Tuesday, June 19, 2012

WASIFU WA WILLY EDWARD - ALIYEKUWA MHARIRI WA JAMBO LEO

Willy Edward Daniel Ogunde ambaye alikuwa Mhariri Mkuu wa gazeti la Jambo Leo alizaliwa Machi 7, 1974 katika Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Alisoma shule ya msingi Mapinduzi mwaka 1983 hadi 1989 kisha elimu ya Sekondari katika shule ya Serengeti mwaka 1990 hadi 1993.Baadaye alijiunga na shule ya Sekondari Musoma kidato cha tano na sita mwaka 1994 na 1995.

Mwaka 1996 alijiunga na Kampuni ya uchapishaji wa magazeti ya BTL akiwa mwandishi wa gazeti wakati huo likiitwa Majira Jioni.
Akiwa na kampuni hiyo alipata mafunzo mafupi ya kikazi yakiwemo ya kompyuta na ya uandishi wa habari.
Mwaka 1998 alihamishwa kitendo kutoka kwenye gazeti la Majira Jioni kwenda kwenye gazeti jipya la Dar Leo na kuwa mwandishi wa habari wa hazeti hilo lakini pia akishikilia nafasi ambazo alikuwa akizitumikia kwenye gazeti la Majira Jioni.
Alifanikiwa kuaminika na kutokana na uwezo wake kazini alipanda daraja na kuwa Mhariri wa gazeti la Dar Leo kuanzia mwaka 2002 hadi 2005.
Kipindi cha mwaka 2006 hadi 2007 alikuwa akitumikia nafasi ya Mhariri wa Msaidizi wa Michezo gazeti la Majira na baadaye 2006 hadi 2007 akawa Mhariri wa Michezo wa gazeti hilo .
Mwaka 2006 hadi 2007 alipata cheti cha elimu ya uandishi wa habari katika Chuo cha Ceylon (CSJ).
Amesafiri nchi mbalimbali duniani katika kuripoti habari za michezo na burudani ikiwemo Afrika Kusini mwaka 2003 hadi 2006 kwenye mashindano ya Big Brother Africa.
Pia mwaka 2007, 2008 na 2009 Kenya, Senegal na Uingereza kuripoti habari za michezo kupitia Super Sport.Mei mwaka huu alisafiri kwenda nchini Uturuki kwenye kongamano ya wadau wa masuala ya mawasiliano ambako alikuwa kiongozi wa wahariri waliotoka Tanzania na kutoa mada kw iliyohusu mwenendo wa vyombo vya habari nchini Tanzania.
Nje ya kazi ya uandishi wa habari mwaka 2008 na 2009 alifanya kazi katika kampuni ya matangazo ya ZK akiwa Ofisa Habari na Uhusiano.
Miongoni mwa vyombo vya habari ambavyo aliwahi kufanya kazi enzi za uhai wake ni pamoja na Kampuni ya New Habari ambayo aliitumikia mwaka 2007 na 2008 akiwa Mhariri Msaidizi wa gazeti la Bingwa.
Hatimaye mwaka 2008 alikuwa Mhariri Mkuu wa gazeti la Bingwa kabla hajaacha kazi katika kampuni hiyo na kujiunga na Kampuni ya ZK.
Alijiunga na gazeti la Jambo Leo mwaka 2010 akiwa Mhariri wa Habari na kuanzia mwaka jana hadi mauti ilipomkuta alikuwa Mhariri Mkuu wa gazeti la Jambo Leo.

No comments: