Thursday, July 5, 2012

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHESHIMIWA SAID AMOUR ARFI (MB), WIZARA YA UJENZI, KUHUSU MAPITIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013



Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi  wa rehema, kwa kunipa afya njema na kuendelea kunipigania siku zote na sasa nimesimama hapa ili kutoa maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu utekelezaji wa Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha  2011/2012 na mpango wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Kwa mujibu wa kanuni za bunge, kanuni ya 99(7) toleo la mwaka 2007.

Mheshimiwa Spika, kadhalika, kipekee, nitoe shukrani kwa familia yangu kwa kuniwezesha kutimiza majukumu yangu ya kibunge na  kichama. Aidha, pongezi ziende kwa viongozi wenzangu wa chama cha Demokrasia na Maendeleo–CHADEMA kwa kazi kubwa wanayoifanya bila kuchoka katika kukidhi matarajio ya Watanzania kuwa CHADEMA ndio chama mbadala kuongoza nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee nimshukuru sana Kiongozi wa Upinzani Bungeni kwa kutupa dhamana ya kuisimamia wizara hii yenye changamoto nyingi mimi pamoja na Waziri kvuli Mhe. Pauline Gekul, tunapenda kumhakikishia kuwa tutatekeleza wajibu wetu kwa uwezo na nguvu zetu zote kwa yalivyo matarajio ya watanzania kwa chama chetu.
Mheshimiwa Spika, mwisho, lakini kwa umuhimu, niipongeze Kamati ya Miundombinu pamoja na Mwenyekiti wake kwa ushirikiano na kazi kubwa tunayoifanya katika kuhakikisha thamani halisi ya fedha za walipakodi inaonekana katika miradi ya maendeleo kwenye sekta ya miundombinu.



2.0 UJENZI NA UBORA WA BARABARA
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uchumi kwa mwaka 2011, kasi ya ujenzi wa mtandao wa barabara ulipungua kutoka asilimia 10.2 mwaka 2010 hadi asilimia 9.0. Inaendelea  kuainisha kuwa mwaka 2011 “jumla ya kilomita 29,369 zilifanyiwa tathimini, kati ya hizo kilomita 5,727 sawa na asilimia 59.1 za barabara kuu zilikuwa katika hali nzuri, ikilinganishwa na kilomita 8,364.73 sawa na asilimia 65 mwaka 2010. Hii ina maana kuwa ubora wa barabara umepungua kwa asilimia 5.9 mwaka 2011 …..Aidha kilomita 862, sawa na asilimia 9 zilikuwa na hali mbaya ikilinganishwa na kilomita 842.93 sawa na asilimia 7 mwaka 2010”
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka kupata majibu ni kwanini hali hii ilitokea na hasa ikizingatia kuwa bajeti ya wizara ya ujenzi iliongezeka kwa zaidi ya asilimia 100 ukilinganisha na mwaka 2010, wakati huohuo ubora wa barabara zetu kupungua? Kuna uhusiano gani kati ya fedha kuongezeka na barabara kupungua ubora?
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo taarifa hiyo inavyojionyesha ni ukweli uliowazi kuwa barabara nyingi zimekuwa zikijengwa chini ya kiwango na mfano mzuri ni barabara ya Misigiri - Shelui (Iramba Magharibi). Itakumbukwa kuwa Mbunge wa Iramba Magharibi wa wakati huo Mhe. Juma Kilimba aliitahadharisha serikali kuhusiana na ujenzi wa barabara hiyo kuwa uko chini ya kiwango kwa kuwa alikuwa mfuatiliaji wa masuala ya msingi, lakini serikali haikuchukua hatua yoyote kukabiliana na hali hiyo.
Mheshimiwa Spika, kutokana na serikali kutochukua hatua wakati huo taarifa zilizopo ni kuwa barabara hiyo inapaswa kujengwa  upya na sio kufanyiwa ukarabati. Hii ni hasara kubwa sana kwa Serikali kwani kwa kipindi cha chini ya miaka 3 tunaenda kujenga barabara ambayo tayari ilishajengwa badala ya kutumia fedha hizo kujenga barabara mpya.
Kambi ya upinzani, inataka kupata majibu ni hatua gani zimechukuliwa na serikali kwa mkandarasi pamoja na mshauri mwelekezi ambao walihusika na ujenzi huu. Pia tunawataka wabunge wawe wanafuatilia miradi ya barabara ambayo inajengwa kwenye majimbo yao ili kuliepusha taifa na hasara kubwa kama hii na haswa kufuatilia viwango. Aidha, Serikali ichukue hatua kila taarifa inapotolewa ili kuepuka hali hii isijirudie tena.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Kyamyorwa-Buzirayombo (km-120) nayo ilijengwa chini ya kiwango kilichopelekea barabara hii kukataliwa kupokelewa na kutakiwa mkandarasi kurudia kufanya marekebisho kwa viwango vinavyotakiwa.
Kambi ya Upinzani inataka kujua hatua iliyofikiwa hadi sasa kwani ni takriban miaka minne imepita. Pia tunataka kujua ni hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa barabara ya Kilwa (Dar es Salaam) ambayo ilijengwa chini ya kiwango.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani, katika kupitia kitabu cha pili cha mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti ya mwaka kwa kipindi kinachoishia mwezi Juni, 2012 kinaonesha fedha za maendeleo zilizotolewa na serikali hadi mwezi wa April 2012.  Kati ya miradi 61 iliyotengewa fedha, miradi 26 hazikupelekewa fedha kabisa pamoja na kwamba Bunge lilipitisha fedha kwa miradi hiyo.(Kiambatisho: katika Randama ya mapitio ya utekelezaji na  mpango  wa bajeti 2011/2012)
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni kwanini miradi hiyo haikutengewa fedha kwa mujibu wa bajeti iliyopitishwa na Bunge hili.
2.1 Miradi ya Barabara.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapenda kulikumbusha Bunge lako Tukufu na Watanzania kwa ujumla kuwa mikataba mingi ya ujenzi wa barabara iliwekwa mwaka 2009/2010 tukielekea kwenye uchaguzi mkuu na muda wa kukamilika miradi hiyo si zaidi ya miezi 36. Mikataba yote iliyosainiwa 2009 inapaswa kukamilika mwaka 2012 na ile ya mwaka 2010 inapaswa kukamilika mwaka  2013. Na takriban miradi yote ya ujenzi wa barabara hadi sasa imeshatekelezwa  chini ya asilimia 50%.
Mheshimiwa Spika, kwa uchache miradi inayotakiwa kukamilika mwaka huu ni pamoja na barabara ya Sumbawanga hadi Kibaoni, Sumbawanga hadi Matai na Kasanga. Pia barabara ya Handeni –Mkata, Tunduma-Sumbawanga na nyinginezo hazitakuwa zimekamilika mwaka huu kwa mujibu wa mkataba, matokeo yake barabara hizi zitachukua muda mrefu kukamilika na kuligharimu taifa fedha nyingi zaidi kwa malengo ya mafanikio na kisiasa na gharama hizo zitabebwa na watanzania  masikini wasio.  
Mheshimiwa Spika, miradi iliyosainiwa mwaka 2010 na kutarajiwa kukamilika mwaka 2013, ni pamoja na:  barabara ya Manyoni - Itigi-Chaya yenye urefu wa km 89.30 tarehe ya kuanza kazi rasmi ilikuwa 20 Disemba 2010 na tarehe ya kumaliza kazi ni 20 Disemba 2013. Mkandarasi wa mradi huu ni Sinohydro Coorporation Limited, China. Mpaka mwezi May 2012 hali ya utekelezaji wa Mradi huu ilikuwa imefikia kuwa kusafisha eneo la ujenzi 46%, kujenga tuta la barabara 13.7%, kujenga tabaka la sementi 0%, kujenga tabaka la kokoto 0%, kujenga tabaka la lami nyepesi 0%.
Mheshimiwa Spika, hali ni hiyo hiyo kwa barabara ya Tabora –Nyahua yenye urefu wa kilomita 85.0, barabara ya Tabora –Urambo yenye kilomita 94.0, Tabora-Nzega yenye kilomita116.  Changamoto kubwa ni kuwa kila mradi wa ujenzi wakandarasi wanaidai serikali fedha, na Serikali haijaweza kulipa na hivyo katika miradi hiyo wakandarasi wamepunguza kasi na kutoa tangazo la dhamira ya kusimamisha ujenzi katika baadhi ya barabara mwezi mei 2012 kwa kutokulipwa madai yao kwa wakati.
Kambi ya upinzani, inataka kupata taarifa ni kwanini wakandarasi hawa hawajalipwa kwa wakati ili waweze kutekeleza miradi hii kama ilivyokusudiwa wakati Fedha zilizotengwa na kuidhinishwa na Bunge kiasi cha shilingi 14,415,640,000 (volume 4 development) mwaka jana kwa ajili ya mradi huu zilienda wapi?
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara ya Geita-Sengerema umekamilika kwa asilimia 100 tangu Februari 2010, lakini mkandarasi bado anadai shilingi 273,702,658.35 ambayo inasababisha matatizo mengi ya kimkataba ikiwemo kuongezeka kwa riba ya ucheleweshaji malipo na kuongeza mzigo wa deni. Hivyo hivyo barabara ya Sengerema –Usagara Km 40 ambayo imekamilika na kupokelewa Serikalini mwaka 2010; iliyokuwa inajengwa na Mkandarasi Sinohydro Cooperation Limited ambaye anadai shilingi 5,728,347,080.97, na mhandishi mshauri anadai shilingi 637,866,136.29. na hivyo kulifanya deni kuwa shilingi 6,366,213,217.26. Na kutokana na deni hili linasababisha riba ya deni kuendelea kuongezeka kutokana na masharti ya mkataba. Kambi ya Upinzani inataka kupata majibu ni lini deni hili litalipwa? Na je, fedha za kulipia deni hili zipo kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha?
Mheshimiwa Spika, barabara ya Kyaka-Bugene kilomita 59.1 mkataba ulisainiwa mwaka 2010 hadi sasa asilimia 57 ya mkataba umepita na kazi za ujenzi unasuasua na hivyo kufanya hadi sasa  utekelezaji ni asilimia 20 tu, kutokana na tatizo la malipo. Aidha, Kambi ya Upinzani inataka kujua hatua madhubuti zilizochukuliwa ili kukamilisha mradi huu sambamba na kipande cha Ndundu-Somanga kilomita 60 kwenye barabara itokayo Dar es Salaam kwenda Mtwara.
Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara ya Ushirombo- Lusaunga kilomita 110, kazi zimesimama tangu tarehe 23 August, 2011 hadi sasa kutokana na madeni. Kama tulivyotangulia kusema awali miradi hii ilikuwa na lengo la kisiasa kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2010, kuliko uwezo halisi wa Serikali kuhimili kulipia huduma kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Kagoma-Lusaunga kilomita 154 ni miongoni pia ya mikataba ya ujenzi iliyosainiwa mwaka 2009; pamoja na kuongezewa muda zaidi ya miezi 36 ya awali inatakiwa ikamilike Januari 2013. Lakini mkandarasi ametoa taarifa ya kupunguza kasi ya ujenzi kwa sababu anadai jumla ya shilingi bilioni 12.56 na dola za Kimarekani milioni 14.56. Kambi ya Upinzani inataka kufahamu mkakati wa Wizara wa kulipa deni hili kwa kazi ambayo tayari imefanyika ili mradi ukamilike kwa wakati, na hatua zilizochukuliwa za kuhamisha nguzo za umeme, simu na mabomba ya maji katika mji wa Biharamulo.

Mheshimiwa Spika, usanifu wa barabara na utayarishaji wa vitabu vya zabuni barabara ya Kidahwe-Kasulu-Kibondo-Nyakanazi (kilomita 310) uliahirishwa kutokana na tatizo la fedha. Kambi ya Upinzani inataka kujua hatua iliyofikiwa hadi sasa, kwani barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa Taifa na kiungo kwenda kanda ya ziwa na nchi jirani.
2.3 Ujenzi wa Miradi Maalum ya Barabara.
Mheshimiwa Spika,  bajeti  ya serikali ya mwaka jana ilionyesha kuwa zilikuwa zimetengwa fedha kiasi cha shilingi 348,075,000,000 kwa ajili ya kitu kinachoitwa “Special road construction Projects” (fungu 4168), na katika hotuba ya Kambi ya Upinzani  tulihoji hapa bungeni kuhusiana na fedha hizi .
Mheshimiwa Spika, naomba kunukuu “Mheshimiwa Spika, kitabu cha Miradi ya Maendeleo (sehemu-A juzuhu iv) katika fungu 98, kasma 4168 utaona kuwa kuna mradi unaitwa “Miradi ya ujenzi wa barabara maalum” (special road construction projects) na fungu hili limetengewa kiasi kikubwa kuliko mradi mwingine wowote wa ujenzi wa barabara katika mwaka huu wa fedha kwani zipo jumla ya shilingi 348,075,000,000 na hizi zote ni fedha za ndani. Kwa hakika hizi ni fedha nyingi sana na hasa ikizingatiwa kuwa kitabu hicho kimeonyesha miradi yote ya ujenzi wa barabara ambayo itatekelezwa katika mwaka huu wa fedha, ila hii miradi maalum haijaonyeshwa ni miradi ya barabara gani na zitajengwa wapi.
Mheshimiwa Spika, kasma hii kwa mwaka wa fedha 2009/2010 na  2010/2011 haikuwa imetengewa kiasi chochote cha fedha na ndio maana imetustua kuona mwaka huu fedha nyingi kiasi hicho kinatengwa kwa miradi isiyojulikana kuwa itajengwa wapi.
Kambi ya Upinzani tunataka kupata maelezo ya kina ni miradi gani hii ambayo haiwezi kuandikwa na inatengewa fedha nyingi kiasi hicho? Kwani hii italiwezesha Bunge kuweza kupitisha bajeti inayoifahamu, na kuisimamia serikali kwa kuweza kufuatilia utekelezaji wa miradi hii. Pili, fedha hizi zipangwe kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara za kimkakati ambazo Kambi ya Upinzani imependekeza ili ziweze kuunganisha mikoa husika na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi” Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, majibu ya serikali yalikuwa kama ifuatavyo “fedha hizi ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi tunayotakiwa tuchangie fedha ili tupewe mikopo. Sehemu kubwa ya miradi yetu ya barabara inatekelezwa kwa fedha za mikopo” mwisho wa kunukuu. (Chanzo: majibu ya hoja za waheshimiwa wabunge yaliyotolewa na wizara ya ujenzi)
Mheshimiwa Spika, kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha 2012/2013  hakuna fedha yoyote ambayo imetengwa kwa ajili ya kasma hii na hili linaendelea kuzua maswali na hasa kutokana na majibu yaliyotolewa mwaka jana kuhusiana na fedha hizi .
Kambi ya Upinzani inataka kupata majibu kuhusiana na mambo yafuatayo:

  1. Je, Mwaka huu wa fedha hatutegemei kukopa fedha kwa ajili ya miradi ya barabara na hivyo kulazimika kuchangia?
  2. Fedha zilizokuwa zimetengwa kwenye bajeti ya mwaka 2011/2012 zilitumika kugharamia mikopo ipi na kwa ajili ya miradi ipi ya barabara?
  3. Fedha hizi ziliwekwa kwenye akaunti ipi kwani kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2010/2011 inaonyesha kuwa TANROADS walikuwa hawajafungua akaunti maalum kama ambavyo sheria inataka kwa ajili ya Counter part funds.
Mapendekezo na Ushauri
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapenda kutoa mapendekezo na ushauri kama ifuatavyo:-

  1. Serikali ihakikishe kwanza inalipa madeni yote yaliyopo ili kuwezesha miradi ya ujenzi wa barabara ukamilike kwa haraka.
  2. Serikali ikamilishe utaratibu wa kupata wakandarasi katika vipande  ambavyo havijaanza kujengwa  katika barabara ya Manyoni-Itigi Tabora na Tabora-Urambo, Kigoma na kukamilisha kipande cha Ndundu-Somanaga,  barabara ya Dar-Lindi hadi Mtwara na Kibaoni –Mpanda, barabara ya Sumbawanga –Mpanda, ili barabara hizi zikamilike kwa pamoja na kukamilisha miradi husika.
  3. Serikali itoe kipaumbele kwa barabara ambazo zinatumika kuhamisha shehena kubwa ya mazao ya chakula kutoka maeneo ya uzalishaji, kama vile barabara ya Mpanda-Tabora na nyinginezo.
  4. Kuongeza kasi katika kuhakikisha upanuzi wa barabara ya Dar-Chalinze ili kupunguza msongamano na ajali katika barabara hiyo.
  5. Itenge fedha za kutosha kwa ajili ya barabara kuu ya kutoka Iringa-Dodoma-Kondoa-Babati hadi Arusha kwani barabara hii ndiyo inaunganisha kusini na kaskazini mwa nchi yetu.
  6. Kutengeneza mpango mkakati na mpango wa utekelezaji katika majiji ya Mwanza, Arusha na Mbeya ili kukabiliana na changamoto ya msongamano wa magari kama ilivyo Dar es Salaam leo.
3.0 SAKATA LA BOMOA-BOMOA NCHINI
Mheshimiwa Spika, mwanzoni mwa mwaka uliopita 2011 karibu nchi nzima liliendeshwa zoezi la kuweka alama ya X nyumba na mali zote zilizopo katika hifadhi ya barabara ili kupisha nafasi hizo kuwa wazi au kupisha upanuzi wa barabara.
Mheshimiwa Spika, zoezi hili limezua malalamiko mengi sana miongoni mwa wananchi walioathirika na hali hiyo, na jambo hili likamfanya Mhe. Waziri Mkuu kutoa kauli kama ilivyonukuliwa na vyombo vya habari tarehe 06/03/2011, naomba kunukuu; “Rais aliona sekta ya barabara panalegalega na kumrudisha Dk. Magufuli kwenye Wizara hii, lakini ameanza kwa spidi kubwa hivyo tumemwagiza asimamishe oparesheni hii hadi suala hili litakapojadiliwa na Baraza la Mawaziri na kuongeza kuwa kasi hiyo imeitisha”
Mheshimiwa Spika, kutekeleza agizo hilo katika jiji la Dar es Salaam juu ya bomoabomoa katika barabara ya Morogoro Waziri Mkuu aliagiza ofisi ya Mkuu wa Mkoa kufanya tathmini ya zoezi hilo kabla halijaanza kutekelezwa na kutoa taarifa hapo baadae.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunaitaka serikali kufanya tathmini ya kina kabla ya kuanza kutekeleza zoezi hilo kwa sababu lina mkanganyiko mkubwa sana ukizingatia kuwa wapo wananchi waliokuwa wanaishi katika baadhi ya maeneo hata kabla ya sheria ya hifadhi ya barabara ya mwaka 2007 haijatungwa. Pia Halmashauri nyingi nchini pamoja na Wizara ya Ardhi wametoa leseni za makazi/ ramani/ vibali/ hati za ardhi katika maeneo ambayo yapo kwenye hifadhi ya barabara.
Mheshimiwa Spika, pamoja na umuhimu wa kuboresha miundombinu ya barabara nchini, Kambi ya Upinzani tunaitaka serikali kufanya maamuzi ya pamoja kama serikali (collective responsibility) kuanzia serikali kuu mpaka serikali za mitaa kuhusu utekelezaji wa zoezi la bomoabomoa na sio kutumia sababu moja tu ya utekelezaji wa sheria ya hifadhi ya barabara ya mwaka 2007.

3.1. Fidia kwa Wananchi.
Mheshimiwa Spika, katika miradi mingi ya ujenzi wa barabara kumejitokeza ulipuaji wa baruti miamba karibu na makazi ya wananchi na athari zake hujitokeza baada ya kazi  kumalizika jambo ambalo  huwapa hasara wananchi na usumbufu, wakati wa  kudai fidia zao huleta kero kwa wananchi. Maeneo mengi nchini  kama barabara ya Minjingu/Babati/Dareda, Nyahua hadi Tabora, Kagoma-Lusaunga hadi Biharamulo wameathirika na hilo.

Mheshimiwa Spika, jambo hili kwa kiasi kikubwa linatokana na ukweli kwamba wahandisi washauri wengi hawafanyi upembuzi yakinifu kwa madhara ambayo yanaweza kutokea katika zoezi la ulipuaji wa miamba. Tukumbuke kuwa tatizo hili la fidia ya ulipuaji wa miamba imekuwa ni adha kubwa kwa wananchi wa maeneo husika.  Hivyo basi, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kufanya upembuzi yakinifu kwa maeneo tajwa yaliyoathirika na ulipuaji na hivyo kutoa fidia stahiki kwa wahusika.

Mheshimiwa Spika, masuala ya utoaji wa fidia hapa nchini kwa muda mrefu sasa yamekuwa hayazingatii katiba ya nchi, sera, sheria, kanuni za ardhi na maslahi ya wamiliki wa ardhi husika.  Hii ni kutokana na manung’uniko ya wananchi wanaohamishwa katika maeneo yao kulipwa viwango vidogo vya fedha kama fidia. Vilio vya wananchi vimekuwa vikisikika katika vyombo mbalimbali vya habari na hata kesi mbalimbali kufunguliwa katika Mahakama za ardhi nchini kuashiria wananchi kutoridhika na michakato ya fidia inayofanyika katika maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, “fidia ya ardhi” ni gharama ambazo mmiliki halali wa ardhi hulipwa kwa kuzingatia haki zake juu ya ardhi husika, yaani; thamani ya ardhi, maendelezo katika ardhi husika na maslahi mengine juu ya ardhi kwa mmiliki. Endapo mwananchi ambaye eneo lake linachukuliwa kwa ajili ya upanuzi wa barabara, ni haki yake ya msingi kushiriki katika hatua zote ikiwa ni pamoja na kupewa fidia kwa mujibu wa kifungu cha 3(g) cha sheria za ardhi na.4 na na.5, 1999.
Mheshimiwa Spika, ni muda mrefu sasa utaratibu huu wa kuwashirikisha wananchi katika hatua zote muhimu kwa ajili ya kuweza kupata fidia kwa mujibu wa sheria kama ambavyo tumeelezea hapo juu haufuatwi.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na taarifa kwamba serikali imetenga kiasi cha zaidi ya Sh. bilioni 20 kwa ajili ya shughuli ya kuwalipa fidia wananchi ambao nyumba zao zitabomolewa kwa ajili ya kupisha utekelezaji wa mradi wa ujenzi na upanuzi wa barabara kati ya Tandika Devis Kona Manispaa ya Temeke hadi Jet-Kona Manispaa ya Ilala. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge juu ya matumizi  halisi ya fedha tajwa hapo juu.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa pia na malalamiko ya wananchi wa maeneo mbalimbali kama vile Vijiji vya Mazingara, Mkata, Vibaoni, Kilole wilaya ya Bagamoyo, wilaya ya Handeni, Wilaya ya Ruangwa na maeneo mbalimbali katika mikoa ya Kigoma, Kagera, Tabora, Rukwa na maeneo mengine ambayo miradi ya ujenzi wa barabara inatekelezwa hapa nchini kuhusiana na fidia ama kuwa ndogo, kutokulipwa kwa wakati au kutokulipwa kabisa na kuwafanya Watanzania hawa kuwa masikini.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sheria na taratibu ni kuwa msingi wa kukadiria thamani ya ardhi yoyote na uboreshaji kwa ajili ya ulipaji wa fidia vigezo vinavyotumika ni pamoja na thamani ya ardhi hiyo katika soko, Maendelezo yanayofanyika katika ardhi kama vile majengo na mazao yanatakiwa kulipwa kwa mmiliki wa ardhi kama gharama halali na halisi alizotumia kufanya maendelezo katika ardhi husika, posho ya usumbufu, gharama za nauli pamoja na riba ya miezi kumi na mbili kulingana na viwango vya riba vya kibenki. Riba kwenye fidia yoyote italipwa na serikali kuu au mamlaka ya serikali ya mitaa pale tu ambapo malipo ya fidia hayakulipwa kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba miliki ya mtu inapoingiliwa, mabadiliko ya kimaisha lazima yatatokea. Mfano ni wahanga wengi ambao wamekuwa wakiishi katika maeneo yao kwa muda mrefu. Kwa sehemu kubwa, wanapohamishwa pasipo kupatiwa ardhi mbadala, matokeo yake ni kuwafanya waishi maisha ya kutangatanga katika nchi yao. Ni haki yao kupatiwa ardhi maeneo mengine na ardhi hiyo iwe imepimwa ili kuongeza uhakika wa ardhi husika na pasipo kufikwa na bomoabomoa nyingine au kuhamishwa, jambo ambalo limekuwa halifanyiki hapa nchini na hivyo kuwafanya wananchi ambao wanakumbwa na bomoabomoa kujikuta katika wakati mgumu sana wa kuweza kuendeleza maisha yao.
Kambi ya Upinzani tunaitaka serikali iwe na utaratibu wa kuwalipa wananchi fidia timilifu na kwa wakati na wawe wanalipwa kabla ya bomoa bomoa kufanyika kwani kitendo cha kubomoa kabla ya fidia kinawafanya wananchi husika kuathirika sana na hivyo kushindwa kuendesha maisha yao.

Kambi ya Upinzani inapendekeza hatua zifuatazo ziweze kuchukuliwa na serikali ili kuondokana na hali hii:

  1. Wizara ya ardhi kurejelea ramani (Master plan) ya jiji la Dar es Salaam na nchini kote kufahamu bayana barabara za wilaya na mikoa na mikakati ya mpango wa uendelezaji wa barabara na pia kuwafahamisha wananchi kuhusiana na mipaka hiyo.
  2. Serikali iwachukulie hatua watendaji wanaokiuka utaratibu wa matumizi ya hifadhi ya barabara na kusababisha usumbufu kwa wananchi. Hali halisi inaonyesha kwamba wenye taaluma hii ndio wamekuwa wakipotosha watanzania kwa kuruhusu umiliki wa ardhi kwa matumizi mengine tofauti na yaliyopangwa mathalani ardhi kwa ajili ya barabara. Pia, wamekuwa wakipima na kugawa viwanja mijini kiholela bila kujali kama kuna umuhimu wa kuwa na maeneo ya barabara, shule, zahanati, soko, nyumba za ibada, viwanja vya michezo na matumizi mengine.
  3. Serikali iwajibike na sio kufumbia macho uvunjwaji wa utaratibu uliowekwa katika hifadhi za barabara na matumizi mengine kwa manufaa ya wananchi. Mfano hai ni katika miji ambayo ina hadhi ya majiji na manispaa kama Dar es Salaam, Mwanza, Iringa, Mbeya na Arusha. Mipango mikuu ya majiji na manispaa hizi hazifuatwi kabisa.
  4. Maafisa mipango miji wakaguliwe utendaji wao unaotakiwa kufuata maadili ya kazi. Hii ni kutokana na kuwa ni maafisa wanaolalamikiwa sana na wananchi kwa tabia yao ya kudai na kupokea rushwa. Kinachotakiwa ni kuangalia Mipango Mikuu ya miji na kuangalia hali halisi ya ujenzi.
  5. Pale inapolazimika kuvunja pande zote mbili za barabara basi walipwe fidia wote na si upande mmoja wa barabara na mwingine kutokulipwa ili kuondoa malalamiko ya wananchi na kuwatendea haki sawa.

4.0 WAKALA WA BARABARA TANROADS

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali kuhusu miradi inayofadhiliwa na wafadhili ya mwaka 2010/2011 inaonyesha kuwa kiasi cha dola za kimarekani 73,520.38 kililipwa kama kodi kwa AIRTEL TANZANIA LTD kwa ajili ya mwezi April  ambazo ni sawa na shilingi 110,280,000 . Na fedha hizi zilitumika kutoka kwenye fungu la fedha za miradi ambayo inafanywa kwa ubia baina ya Serikali na wafadhili kinyume na mikataba na  hati ya makubaliano.
Kambi ya Upinzani inahitaji kupata maelezo ya ukiukwaji uliofanywa; pia kodi hiyo ni kwa ajili ya mwezi April tu au kwa ajili ya mwaka mzima?

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye randama ya wizara ya ujenzi fungu 6383 utaona kuwa wakala wa barabara kwa mwaka huu wa fedha wametenga kiasi cha shilingi milioni 120.5 kwa ajili ya kuanza kazi za ujenzi wa makao makuu. Kambi ya Upinzani inaona kiasi kilichotengwa ni kidogo sana bila ya kuangalia athari ya kuendelea kupangisha ofisi za wakala katika jengo la AIRTEL. Aidha, tunashauri wakala wa barabara kujenga ofisi zao wenyewe katika kipindi kifupi kijacho.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka maelezo ni kwa nini wakala ukapangishe jengo la ofisi kutoka miongoni mwa wateja ambao anapaswa kuwahudumia na kuwasimamia (Hasa kwenye suala la kuweka mabango ya matangazo kandokando mwa barabara).Makampuni mengine ya simu yatatendewa haki? Na je Airtel akiweka bango vibaya wakala utaweza kumwajibisha ama utakuwa na hofu ya kuondolewa kwenye jengo hilo?.

Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo hiyo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonyesha kuwa wakala wa barabara alitumia kiasi cha shilingi 49,581,000 kwa ajili ya ukarabati wa dharura kwenye eneo  la Same –Himo, na fedha hizi kiasi cha shilingi 46,958,975 zililipwa kutoka makao Makuu ya wakala na kiasi cha shilingi 2,471,525 kililipwa na Tanroads Mkoa wa Kilimanjaro  bila fedha hizo kuidhinishwa na Benki ya Dunia .

Kambi ya Upinzani inataka kupata majibu je ni utaratibu gani unatumika katika kukarabati barabara?   Je, fedha hulipwa na wakala moja kwa moja au hutumwa kwa wakala kwenye mkoa husika?

Mheshimiwa Spika,  taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonyesha kuwa wakala ulilipa malipo ya awali ya kiasi cha dola za kimarekani 7,495,658.50 ambazo ni sawa na shilingi 10,068,269,000 kwa kiwango cha shilingi 1,550 kwa dola 1, kabla ya mkataba No.TRD/HQ/1064/2010/11 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Arusha – Minjingu (98.0 km) kabla mkataba wa ujenzi kuidhinishwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali , kinyume na sheria ya manunuzi ya umma kifungu cha 55 (6) NO.21 ya mwaka 2004.

Kambi ya upinzani tunataka kupata maelezo ya kina juu ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya waliohusika kuvunja sheria na kupuuza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambayo ipo kikatiba na kisheria, kwani kama hatua hazitachukuliwa jambo hili linaweza kuisababishia serikali hasara kutokana na mikataba kutokidhi viwango vya kisheria.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali/wakala kuangalia upungufu wa wataalam wahandisi na mafundi mchundo katika ofisi zao nyingi mikoani na kuajiri wataalam wa kutosha ili kuwezesha usimamizi mzuri wa miradi na kazi nyingine za kitaalam zifanyike kwa ufanisi. Kadhalika, tunaishauri Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI na Wizara ya Ujenzi kuangalia uwezekano wa kuanzisha Wakala wa Ujenzi wa Barabara Vijiji (Tanzania Rural Roads Agency) na kuajiri wataalam wa kutosha kwa usimamizi bora wa barabara za vijijini.

5.0 BODI YA MFUKO WA BARABARA
Mheshimiwa Spika, mwaka 2011 mfuko wa barabara ulikusanya mapato ya shilingi bilioni 401.935 ikilinganishwa na shilingi  bilioni 278.231 zilizokusanywa mwaka 2010 sawa na ongezeko la asilimia 44.5; ongezeko hilo linatokana na kupungua kwa uchakachuaji wa mafuta kutokana na kuongezeka kwa bei ya mafuta ya taa ambalo limekuwa ni tatizo kubwa sana kwa wanachi waishio vijijini.
Mheshimiwa Spika,bodi ya Mfuko wa Barabara ilianzishwa mwaka 2000 ikiwa ni moja ya mikakati ya kuboresha Sekta ya barabara hususani katika kukusanya, kutoa na kuratibu matumizi ya fedha za matengenezo ya barabara. Sheria ya Ushuru wa Barabara (Marekebisho Na. 2) ya mwaka 1998, iliyounda Bodi ya Mfuko wa Barabara na Mfuko wa Barabara, ilifanyiwa marekebisho mwaka 2006, na kuitwa “Road and Fuel Tolls Act Cap 220, Revised edition 2006”. Hadi sasa vyanzo vya mapato kwa mujibu wa sheria ni kama ifuatavyo: ushuru wa barabara unaotozwa katika mafuta ya petroli na dizeli, ushuru wa magari ya kigeni mipakani na  tozo ya magari yaliyozidisha uzito.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Waziri wa Ujenzi ya mwaka 2011/12 katika ukurasa wa 97 kuhusu bodi ya barabara alisema; nanukuu “bodi itaanzisha utaratibu wa kuwatumia wataalamu washauri waliopo maeneo husika (local consultants) kwa ajili ya kukagua ubora wa kazi (value for money) wakati miradi ya matengenezo inapoendeleaKambi ya Upinzani inahoji  kama ahadi hii ya serikali imetekelezwa kwa kiwango gani ikiwa sote tumeshuhudia barabara zikiendelea kujengwa bila ubora kwa kuzingatia thamani ya pesa na mifano ya barabara hizi ni mingi maeneo mbalimbali ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, tatizo la magari kuzidisha mizigo halitaweza kutatuliwa kwa kutoza faini magari yanayozidisha viwango vya mizigo. Serikali kuendelea kutegemea mapato kutokana na uvunjifu wa sheria ni kuruhusu uvunjaji wa sheria kwa makusudi. Pia kuruhusu uharibifu wa barabara zinazojengwa kwa kodi za watanzania ni utaratibu wa ajabu wa kutunza barabara

Mheshimiwa Spika, ni wazi kuendelea kutoa adhabu za tozo au faini kwa wanaozidisha uzito hakutaweza kutatua tatizo hili. Kambi ya Upinzani  tunaitaka serikali kubadili mfumo wa kuongeza mapato ya mfuko wa barabara kwa kutegemea faini na tozo hizi na kuandaa sheria maalumu ya kudhibiti uzidishaji wa mizigo kwa magari na iweke adhabu kali zaidi ili kuweza kuzilinda barabara zetu na madaraja ambavyo vyote hivi tunavijenga kwa gharama kubwa.

Mheshimiwa Spika,    kwa mujibu wa taarifa za serikali ni kuwa hadi Aprili 2011 magari yapatayo 732,307 yalikuwa yamepimwa ambapo kati ya hayo magari 168,041 yalikuwa yamezidisha uzito ambapo ni sawa na asilimia 22.95 ya magari yote yaliyopimwa. Fedha zilizokusanywa kutokana na tozo ya uharibifu wa barabara na malipo ya kupitisha mizigo mipana ilikuwa shilingi milioni 1,094.718.
Mheshimiwa Spika , ukiangalia kiwango cha fedha zilizotozwa kama faini na tozo mbalimbali , na ukaangalia uharibifu wa barabara uliofanywa na magari hayo na kisha ukawianisha na gharama inayohitajika kwa ajili ya kujenga kilomita moja ya lami ni wazi kuwa kuendelea na utaratibu wa kutoza faini hakulisaidii taifa bali ni kuendelea kuharibu barabara zetu ambazo tunazijenga kwa gharama kubwa sana.  Kwa mfano gari iliyokuwa inatoka Dar Es Salaam kuelekea Mwanza ikiwa na mzigo uliozidi ni hakika kuwa kiwango cha uharibifu wa barabara na madaraja yetu kitakachotokea hakiendani na faini itakayotozwa.
Kambi ya Upinzani, tunaendelea kushauri kuwa pamoja na faini na tozo hizi, pawepo na utaratibu wa kisheria kwa zile kampuni ambazo zitabainika kuwa wanaongoza kwa kuongeza uzito wa mizigo kwenye magari yao wawe wanafungiwa kupita barabarani kwa vipindi kama vile kwa miezi mitatu, sita au hata mwaka mmoja ili liwe fundisho na itasaidia kuzinusuru barabara zetu na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu na ambao kulipa faini sio tatizo kwao kwani fedha wanazo.
Mheshimiwa Spika,utekelezaji wa ukusanyaji wa mapato ya mfuko wa barabara kwenye ushuru wa barabara katika mafuta ya petrol na dizeli chini ya mkakati wa kudhibiti uchakachuaji wa mafuta ya petrol na dizeli ulivyoainishwa na waziri katika hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2011/2012 ukurasa 97 nanukuu “kudhibiti uchakachuaji wa mafuta” ,kwa kuongeza kodi kwenye mafuta ya taa, hatua zilizochukuliwa zimeendelea kuwaumiza mwananchi na haswa waishio vijijini ,Kambi ya Upinzani tunaitaka serikali kupunguza kodi hii kwenye mafuta ya taa ili wananchi waweze kupunguza ukali wa maisha.
Ajali za barabarani.
Mheshimiwa spika ,kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uchumi ni kuwa ajali za barabarani zimekuwa zikiongezeka kwa kasi tangu serikali ya awamu ya nne ilipoingia madarakani mwaka 2005 na hii inatokana na takwimu zinazoonyesha kuwa mwaka 2005 zilikua ajali za barabarani (16,388), 2006 (17,039), 2007 (17,753), 2008 (20,615), 2009 (22,739), 2010 (24,665) na mwaka 2011 (23,986).
Mheshimiwa Spika, ajali hizi ni dhahiri kuwa zimelisababishia taifa hasara kubwa sana kama vile kupoteza nguvu kazi kutokana na vifo vya ajali hizi, watu kupata ulemavu wa kudumu na hivyo kuwafanya wengine kuwa tegemezi kutokana na ulemavu walioupata nk. Miongoni mwa vyanzo vya ajali hizi ni pamoja na barabara kujengwa chini ya kiwango na nyingine kuwa na utelezi kama mvua zinanyesha na hivyo kuyafanya magari kushindwa kutulia barabarani.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kupitishwa kwa sera ya usalama barabarani Januari 2008 lakini jambo la kushangaza ni kuwa mpaka sasa wizara inaendelea na maandalizi ya mikakati ya utekelezaji wa sera na bado sheria ipo kwenye hatua ya rasimu. Kambi ya Upinzani inataka kujua ni lini muswada wa sheria ya Usalama barabarani utawasilishwa Bungeni.
Kambi ya upinzani, inataka kujua ni mikakati gani ambayo wizara na serikali imechukua ili kukabiliana na wakandarasi hawa wanaojenga barabara chini kiwango na hatimaye kuchangia engezeko la ajali za barabarani? Kwani kuna taarifa kuwa baadhi yao ndio hao hao wanaopewa kandarasi za kujenga barabara nyingine nchini hata baada ya kubainika kuwa baadhi ya maeneo wamejenga barabara kwa kiwango cha chini.
6.0 WAKALA WA MAJENGO TANZANIA
Mheshimiwa Spika, Wakala wa Majengo ulianzishwa mwezi Mei mwaka 2002 chini ya Sheria Na. 30 ya mwaka 1997 ya Wakala za Serikali. Lengo la kuanzisha Wakala huu ni kuwezesha kuwa na nyumba bora zaidi za kuishi watumishi wa Serikali wakiwa kazini na baada ya kustaafu kwa kujenga nyumba na kuwakopesha; kujenga majengo ya Serikali kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa na kuyatunza; na pia kutoa huduma za ushauri wa kitalaam kuhusiana na majengo.
Mheshimiwa Spika, wakala wa majengo mbali na dhana nzuri ya uanzishwaji wake, lakini wakala umekuwa haupatiwi fedha za kutosha ili kutekeleza majukumu yake. Mfano mzuri ni kwamba mwaka wa fedha uliopita zilitengwa shilingi billion 5.3, lakini fedha zilizotolewa ni shilingi bilioni 2.8.  Mwaka huu wa fedha wakala wa majengo wametengewa shilingi bilioni 5.98. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni kwanini fedha zinazotengwa kwa wakala huyu hazitoshi kutimiza majukumu yake au ni mtindo ule ule wa taasisi kuwepo tu lakini hazitoi tija yoyote kwa maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaamini kabisa kama kweli Wakala wa majengo alitakiwa kujenga nyumba za watumishi wa Serikali, basi ni dhahiri kuwa wakala huyu anashindwa kuelewa vizuri majukumu yake. Tatizo sugu la ukosefu wa nyumba za walimu, madaktari, na watumishi wengine, majengo ya mashule na majengo kadhaa ya Serikali ambayo ujenzi wake ndilo jukumu lake la msingi wanakiacha badala yake ujenzi wa majengo hayo unajengwa na wakandarasi binafsi jambo linalopelekea majengo hayo kujengwa kwa ubora wa viwango vya chini kabisa.  Hii ni hasara kwa serikali na kwa wananchi ambao wanachangia katika ujenzi wa shule na nyumba za waalimu.  
Mheshimiwa Spika, wakala wa majengo lengo lake halikuwa ni kufanyabiashara lakini kwa sasa wakala umejikita katika kufanyabiashara zaidi kuliko kujenga nyumba za watumishi wa umma. Shirika la Nyumba la Taifa nalo lina majukumu ya ujenzi wa nyumba za kuishi, majengo kwa ajili ya kuuza kama itakavyoamuliwa na bodi, kujenga majengo kama sehemu ya mradi ulioidhinishwa na bodi na pia kutoa na kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya ujenzi kwa kuanzisha vifaa au njia nyinginezo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuangalia majukumu hayo ni dhahiri taasisi hizo zote mbili inakuwa ni kama wanashindana kwani wote wanajenga nyumba na wote wanauza nyumba. Hizi zote ni taasisi za Serikali ni kwanini zisiwe taasisi moja? Aidha, serikali ilibinafsisha viwanda karibia vyote vilivyokuwa vinatengeneza mali ghafi za ujenzi kama vile matofali, vigae na mabati. Sasa kama wanaamini sekta binafsi inaweza kufanyakazi ambazo ni majukumu ya serikali, na kwa kuwa taasisi hizo kwa sasa zinafanya biashara zaidi ni bora kazi za kujenga na kuuza nyumba zirudi kwenye sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu taarifa za hali ya uchumi wa taifa inaeleza kuwa wakala uliendelea kusimamia miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za viongozi ambazo ni za waheshimiwa Majaji mikoa ya Ruvuma,Dar Es Salaam,Tanga,Arusha,Tabora,Mwanza, Mbeya na Dodoma.
Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo inaendelea kueleza kuwa wakala uliendelea na ujenzi wa nyumba za wakuu wa Wilaya za Bariadi, Urambo na Siha pamoja na nyumba nyingine za viongozi wa Serikali Wilaya ya Kasulu.
Mheshimiwa Spika, katika Bunge la bajeti la mwaka 2011/2012 Kambi ya Upinzani ilihoji ni wilaya zipi ambako nyumba za DSO, DAS, OCD na DMO zingejengwa. Katika kitabu cha majibu ya hoja za waheshimiwa wabunge kilichotolewa na wizara ya ujenzi mwezi Agosti 2011 uk.14 kwenye hoja hiyo majibu yalikuwa, naomba kunukuu “Nyumba za DSO,DAS,OCD,na DMO zinajengwa katika Wilaya zifuatazo; Bahi 2 (OCD na DSO, Ukerewe 2 (OCD na DSO),Mvomero 1(DAS) na Kondoa 1 (Hakimu)”.
Kambi ya Upinzani inataka kupata majibu sahihi kuwa ni taarifa zipi sahihi kuhusiana na nyumba zilizojengwa na kusimamiwa na wakala wa ujenzi na haswa kwenye Wilaya. Je, ahadi hii ya serikali ilitekelezwa?
Mheshimiwa Spika, mbali ya usahihi wa takwimu kuwa na utata, inaonyesha kuwa wakala wa majengo umejikita zaidi kujenga nyumba za viongozi wakuu katika mikoa na wilaya na kuwauzia nyumba pindi wanapostaafu. Maana yake ni kwamba watumishi wa kada ya chini wao hawajengewi nyumba kama ambavyo niliainisha awali aina ya kada ya utumishi wa umma ambao wanahitaji sana kupatiwa nyumba wawapo katika utumishi na wamalizapo muda wa utumishi.
Mheshimiwa Spika, ukisoma randama ya wizara kasma 220703 inaonyesha kuwa kiasi cha shilingi 288,000,000 zimetengwa kwa ajili ya kulipia pango la ofisi Holland ambako wizara imepanga.
Kambi ya upinzani, inauliza hivi ni sahihi kweli kwa wizara ambayo imechukua jukumu la kujenga nyumba na ofisi za serikali kushindwa kuwa na jengo lake la ofisi na badala yake inapanga? Ni lini wizara hii itajenga jengo lake kwa ajili ya ofisi zake pamoja na taasisi mbalimbali zilizopo chini yake utaanza?

7.0 BARAZA LA TAIFA LA UJENZI
Mheshimiwa Spika, Baraza la Taifa la Ujenzi ni Taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria ya Bunge namba 20 ya mwaka 1979 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2008 (“National Construction Council Act, CAP 162, R.E. 2008”). Baraza lilianzishwa ili kusimamia maendeleo ya sekta ya ujenzi na pia kutoa uongozi mkakati unaolenga katika maendeleo ya sekta ya ujenzi kwa kutilia mkazo ukuzaji wa uwezo wa ndani.

Mheshimiwa Spika, moja wapo ya majukumu ya msingi ya baraza ni Kusimamia na kuongoza juhudi za kukuza na kuendeleza sekta ya ujenzi nchini Tanzania kwa kuzingatia ukuzaji wa uwezo wa ndani ya nchi ili kwenda sambamba na maendeleo na ushindani wa kimataifa; kusimamia na kuratibu maendeleo na utekelezaji wa viwango, kanuni na miongozo ya kiufundi inayohusiana na sekta ya ujenzi.
Mheshimiwa Spika, baraza linatakiwa kufanya ukaguzi wa kiufundi katika miradi ya ujenzi ili kupata maelezo kuhusu mwenendo na utekelezaji wa miradi ikiwa ni pamoja na mapungufu yaliyopo, na utatuzi wake. Ukaguzi unaweza kufanyika katika hatua yeyote ya mradi ikiwa ni pamoja na matayarisho ya utekelezaji, wakati wa utekelezaji na baada ya mradi kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa watumiaji wa barabara kuwa zinajengwa chini ya kiwango kiasi kwamba ajali nyingi chanzo chake ni ubora hafifu wa baraba. Kambi ya Upinzani inataka kuelewa hadi sasa toka kandarasi nyingi zilipoanza kazi ukaguzi umeishafanyika katika miradi mingapi ya barabara?

Uwezo wa Wahandisi Washauri
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kufanya uchunguzi wa kina wa makandarasi na wahandisi washauri wa ujenzi wa barabara ya Namtumbo-Tunduru juu ya uwezo na utaalam wao. Mheshimiwa Spika, inasemekana kuwa wataalam wengi katika mradi huo hawana sifa, hivyo basi ili kuondoa mashaka hayo, tunashauri uhakiki ufanyike katika mradi huo na miradi yote ya ujenzi wa barabara nchini na ikithibitika ndivyo hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao.
8.0 TEMESA
Mheshimiwa Spika, sambamba na matumizi makubwa ya Serikali katika posho mbalimbali, na mbali na kutokuwepo kwa sera madhubuti inayosimamia ununuzi na aina ya magari kwa kada mbalimbali katika utumishi wa umma, Serikali ina tatizo jingine kubwa la matumizi makubwa yasiyoratibiwa katika matengenezo na ununuzi wa mafuta ya magari. Kwa mujibu wa Ripoti ya Kiufanisi na Kiuchunguzi kama ilivyotolewa na CAG ya tarehe 31Machi, 2012 ni kwamba Wizara ya Ujenzi ndio yenye jukumu la kununua, kusajili na kufanya matengenezo ya magari ya Serikali, ikisaidiana na Wakala wake TEMESA (Tanzania Electrical, Mechanical and Electronics Services Agency).
Mheshimiwa Spika, taarifa ya CAG inaonesha kwamba Wizara ya Ujenzi haijaweka mfumo wa kusimamia matengenezo ya magari. Pia hakuna sera yoyote ya ununuzi na matengenezo ya magari na hivyo hakuna mwongozo toshelezi juu ya usimamizi wa ununuzi na matengenezo ya magari. Wizara haijatoa mwongozo kwa TEMESA juu ya hatua na michakato ya kufuata na wala Wizara haisimamii utendaji wa TEMESA ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, Wizara pia haina kumbukumbu za kila wakati kama chombo cha usimamzi wa matengenezo ya magari. Mfumo wa matengenezo ya magari ya Serikali hausimamiwi ipasavyo na TEMESA kwa kuwa magari ya Serikali hayakaguliwi kabla na baada ya matengenezo.
Mheshimiwa Spika, mapungufu haya ya Wizara na TEMESA katika kusimamia matengenezo ya magari ya Serikali kunapelekea Serikali kupoteza fedha nyingi sana kwani licha ya kuwa hakuna usimamizi wa kutosha lakini pia hakuna taarifa au kumbukumbu za matengenezo ya magari na gharama zake.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasikitishwa na matumizi makubwa ya fedha za walipa kodi kwa matengenezo ya magari ya Serikali ambayo hayana usimamizi madhubuti. Gharama kubwa sana inatumika kwa mafuta na matengenezo ya magari.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunaitaka serikali ieleze ni lini itakamilisha sera ya ununuzi na matumizi ya magari ya serikali na kuanza kutumika ili kuliepusha taifa na hasara ambayo inaweza kuepukika.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi ya Upinzani,
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.


…………………………………….
Said Amour Arfi (Mb)
Msemaji Mkuu Kambi ya Upinzani- Miundombinu
5.07.2012

No comments: