                      Msowero Sisal Estate, Shamba lenye ukubwa wa  hekta 5200 lipo wilaya ya Kilosa Morogogo , shamba liliuzwa  na mamlaka ya Mkonge Tanzania kwa kampuni ya Noble Azania  Agricultural  Enterprises  mwaka 1993. Shamba limepandwa mkonge hekta 900 tu ambazo ni 17% ya shamba lote na alizeti  na mtama zimepandwa hekta 200 tu.  Hekta 4100 hazijaendelezwa toka mwaka 1993!

12)                      Rudewa Sisal estate, shamba lina ukubwa wa hekta 6351, liliuzwa kwa  kampuni ya  Farm land  mwaka 1992. Kampuni husika iliuza  shamba kwa kampuni ya China State Farms Agribusiness (Group) corporation  Tanzania Limited  (CSFACOT) kwa kiasi cha dola za kimarekani  milioni 1.2 mwaka  2000. Mwekezaji ameweza kuendeleza 32% tu kwa kupanda mkonge  hekta 2018 !

13)                      Kimamba Fibre Estate, shamba lenye ukubwa wa hekta 5743  liliuzwa kwa kampuni ya  ANCO ltd  mwaka 1998. Mwaka  2009 Kampuni ya ANCO  ltd iliuza hekta  3,043  kwa kampuni ya Sino  na kubakiwa na  hekta 2700.  Mustakabali wa shamba walilouziwa Sino haujulikani, ila  shamba lililobaki ANCO ltd limeendelezwa kwa 46.3% tu!

Mheshimiwa Spika, mashamba ambayo hayajaendelezwa kabisa ni:
1)     Kikulu Sisal estate  ,lenye ukubwa  wa hekta 5900 lililouzwa kwa Chavda Group, mwekezaji  alieka dhamana shamba,kama kawaida yake akachukua , mkopo hakuendeleza shamba.
2)     Kibaranga Sisal Estate lenye ukubwa wa hekta 6,900, liliuzwa kwa kampuni ya katani ltd, iliposhindwa  kuendeleza  serikali ililiweka chini ya PSRC na bodi ya Mkonge.

3)     Kwamngwe sisal estate,  lenye ukubwa  wa hekta 3700, liliuzwa kwa Chavda  Group mwaka 1998, alichukua mkopo, hakuendeleza shamba.

4)     Kwafungo Sisal Estate, lenye ukubwa wa hekta 2310, liliuzwa kwa Chavda Group mwaka 1998, mwekezaji alitumia hatimiliki ya  shamba kuchukua mkopo, ambapo hakutumia kwa kusudi la kuendeleza shamba. Shamba hilo bado linashikiliwa na CRDB.

5)     Bombuera Sisal Estate, lenye ukubwa wa hekta 2370, lipo Korogwe, liliuzwa kwa Chavda Group mwaka 1998. Mwekezaji alitumia hatimiliki ya shamba kupata mkopo. Hakuliendeleza shamba. Mwaka 2002 CRDB iliuza shamba kwa AMC Arusha Ltd.

6)     Hale Mwakiyumbi Sisal Estate, lenye ukubwa wa hekta 4,309. Shamba liliuzwa kwa Chavda Group, 1998. Alitumia hatimiliki  kupata mkopo ambao hakuutumia kwa kusudi lakuendeleza shamba na kulitekeleza. Shamba linashikiliwa na CRDB.

7)     Allidina Sisal estate, lenye ukubwa  wa hekta 2300, liliuzwa kwa Noble Azania Agriculture  Enterprises mwaka 1993. hakuna uwekezaji wowote uliofanyika!

8)     Msowero (Godes) Farm, lenye ukubwa wa hekta 5,000. lilikuwa linasimamiwa  na wizara ya Kilimo chini ya Tanzania Livestock  research organization  (TALIRO) Mwaka 1993 serikali ya CCM ilipanga kujenga  chuo cha mifugo. Mpango ambao haukukamilika ,shamba likabaki bila usimamizi wowote.

9)     Rutindi Sisal estate,lina ukubwa wa hekta  1,087. Shamba  liko Morogoro,  linamilikiwa na kampuni ya Noble Azania Agricultural Enterprises. Shamba halijaendelezwa na mwekezaji toka amelinunua.

10)                      Magole Sisal Estate, lina ukubwa wa hekta 1,149. Lipo Dumira, kilometa 65 toka  Kilosa. Lilikuwa la serikali chini ya mamlaka ya mkonge  Tanzania. Japo halijabinafsishwa liko katika hali mbaya.

11)                      Mauze Sisal Estate , lina ukubwa wa hekta  2,842.5. Shamba lilikuwa na deni la shilingi milioni 1.36 kutoka benki ya NBC. Benki ilishikilia Hati miliki  na kuliweka chini ya  ufilisi wa LART kutokana na kuongezeka kwa deni mpaka milioni 10.  Kwa sasa kuna  vijiji vya Kilangali na Mabwembele  vilivyoanzishwa  na vimesajiliwa  ndani ya shamba. Halmashauri za vijiji hivyo  zinakodisha maeneo katika shamba hilo kwa wanavijiji na watu kutoka  nje ya vijiji kwa gharama  ya shilingi  3,000 kwa ekari moja!

12)                      Myombo na Kilosa  Sisal estate. Mashamba haya yenye ukubwa wa  hekta 2,024 (Kilosa)  na 1843  (Miyombo). Mashamba  yalibinafsishwa na mamlaka ya Mkonge  kwa Kampuni ya Katani mwaka 1998. Baada ya kampuni ya Katani Limited  kushindwa  kuyaendesha ,iliyakodiha  kwa kampuni  ya Agro-Focus. Mwaka 2005  Baraza la Mawaziri liliagiza  kuwa mashamba haya  yatafutiwe mwekezaji  mwenye uwezo  kwani kampuni  ya Agro- focus LTD  imeshindwa kuyaendeleza. Hata hivyo, kinyume na maagizo  mwaka 2009 Bodi ya Mkonge  iliyauza mashamba haya kwa Agro-Focus. Matokeo yake mpaka sasa hakuna uwekezaji wowote uliofanywa. Sehemu kubwa ya shamba ni pori na  sehemu iliyobaki  imekodishwa  kwa wananchi kwa ajili ya  kulima mahindi.

13)                      Madoto  sisal estate, shamba lina ukubwa wa hekta  3,200. Shamba lilinunuliwa na kampuni ya SUMAGRO Ltd ambayo nayo ililiuza kwa East African Breweries mnamo mwaka 2009.  Hakuna uwekezaji wowote uliofanyika !

14)                      Kivungu  Sisal Estate, shamba lina ukubwa wa  hekta 2,200. Shamba lilinunuliwa na  kampuni ya  SUMAGRO Ltd.  Mwaka 1998, ililiuza kwa  East African  Brewaries mwaka 2009. Hakuna uwekezaji wowote uliofanyika!

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kuyarejesha mashamba yote ambayo wawekezaji wameshindwa kuyaendeleza, kama ambavyo taarifa hii imevyoainisha. Hali kadhalika kwa wale wawekezaji ambao wameweza kuendeleza sehemu ndogo na hawana uwezo wa kuendeleleza shamba zima warejeshe sehemu ya mashamba waliyoshindwa kuendeleza ili wapewe wananchi wenye uhitaji!

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapendekeza serikali iangalie hatua za kuchukua dhidi ya wawekezaji katika mashamba 13 ambao wafuatao wameshindwa kuendeleza mashamba kwa 100%. Pamoja na wawekezaji katika mashamba 14 ambao wameshindwa kabisa kuendeleza mashamba waliyonunua, kama ambavyo yameorodheshwa hapo juu.

Mheshimiwa Spika, kwa tathmini hii fupi iliyofanywa na CHC utaona ni kwa namna gani zoezi la ubinafsishwaji mashamba lilifanywa kiholela na kwa hujuma, pasipo kuzingatia maslahi ya umma. Katika hali ya kawaida , watu wote walioshiriki katika zoezi hilo wana kila sababu  ya kuchukuliwa hatua, hakika hawana tofauti na wahujumu uchumi.  Kwa mfano huyu  ’mwekezaji’ anayejiita Chavda Group,  aliuziwa  shamba kwa bei ya kutupa mashamba  saba, yenye ukubwa wa hekta  25,000, katika maeneo tofauti ya nchi hii. Kikubwa alichokifanya ni kutumia hati za shamba kuchukulia mikopo, kisha kutelekeza mashamba!! Hivi kweli unahitaji kuwa na akili nyingi kuyaona haya?  Nyuma ya Chavda Group wako akina nani?

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe ni familia hii hii ya Chavda ( V.G Chavda na kaka yake P.G Chavda),[5] waliojitwalia mkopo wa  $ 3.5m mwaka 1993   chini ya DCP (Debt Conversion Program) wakiahidi kufufua  mashamba ya mkonge Tanga ndani ya miaka 10, na kupata $42 milioni.  Walipopata hayo mapesa, hawakufanya lolote, na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi yao! Mheshimiwa  Spika, kwa utaratibu huu, lazima tuwachukulie wawekezaji wa aina hii kama ni ’waporaji’ na hawana tofauti na majambazi yanayoiba benki kwa kutumia nguvu!

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali, kupitia Wizara ya Ardhi yenye jukumu pana la kusimamia sekta ya ardhi kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo hayajaendelezwa na wawekezaji yanarejeshwa serikalini bure bila fidia kwa ajili ya kutafuta wawekezaji wengine wenye mtaji wa kutosha watakaoyaendeleza  mashamba hayo.

Hali kadhalika, kwa yale mashamba ambayo tayari yana wakulima wadogo wadogo wanaoendesha shughuli zao za kilimo, serikali ipange utaratibu wa kuwamilikisha wananchi maeneo husika, ili kuondokana na ile dhana ya ’uvamizi’ au kukodishwa ardhi kwa ajili ya kilimo. Zoezi hili lazima lifanywe kwa uwazi ili kuepuka udanganyifu uliotokea  katika maeneo mengine ya nchi  ambapo vigogo na watu wenye nafasi  zao walijitwalia ardhi wakijifanya na wao ni sehemu ya wanakijiji!

MASHAMBA YALIYOPENDEKEZWA KURUDISHWA  KWA WANANCHI  MKOA WA ARUSHA
Mheshimiwa Spika, tarehe 17/6/1997  aliyekuwa Mkuu wa mkoa  wa Arusha, Ndugu  D. Ole  Njoolay aliitisha kikao  kilichohudhuriwa na Ndugu Kileo – katibu tawala  Mkoa, Ndugu  P.H Muhale- Afisa Maendeleo ya ardhi (M), ndugu E. K. E Makere – Afisa Ardhi na Ndugu Z.M.S  Meirish – Afisa Ardhi. Kikao husika kilichofanyika  saa 4.35 asubuhi  kilikuwa mahsusi  kwa kuchambua mapendekezo yaliyoletwa  kutoka wilayani kuhusu  taarifa za mashamba makubwa  mkoani Arusha.

Mheshimiwa Spika, mashamba yaliyojadiliwa na kufikia maamuuzi mbali mbali yalihusisha wilaya sita:
a)   wilaya ya Arumeru-  Mashamba 18
b)   wilaya ya Ngoro Ngoro- Mashamba 10
c)   wilaya ya Babati – Mashamba 11
d)   wilaya ya Simanjiro – Mashamba 2
e)   wilaya  ya karatu –Mashamba 6
f)      wilaya ya Monduli – Mashamba 36
(Nakala ya Majina ya Mashamba pamoja na hatua zilizopendekezwa nimeziambatanisha kama sehemu ya hotuba hii). Kambi ya upinzani inaitaka serikali kulieleza Bunge hili tukufu nini mustakabali wa mashamba 83, na hatua zilizochukuliwa kufuatia kikao husika.

Mheshimiwa Spika, mwaka 1999, ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, kupitia barua yenye kumb. Na. RC/AR/ CL 2/3 Vol IV/19 ilimwandikia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Arumeru ikimtaarifu juu ya mashamba 11 ambayo yamepata kibali cha Rais kufuta miliki. Taarifa ambayo ofisi ya mkuu wa mkoa ilipata toka kwa  Katibu Mkuu  wa Wizara ya Ardhi  kwa barua yenye kumbu kumbu namba  CL/46/VOL III  ya tarehe  1 Juni 1999 .
Mashamba hayo:
1)   Shamba namba 78 na 79 - NAIC , Usa River
2)   Shamba namba 90 na 91-  Madiira Coffee ltd
3)   Shamba namba  98/2/1 – Duluti New – Duluti Lodge
4)   Shamba namba 218/2- Maua limited
5)   Shamba  la Oljoro – Salama estate
6)   Shamba la Unit 15  Oljoro – Iman estate
7)   Karangai Sugar Estate ( Tanzania Plantaion)
8)   Shamba Namba 3 – Milimani pharmacy
9)   Shamba  la Nduruma- Lucy estate
10)                      Shamba la Nduruma – Umoja Sisal Estate
11)                      Shamba la DOLLY – DOLLY ESTATE- FLYCATCHERS    (ambalo limegeuzwa uwanja wa Gofu na shamba la wanyama  kinyume na maagizo ya Rais)

Kambi ya upinzani, inaitaka serikali itupe maelezo ya kina  kuhusu mashamba haya!

MIGOGORO YA ARDHI
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tulifanya katika mwaka wa fedha 2011/12, Kambi ya Upinzani itakuwa na utaratibu wa kila mwaka wa fedha kuianishia serikali migogoro mbali mbali ya ardhi inayolikumba taifa letu! Ni jukumu la Serikali kupitia vyombo vyake kuhakikisha kwamba inafuatilia migogoro hii kwa kina na hatimaye kuyatafutia ufumbuzi: 

BAGAMOYO- MKOA WA PWANI
Mheshimiwa Spika, wananchi wa kijiji cha Milo chenye vitongoji vitano:- Milo, Relini, Kengeni, Kisiwani na Migude, kilichoandikishwa chini ya sheria ya kijiji (chenye shule ya msingi na zahanati na kijiji) wanailalamikia Kampuni ya Noble-Azania Agricultural Enterprises Limited ambayo inadai ni wamiliki halali wa eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 3000. Eneo ambalo limekimeza kitongoji cha migude na sehemu ya kijiji cha milo. Kwa upande mwingine, Kampuni ya Azania, inadai wanakijiji hao ni wavamizi kwa kuwa wao wana umiliki halali wa eneo husika kupitia umiliki namba 36911.

WILAYA  YA MPANDA – KATAVI
Mheshimiwa Spika, mkoa mpya wa Katavi, anakotoka Waziri Mkuu, ni kati ya maeneo yenye migogoro mingi sana ya ardhi, mingi ikiwa ni migogoro sugu, ambayo imeshindwa kutafutiwa ufumbuzi licha ya malalamiko kufika ngazi za juu  serikalini pamoja na kamati ya ulinzi  na usalama  ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Migogoro  inazihusu kata za Kabwe na Korogwe, kijiji cha Nkungwi[6], kijiji cha Kabange, Kijiji cha Mbuguni,  mgogoro baina ya hifadhi ya Ubende na vijiji kumi na nane.

Mheshimiwa Spika, nitawasilisha mezani kwako nyaraka mbali mbali za migogoro hii, kama serikali itaona inafaaa, iyafanyie kazi!

Mheshimiwa Spika, kutokana na muda, nitaelezea mgogoro mmoja sugu, ambao unahusisha watendaji serikalini. Mgogoro  ambao unaambatana na vitisho kwa wananchi, mpaka kufikia hatua wananchi kufunguliwa kesi za jinai[7] ili kuwatisha.  Wananchi wa Kata ya Sibwesa, wilaya ya Mpanda wanalalamikia mtandao ambao umeundwa na watumishi wa serikali, ambao ni waajiriwa wa  Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, wanaofahamika kama Cletus Siwezi, Andrea Malando (Kitengo cha Ardhi) na Bwana Galus Kasonso (Meneja wa mradi wa maji  katika Halmashauri ya Mpanda ).

Mheshimiwa Spika, watumishi hawa wanalalamikiwa na wananchi, wakituhumiwa kuwanyang’anya mashamba yao  kwa kutumia nafasi zao.

Mheshimiwa Spika, mtumishi huyu wa Serikali (kupitia kwa bwana Ramadhani), alishindwa kuthibitisha umiliki wake katika baraza la ardhi la Kata, walikimbilia Baraza la Ardhi na Nyumba la Sumbawanga ambapo ilitolewa hukumu ya upande mmoja! Baada ya hukumu hiyo ya upande mmoja kumekuwa na hujuma dhidi ya wananchi na kuna malalamiko kwamba kuna mbinu ya kuandikwa hati ya kukamata heka  mia tatu  na sitini (360) kutoka mbuga ya Mwamapuli,  kijiji cha Kabage na mbinu yake ya kuendelea kufanya mipango  ya kukamata watu  bila ya kuwa na kosa kwa kutambua kuwa hawana uwezo  wa kukabiliana na kesi za jinai. Jeshi la polisi linahusishwa pia katika mazingira mawili, la kwanza kufungua kesi za kubambikiza, hali kadhalika kumlinda mhalifu!

Mheshimiwa Spika, yanayotokea Mpanda, yanafanyika pia kwenye maeneo mengi ya nchi hii, kwa watu ambao wamepewa dhamana kutoa huduma hii muhimu kwa wananchi, kutumia fursa hiyo kujilimbikizia ardhi, na pale ambapo wananchi wa kawaida wenye  uhitaji wa huduma hiyo kukumbana na urasimu mkubwa uliotawaliwa na rushwa!

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali ijipime kwa kuangalia ni hatua gani stahili itawachukuliwa watumishi hao wa halmashauri kama ushahidi ulivyotolewa, na pengine inaweza pia kubaini mambo mengi mazito yaliyojificha!
MKOA WA MANYARA- BABATI
Mheshimiwa Spika, mgogoro huu  unahusu hifadhi ya Taifa Tarangire na Vijiji vya Gijedabung,  Ayamango[8] na Gedamar[9]. Mheshimiwa Spika, vijiji hivi  vilikaliwa na wananchi toka miaka ya 1960. Hifadhi ya Tarangire ilianzishwa mwaka 1970 kwa kuzingatia tangazo la Serikali (GN) Na. 160. Mipaka yake ilitambulishwa  kwa barabara  iliyozunguka  hifadhi nzima na kuipatia umbo linaloonekana  katikati yake kupitia  Sheria ya mwaka 1974 ya Vijiji na Vijiji vya ujamaa, mpaka ambao wananchi wote waliutambua na kuuheshimu.

Mheshimiwa Spika, mgogoro  ulianza baada ya uongozi  wa hifadhi   ya Tarangire ulipotekeleza  zoezi lake la kuhakiki mipaka yake kwa nia ya kufanya tafsiri yakinifu kwa kutumia vifaa vya kisasa. Wataalam walibaini kwamba ule mpaka wa miaka yote wa barabara, ulioliwekwa na Mamlaka ya Hifadhi yenyewe haukuzingatia vipimo halisi na hivyo kusababisha  eneo lenye ukubwa wa  ekari 16,249.10325 kuingizwa kwenye mamlaka ya vijiji kimakosa. Kwa mantiki hiyo hifadhi iliamuru  wananchi waliokuwa  wakiishi kwenye ardhi hiyo  kuhama mara moja  na kusitisha matumizi  yote juu  ya ardhi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kutokana na amri hiyo, wananchi wengi wa maeneo haya wako katika hali mbaya sana kiuchumi kutokana na ardhi waliyokuwa wanaitegemea kuchukuliwa na serikali!  Wananchi  wamezuiwa kufanya kitendo chochote cha kufanyia matengenezo makazi yao walioishi kwa zaidi ya miaka 50. Ikumbukwe kwamba wananchi hawa hawakuvamia eneo hili bali waliwekwa na mamlaka ya wilaya kwa makosa pasipo kukusudia. Pamoja na serikali kutaka kuwahamisha wananchi hao haijafanikiwa kuwapatia  makazi mapya na mashamba ya kulima.

Mheshimiwa Spika,usumbufu wa Askari  wa Hifadhi  ya Tarangire wanaofanya vitendo vya unyanyasaji  ni kero kubwa  kwa usalama,  utulivu  na ustawi  wa wananchi wa maeneo husika. Kambi ya upinzani haidhani kwamba hifadhi  ni muhimu zaidi kuliko watanzania waliokiweka CCM madarakani.  Ni rai yangu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano awatazame wananchi wa maeneo haya kwa jicho la huruma!  Awatazame wananchi wa maeneo haya kwa jicho la huruma kutokana na kwamba hawana maeneo mbadala ya kuishi ili kuendeleza maisha yao!  Rais wa Jamhuri ya Muungano ana mamlaka ya kuhawilisha  ardhi ya Hifadhi  ya Taifa ya Tarangire inayokaliwa na wananchi wa vijiji tajwa  ili iwe ardhi  ya kijiji, ombi ambalo lilisha wasilishwa Wizara ya Ardhi Nyumba na Makazi, lakini mpaka leo hakuna majibu!


MKOA WA KAGERA- wilaya ya Karagwe
Mheshimiwa Spika,  muda sasa Kambi ya Upinzani, pamoja na wabunge wengi, wamekuwa wakizungumzia juu ya mgogoro baina ya wakulima na wafugaji, kutokana na serikali kutokuwa na mpango endelevu wa kutenga maeneo ya wakulima na wafugaji. Mwaka jana katika hotuba ya Kambi,  tulielezea juu ya mgogoro wa wakulima na wafugaji wa jamii ya Wamasai  katika eneo  la vijiji vya Izava (Chamwino) na Chitego (Kongwa). Mgogoro huu mpaka leo  hujapatiwa ufumbuzi. Kimsingi mgogoro ulisababishwa na ubabe na maamuzi mabovu ya mkuu wa wilaya. Katika hotuba hii, Kambi ya Upinzani inafikisha mbele ya Bunge lako Tukufu kilio cha wanavitongoji  vya Karugwebe, kijiji cha ITEERA  na kitongoji cha MTAKUJA  kijiji cha  CHANYA, Karagwe.

Mheshimiwa Spika, wananchi wanalalamikia kufukuzwa kwenye maeneo yao ya kilimo na kupewa wafugaji matajiri  bila wao kuhusishwa! Baada ya kufukuzwa hawakupewa hifadhi, kitu ambacho kimewafanya wawe wahamiaji wasio rasmi ndani ya nchi yao! Ikumbukwe wananchi hawa walikuwa wanafanya shughuli za kilimo kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20. Madiwani walipohoji katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika ntarehe 31/2/12, walipata vitisho kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Misenyi  aliyekuwa anakaimu ukuu wa wilaya ya Karagwe!

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka kauli ya serikali kuhusiana na matukio haya mawili; hali kadhalika serikali ilitaarifu Bunge lako tukufu, ni lini Serikali itaandaa mpango rasmi wa matumizi ya ardhi kwa wakulima na wafugaji ili kuepuka migogoro isiyokwisha!

MKOA WA DAR- ES- SALAAM
Maeneo ya Pembezoni
Mheshimiwa Spika, miaka ya hivi karibuni serikali imekuwa na mikakati, inayoitafsiri kama mikakati kabambe ya kuendeleza maeneo yaliyomo pembezoni mwa jiji la Dar es salaam. Mipango hiyo imeleta msiba mkubwa sana kwa wananchi wa maeneo hayo! Kwa sababu ya muda, tutazungumzia miradi ya Luguruni na Kwembe Kati, Kinondoni Dar es salaam.

Mheshimiwa Spika, katika maeneo haya, wananchi wameporwa ardhi yao yote  kwa fidia ndogo sana, wamebomolewa makazi yao  na kutimuliwa kutoka  kwenye ardhi yao   kwa nguvu ya dola, wakiwa wamemaskinishwa kupindukia  baada ya kuporwa  rasilimali ardhi yao, na wakiwa na fidia duni  mkononi, wakihamia kwingineko  kuanzisha  makazi yasiyopimwa na ya kimasikini kupindukia!
Miradi hiyo imegubikwa  na utendaji wenye kupindisha sheria, ubabe, usio na utawala bora, ulioteteresha  viwango vya ramani  na upimaji uliochakachua fidia, uliofanya ofa  na hatimiliki kuwa uyoga, uliojaa dhuluma  na hujuma dhidi ya hakiardhi ya wananchi.

Hapo Luguruni tarehe 22/5/2007 Mkurugenzi  wa Makazi  na Ardhi alitangaza  utwaaji wa ardhi  wa 5% ya Ardhi kwa ajili ya miundombinu. Hali hii  ilibadilika kufikia 100% na waliofanya hivyo ni watendaji wa mradi baada ya mkurugenzi husika kustaafu.

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika kinachofanyika  Kwembe  Kati,  kwa maeneo ya miundombinu, biashara na makazi  yalitwaliwa  na Mradi na kutangazwa kuwa mali ya serikali,  licha ya tamko  la Waziri wa Ardhi Mhe. Chiligati Bungeni la tarehe 18/06/2009 na tamko la Naibu Waziri wa Ardhi Mhe. Goodluck Olemedeye  Bungeni tarehe  12/11/2011 kusisitiza ya kwamba  baada ya Rais  kutwaa ardhi na Miundombinu albaki ya ardhi kwa ajili  ya makazi na biashara  ibakie  mikononi mwa wananchi  wamiliki wa ardhi, waiendeleze  wao wenyewe ili waweze kujikomboa kiuchumi.

Katika maeneo yote hayo, baada ya ardhi yote ya wananchi kutwaliwa kwa fidia duni chini ya 20% ya bei ya soko kinyume hata na matakwa ya sheria ya ardhi, namba 4 ya mwaka 1999, sehemu ya II, kifungu cha 3 kinachoelezea misingi mikuu ya sera ya ardhi ya Taifa, wananchi walitimuliwa kimabavu  baada ya makazi  yao kubomolewa kwa tingatinga. Mfano dhahiri ni wa eneo la Luguruni;  fidia iliyolipwa kwa mita moja ya mraba  ilikuwa ni shilingi 1,977, ardhi hiyo hiyo  iliuzwa kwa tshs 30,000 mita moja ya mraba  bila maendelezo yoyote! Hivyo kuzalisha faida ya 1500% …Huu ni wizi na unyonyaji mkubwa.

Mheshimiwa Spika, inasikitisha sana pale  watendaji wa wizara ya Ardhi, wanapotumia  mgongo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania kutengua  toleo la hatimiliki halali za wananchi  wamiliki wa ardhi, kupora ardhi yao  kwa mtindo huu, kupima  viwanja  vipya  juu ya viwanja vya awali.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka serikali hii ya CCM, kuacha kufanya mambo kibabe, na kusitisha kile kinachoendelea katika maeneo ya Luguruni na Kwembe Kati. Ulipaji fidia  unakuwa na mianya  lukuki  ya ubadhirifu  wa fedha,  hivyo kuhitaji  ukaguzi na udhibiti  wa makini sana   wa masuala  yote ya malipo  na matumizi  ya fedha kwenye  miradi ya Luguruni  na Kwembe Kati. Viwango vya fedha  vinavyohusika hapa ni vikubwa  sana kutokana na wingi  wa watu wanaohitaji kufidiwa  na kutokana na mauzo ya viwanja vilivyopatikana katika mchakato mzima  wa kutwaa  na kuuza ardhi,  kuna uhitaji mkubwa  wa ukaguzi na udhibiti mahsusi  wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu.
Suala la ukaguzi ni muhimu kutokana  na tuhuma kwamba malipo ya fidia  yamefanywa  bila kutumia nyaraka halali  za  matayarisho  na ulipaji fedha .

Tatizo la Uvamizi wa Maeneo ya watu
Mheshimiwa Spika, kuna tabia iliyozuka kwa kasi sana, katika manispaa ya Kinondoni, hususan maeneo ya pembezoni, na katika jimbo la Kawe; ninaloliwakilisha tabia hii imekithiri sana kata za Bunju, Mabwepande na Wazo. Kumekuwa na genge la watu wenye silaha  wanaovamia maeneo ya watu, kuharibu mali, kugawa viwanja na kuwauzia watu (wapya) viwanja kwa bei ya kutupa . Hilo genge, baada kufanya uharibifu eneo moja, huhamia eneo lingine!  Hali  hii  imesababisha uvunjifu wa amani, na katika mazingira mengine kusababisha vifo!

Mheshimiwa Spika, hofu ya wananchi inaongezeka kutokana na kutokupata ushirikiano kutoka kwa mamlaka zenye jukumu la kuhakikisha wananchi na mali zao wako katika hali ya usalama. Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na Mkoa wa Dar es salaam  zote zina taarifa  ya genge hili la majambazi wa ardhi, vyombo mbalimbali vya habari vimetoa taarifa kuhusu genge hili la majambazi, hakuna hatua  zilizochukuliwa na wala hakuna dalili kama kuna dhamira ya dhati ya kuweza kutafuta suluhu!

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba serikali ingejipanga katika matumizi bora ya ardhi na kuhakikisha kwamba  Watanzania wanapata ardhi kwa gharama nafuu bila urasimu walarushwa, hili  genge la majambazi wa ardhi lisingepata wateja!

Kambi ya Upinzani inaitaka serikali ieleze Bunge ina mipango gani ya muda mfupi na mrefu kuweza kukomesha kabisa suala la uvamizi wa maeneo ya wazi! Nikiwa mbunge wa Kawe, napenda kuwasisitizia wamiliki wote wa ardhi Jimbo la Kawe, serikali ya wilaya kupitia kamati yake ya ulinzi na usalama imeshindwa kuwapa ulinzi wenu na mali zetu. Niendelee kuwashawishi kila mmoja kwa nafasi yake mmoja mmoja au kwa vikundi kuweka walinzi binafsi kwa ajili ya kulinda mali zao! Na chochote kikitokea mbunge wenu nitawalinda kwa sababu nilishatoa taarifa kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa mpaka serikali kuu!

Majiji ya Viungani  (setelite towns)
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2006/07 Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikishirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam na Manispaa zake tatu ilianzisha Mkakati wa kuanzisha miji midogo sita itakayokuwa na vituo vya huduma za kijamii na za kibiashara. Kutokana na ukubwa wa mpango huo iliamuliwa kuwa utekelezaji uanze katika eneo la Kibamba Luguruni ambalo lilipaswa kuwa eneo la mfano ambapo uzoefu katika uendelezaji ungetumika kwa maeneo mengine ya Jiji na nchi nzima kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, Uanzishwaji wa Mji wa Kibamba uligawanywa katika maeneo makubwa matatu: Eneo Kitovu cha Mji cha Luguruni, eneo la makazi mbadala la Kwembe Kati na uendelezaji wa eneo linalozunguka kituo. Hata hivyo miaka zaidi ya mitano imepita bila uendelezaji huo kukamilika na hivyo sehemu kubwa ya maeneo tajwa kurejea kuwa mapori na kuanza kurejea kwa migogoro ya ardhi katika maeneo tajwa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza matokeo ya tathmini ya utekelezaji wa mpango huo na kueleza bayana kasoro na matatizo yaliyojitokeza sambamba na kuharakisha ujenzi wa mji husika ili kuwa mfano kwa mipango ya ujenzi wa miji mingine ambayo maandalizi yake yanaelezwa kutaka kufanyika katika mwaka wa fedha 2012/2013.

Mheshimiwa Spika, wakati zoezi la  wa Luguruni, Kwembe Kati na Kigamboni yakitawaliwa  na malalamiko makubwa  sana kutoka kwa wananchi, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi imeandaa mpango mpya  wa Makongo.  Mradi huu utasimamiwa na mtendaji aliyeendesha zoezi la kihuni la ujenzi mpya wa mji wa Kigamboni!
Kambi ya Upinzani inaona mradi huo umeanza vibaya kwani msimamizi wake mkuu haaminiki kutokana na miradi aliyoisimamia huko nyuma. Hivyo basi inaitaka Serikali ikutane  na wananchi  na majirani zake wa Makongo tulijadili hili kwa kina! Kutumia mabavu hakutasaidia! Wananchi wa makongo wanataka maendeleo, lakini yasiwe maendeleo yenye lengo la kuwapa mzigo, ufukara na kuwahamisha wale ambao hawatakuwa na uwezo wa kukidhi matakwa ya mradi! Nasisitiza mimi ni mbunge wako, njoo tuzungumze!

UWINDAJI, UFISADI NA  UKIUKWAJI WA SHERIA  ZA MATUMIZI YA ARDHI
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa Ardhi ya Tanzania imegeuzwa shamba la bibi na kikundi cha mafisadi! Kambi ya Upinzani imeshuhudia mkataba ulioingiwa baina  ya kampuni  za Uranium  resourses  PLC, Western Metals Limited  na Game Frontiers  of Tanzania Limited. Mkataba ambao umetengenezwa na Kampuni ya Kitanzania ya REX ATTORNEYS. Na ulisainiwa tarehe 23.3.2007.

Mheshimiwa Spika, mkataba husika,ambao vipengele vyake vinaainisha kwamba unatakiwa uwe wa SIRI unaihusu kampuni ya uwindaji, inayofahamika kwa jina la Game Frontiers  of Tanzania Limited  inayomilikiwa na Bwana Mohsin M. Abdallah  na ndugu Nargis M. Abdallah.   Kampuni hii ya uwindaji, imeingia mkataba na kampuni mbili za kigeni, za kufanya utafiti wa uchimbaji wa madini ya Uranium katika kijiji cha Mbarang’andu kwa malipo yafuatayo:-

a)   Malipo ya $ 6,000,000/- za kimarekani, ambazo zitalipwa kwa awamu mbili ya malipo ya $3,000,000. Malipo ya kwanza yatafanyika pale uzalishaji wa urani utakapoanza.

b)   Malipo ya $ 250,000/- baada ya kampuni za madini kukamilisha utafiti wa madini ya urani na kupata kibali cha uchimbaji wa madini.

c)    Malipo ya $ 55,000 kila mwaka kama fidia ya kushindwa kufanya biashara na usumbufu unaotokana na shughuli za machimbo kwenye kitalu! Malipo hayo yatafanyika kila tarehe 31 Machi.

d)    Malipo ya $ 10,000 kwa vijiji vitakavyoathiriwa na utafiti huo wa urani. Malipo ambayo yametokana na makubaliano baina ya kampuni ya uwindaji na kampuni za madini!

Mheshimiwa spika, nimepitia sheria za uhifadhi wa wanyamapori, The wildlife Conservation Act, 1974 (Sheria ya zamani) na Sheria mpya The wildlife Conservation Act, Act no 5 of 2009. Sheria hizi zinamruhusu mtu aliye na leseni ya uwindaji, kuwinda wanyama tu!

Mheshimiwa spika, hali kadhalika, Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999, Sheria namba 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya Ardhi ya vijiji, sheria namba 5 ya mwaka 1999 inatamka bayana kwamba ardhi inajumuisha vitu vyote vilivyo juu ya ardhi na chini ya ardhi isipokuwa madini au mafuta……… Na kwa mujibu wa sheria za Tanzania linapokuja suala la madini, umiliki unatoka kwa mtu binafsi na kurudi serikalini! Na ni Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini ndiyo pekee yenye mamlaka ya kutoa leseni ya kutafuta madini kwa kampuni za madini!

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali ilieleze Bunge lako tukufu uhalali wa mkataba kati ya Game Frontiers na Uranium Resourses PLC na Western Metals! Ni sheria ipi inayoipa kampuni ya uwindaji haki ya kualika kampuni ya nje kwenye eneo ambalo haina umiliki kufanya utafiti na hatimaye kuchimba madini hatari kama urani? Nini mustakabali wa Watanzania wanaoishi kwenye vijiji vinavyozunguka mbuga hiyo ambao wanaishi maisha yao ya kila siku pasipo kujua kama kuna utafiti wa madini hatari ya urani unaoendeshwa kwa siri kubwa? Ni serikali ya aina gani, yenye uwakilishi mpaka ngazi ya kitongoji na usalama wa taifa mpaka ngazi za chini kabisa za utawala inashindwa kuyaona haya?

MCHAKATO WA KUTOA ARDHI KWA WAWEKEZAJI

Mheshimiwa Spika, uchunguzi uliofanywa na haki ardhi umebaini kuwa katika wilaya ya Kilwa, mwekezaji alikuwa na kampuni iitwayo Bioshape kutoka nchini Uholanzi. Kampuni hii ilipewa ardhi yenye ukubwa wa hekta 80,000 kwa lengo la kulima zao la mbono kaburi, ardhi hiyo ilihusisha vijiji vinne ambavyo ni Mivuji, Migelegele, Liwili na Inokwe. Mwekezaji hakutumia eneo lote na kulima hekta 800 tu katika kijiji cha Mavija ambazo ziligeuka kuwa pori baada ya mwekezaji kutelekeza shamba, vifaa na wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika, katika wilaya ya Kisarawe, mwekezaji alikuwa ni kampuni inayoitwa SunBiofuels kutoka nchini Uingereza. Kampuni ilipewa ardhi ya ukubwa wa ekari zipatazo 9000 iliyojumuisha ardhi za vijiji 11 ambavyo ni Marumbo, Muhaga, Mtamba, Mzenga A, Kurui, Chakenge, Mitengwe, Paraka, Kidugalo, Vilabwa na Chakaye. Mwekezaji huyu hakulima shamba lote bali alilima shamba la mfano katika eneo la ekari zipatazo 3000 lililopo kijiji cha Mtamba ambalo lilikuwa na mazao ambayo mengi yameanza kuzaa matunda huku yakiwa tayari kwa kuvunwa, pia Bagamoyo kampuni iliyohusika inaitwa Sekab Bioenergy Tanzania Limited.

Mheshimiwa Spika, ieleweke kuwa katika maeneo yote ardhi zilikuwa za aina mbili; zilizomilikiwa na wanakijiji na zile za vijiji ambazo zilipaswa kuhawilishwa kwanza na kisha kutolewa kwa mwekezaji. Kwa jumla, wananchi katika vijiji, watendaji wa vijiji, wajumbe wa kamati za vijiji kwa pamoja walisema hawakuridhika na mchakato uliotumika kutoa ardhi kwa wawekezaji.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani  inasikitika mchakato kujaa mizengwe, hadaa, utapeli kwa wananchi na hata harufu ya rushwa kwa baadhi ya watendaji wa vijiji, maofisa ardhi katika wilaya na vigogo wa juu katika wilaya na halmashauri. Hata pale ambapo wananchi walirubuniwa kutoa ardhi zao kwa kuelezwa kuwa mwekezaji ataleta neema katika maeneo yao, bado fidia hazikuwafikia, zilichelewa au fidia iliyotolewa ilikuwa ndogo, huku zoezi la kutathmini mali zilizopo katika ardhi zao likiwa siyo la wazi na shirikishi. Hata vigezo vya tathmini kwa ardhi na mazao havikuwekwa bayana kwa pande husika.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani kwa niaba ya wananchi inaitaka serikali kuzingatia sheria na kusimamia utekelezaji wake kwa ngazi mbalimbali kwa kuwatendea haki wananchi kuwapa huduma zenye uhalali kisheria ikizingatiwa fidia zilizotolewa hazikurandana na hali halisi ya soko kwa wakati husika.
Mheshimiwa Spika,Serikali katika hotuba yake hapa bungeni kupitia Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi mwaka wa fedha  2011/12 ilikiri kuwa na changamoto ya  kutokuwa na mfumo thabiti na utunzaji wa kumbukumbu za sekta ya ardhi na kutoa ahadi ya kujenga mfumo mmoja wa kuhifadhi kumbukumbu za ardhi kwa njia ya kielekroniki (Integrated Land Management System) utakaounganisha mifumo yote ya utunzaji wa kumbukumbu za sekta ya ardhi. Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kueleza wananchi mfumo huu umefikia wapi na utekelezaji wake uko je?
Mheshimiwa Spika, kutokana na tatizo la ardhi kwa maana ya uwekezaji na matumizi mbalimbali ya serikali kutopatikana kwa urahisi  mijini na vijijini, serikali kupitia wizara iliahidi hapa bungeni kuanzisha chombo kitakachosimamia hazina ardhi (Land Bank) ili kurahisisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya miradi ya uwekezaji na kuunda mfuko wa kulipa fidia(Land Compensation Fund) kwa mujibu wa sheria za ardhi ili kuiwezesha serikali kulipa fidia timilifu na kwa wakati inapotwaa ardhi kwa maslahi ya umma. Kambi ya Upinzani inataka kupata majibu kutoka kwa serikali ni hatua gani ziliendelea kuchukuliwa ikizingatiwa kuwa tatizo la fidia limeendelea kuwepo na kuwa kero kwa wananchi?

SEKTA YA NYUMBA
Mheshimiwa Spika, sekta hii ni sekta pekee inayoweza kuleta na kutekelezwa kwa dhana nzima ya maisha bora kwa kila Mtanzania. Nchi yetu na Watanzania kwa ujumla bado tuna matatizo makubwa ya nyumba bora na za bei nafuu kutokana na bei kubwa ya simenti na bati- bidhaa muhimu katika kutimiza azma ya ujenzi.

Mheshimiwa Spika, tulisema na tunasema kuwa bei ya simenti na bati inaweza kuwa chini ya shilingi elfu saba, kama serikali itakuwa na utashi wa kuwahudumia wananchi kwa dhati. Bei ya  simenti Uturuki  na Paksitani ukinunua tani 600,000 bei ya tani moja ni dola za Marekani 70 hadi bandarini. Guangzhou –China tani moja ni dola za marekani 26. Kwa hesabu za kawaida kwa mfuko mmoja ni dola 3.5  sawa na shilingi 5250/- kama ukinunua Pakstani au Uturuki. Ukinunua China bei itakuwa dola 1.3. sawa na shilingi 1950/-

Mheshimiwa Spika, Kambi  ya Upinzani bado inasisitiza kuwa kama Serikali ina dhamira ya kweli mfuko wa simenti hauwezi kuuzwa zaidi ya shilingi 7,500. Hivyo basi tunaitaka Serikali itueleze kwa nini bei ya simenti inauzwa zaidi ya shilingi 14000 Dar es salaam na nje ya Dar es Salaam bei ni zaidi ya hapo, wakati malighafi zinapatikana hapa hapa nchini na kiwanda kikubwa cha simenti kinatumia gesi asili ili kupunguza gharama za umeme.

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza gharama hizi na ni faida kiasi katika kodi tunayopata kwa kuwalangua Watanzania. Serikali haioni kwamba  ina wajibu wa kuondoa hizi kero wananchi wajenge nyumba bora na kwa bei nafuu?

SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA
Mheshimiwa Spika, Shirika la Nyumba la Taifa, lilipoanzishwa  mwaka 1962, moja kati malengo yake  ilikuwa ni kujenga nyumba za bei nafuu kwa ajili ya Watanzania  wafanyao  kazi mijini . Hata hivyo kwa kadiri  siku zilivyosonga  mbele, shirika hili liligeuka kutoka kuwahudumia masikini na watu wenye kipato cha kati na badala yake linawahudumia watu wa kipato cha juu.

Mheshimiwa Spika, Shirika la Nyumba la Taifa linahudumia asilimia 0.5 tu ya watanzania wote wa nchi hii.  Swali la msingi ni je Serikali imeweka mikakati gani ya kuhakikisha kuwa shirika hili linahudumia Watanzania wengi zaidi kwa kuwapatia nyumba za bei nafuu?
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/2012 Kambi Rasmi ya Upinzani imepata taarifa kuhusu ujenzi inaoendelewa kufanywa na Shirika la Nyumba katika maeneo mbalimbali nchini. Kambi rasmi ya upinzani inataka Wizara kutoa maelezo kwa umma kuhusu migogoro iliyojitokeza kati ya shirika na wapangaji na hatua ambazo zimechukuliwa kushughulikia malalamiko yaliyotolewa hususan katika maeneo ya Chang’ombe, Ubungo na mengineyo.”


KODI YA ONGEZEKO LA THAMANI  (VAT) NA ONGEZEKO  LA MTAJI (CAPITAL GAIN TAX)  KWENYE  MAUZO YA NYUMBA ZINAZOJENGWA NA SHIRIKA

Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa inayowakabili Watanzania wengi ni kuweza kupata nyumba za bei nafuu. Suala hili tulilizungumza mwaka jana, na tutaendelea kulizungumza! Kwa sheria zetu za kodi, nyumba mpya iliyojengwa kwa ajili ya kuuzwa inapaswa kutozwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) pale inapouzwa, na anayelipa kodi hiyo ni mnunuzi!.
Mheshimiwa Spika, suala la msingi ni kuwa nyumba hiyo wakati inajengwa vifaa vyote vya ujenzi vililipiwa kodi hiyo, hivyo kitendo cha mnunuzi kulipa kodi ya VAT wakati wa kununua nyumba hiyo ni kulipia kodi mara mbili (DOUBLE TAXATION). Je, serikali haioni kama haimsaidii mwananchi kuweza kuishi kwenye nyumba nzuri na kwa gharama iliyo nafuu?

Mfano dhahiri ni kwamba kwa mwaka wa fedha  2010/11 shirika  lilitarajia kujenga nyumba  49, zenye jumla ya thamani  ya shilingi  bilioni 4.08. Kwa gharama iliyotumika, wastani  wa nyumba moja ililigharimu shirika shilingi milioni 83.4.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa Kazi za Shirika la Nyumba la Taifa kuanzia  Julai 2010 hadi Mei 2011 walitarajia kupata  shilingi bilioni  6.3  kutokana na mauzo  ya nyumba hizo, yaani faida ya shilingi  bilioni 1.9  Kwa tafsiri nyingine nyumba moja itauzwa na shirika la nyumba kwa shilingi milioni 129.2, wakati gharama halisi za ujenzi ni shilingi  milioni 83. Kwa kila nyumba iliyouzwa shirika limepata faida ya  shilingi  milioni 46.

Mheshimiwa Spika, sheria ya mikopo yaani "Government Loans, Guarantees and Grants Act 1974 and amendments 2003" inalifanya shirika la nyumba la taifa kulazimika kupata kibali kutoka Wizara ya Fedha hata pale ambapo halihitaji kupata dhamana ya serikali na pia hata kwa mikopo ya ndani ya nchi. Wote tunafahamu rasilimali ambazo shirika hili linazo. Pamoja na kufahamu yote, bado tumeamua kuliweka shirika hili katika urasimu mkubwa wa kiserikali wa kupata vibali kutoka wizara ya fedha bila ya sababu za lazima. Je, serikali imedhamiria kutekeleza ahadi zake katika ujenzi wa nyumba na kuliwezesha shirika kujiendesha kibiashara kama sheria yake inavyolitaka? Kambi ya Upinzani inaitaka serikali itoe ufafanuzi ni lini inatarajia kuanzisha mchakato wa kurekebisha sheria hiyo?

MAMLAKA YA/WAKALA WA KURATIBU BEI ZA PANGO LA NYUMBA

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Kambi ya Upinzani kwa mwaka wa fedha 2011/2012 tuliitaka serikali kuanzisha  chombo kitakachoweka utaratibu  utakaotambulika kisheria ili kiwe kinatoa miongozo ya kudhibiti gharama za kodi za nyumba  kwa ujumla wake. Kwa maana nyingine ni kuanzisha mamlaka ya udhibiti itakayoitwa”Real Estate Regulatory Authority”. Tunarudia tena kusisitiza ushauri wetu huo.

Mheshimiwa Spika, sekta hii ambayo imejaa changamoto ambazo kama zikifanyiwa kazi ni dhahiri pato la taifa litaongezeka na pia tatizo la ajira linaloikabili nchi yetu linaweza kupungua kwa kiasi kikubwa kama si kuondoka kabisa. Swali muhimu la kuuliza ni kwa vipi Serikali itabadilidha changamoto kuwa fursa?
Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuangalia kwa makini kuwa mamlaka ya udhibiti ndiyo inayoweza kubadilisha changamoto zilizopo katika sekta hiyo kuwa fursa.

Mheshimiwa Spika, ninawashukuru waheshimiwa wabunge wote kwa kunisikiliza na naomba kuwasilisha.


................................................
Halima James Mdee(Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani- Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi.
11.07.2012

No comments: