Wednesday, June 20, 2012

WAFUASI WA UAMSHO KIZIMBANI

WATU 33 wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa Jumuiya ya Mihadhara ya Dini ya Kiisilamu ya UAMSHO, jana walifikishwa katika mahakama ya wilaya Mfenesini wakikabiliwa na mashitaka ya kufanya mkusanyiko isivyo halali.
Watuhumiwa hao wakiwemo wanawake nane, wanaume 25 na watoto wawili wa miaka 15 na 17 walidaiwa kutenda kosa hilo juzi huko Donge wilaya ya Kaskazini 'B' Unguja, wamefikishwa mbele ya hakimu Fatma Muhsin Omar kujibu mashitaka hayo.

Pamoja na shitaka hilo, watuhumiwa hao pia walishitakiwa kwa kosa la kukataa amri ya kutawanyika, mashitaka ambayo yaliyasilishwa na Mwendesha Mashitaka wa mahakama hiyo Mkaguzi wa Polisi Khamis Abdulrahman.

Akiwa mahakamani hapo, Mwendesha Mashitaka huyo aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Muhammad Nyange Haji (28) Mkwajuni, Idd Makame Alawi (36) Chumbuni, Juma Pandu Salum (30), Kassim Abdulrahman Abdallah (30) Mbweni pamoja na Juma Faki Juma (27) Chumbuni.
Wengine ni Mohammed Juma Jongo (30) Sogea, Khamis Humoud Khamis (39) Magomeni, Khamis Ali Suleiman (59) Mwanakwerekwe, Salum Shaabani Hamadi (18) Amani, Mussa Hassan Haji (15) Magomeni, Suleiman Abdallah Khamis (32) Mwanakwerekwe, Seif Adinani Seif (31) Mwanakwerekwe na Mohammed Najim Suleiman (23) Darajabovu.
Watuhumiwa wengine ni Khamis Ali Jamali (28) Bububu, Mohammed Salum Bakari (27) Nyerere, Mussa Hamadi Mussa (32) Magomeni, Othman Ali Khamis (22) Tomondo, Kassim Shehe Khamis (5) Mahonda, Kheri Jecha Kheri (21) Donge, Shukuru Pembe Juma (20) Donge, Khamis Juma Ali (38) Donge na Machano Omar Amour (27) Bumbwini.
Watuhumiwa wengine waliotinga katika kizimbani hapo ni Ali Haji Makame (45) Fukuchani, Nahoda Haji Ussi (60) Donge, Jabu Simai Sharif (17) Mkwajuni, Riziki Omar Chande (42) Mfenesini, Halima Ali Kassim (38) Bububu na Zuhura Salum Said (23) Amani.
Wengine ni Mtumwa Haji Omar (47) Kianga, Maryam Mohammed Bakari (30) Amani, Khadija Salum Juma (23) Darajabovu, Hafsa Mohammed Mahfoudh (19) Kinuni na Saada Ali Ramadhani (28) Jang'ombe.
Wote hao walidaiwa mahakamani hapo kwamba, kinyume na vifungu vya 55 (1) na 56 cha kanuni ya adhabu sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar, walipatikana wakiwa wamekusanyika isivyo halali kwa dhamira ya kutenda kosa.
Sambamba na shitaka hilo, pia walidaiwa kukataa amri ya kutawanyika mara baada ya kuonywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kufanya hivyo, kitendo ambacho ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 60 cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.

Mahakama iliambiwa kuwa, matukio yote hayo yalitokea Juni 17 mwaka huu baina ya saa 9:45 alaasiri na saa 10:35 katika maeneo ya Mahonda na Donge wilaya ya Kaskazini 'B' Unguja.

Wakati watuhumiwa 32 wakikana mashitaka hayo, mshitakiwa Ali Haji Makame hakuwepo mahakamani hapo licha ya kusomewa shitaka hilo, na habari zilizoelezwa mahakamani hapo zimedai kuwa amelazwa hospitali kwa ajili ya matibabu.
Watuhumiwa wote hao wanasimamiwa na Wakili wa Kujitegemea Suleiman Salim Abdallah, ambaye aliiomba mahakama hiyo iwapatie wateja wake dhamana kwa masharti nafuu yatakayoweza kutekelezeka, ombi ambalo halikupingwa na upande wa mashitaka.
Akikubaliana na hoja hizo, hakimu Fatma Muhsin Omar aliwataka watuhumiwa hao kila mmoja kujidhamini kwa bondi ya shilingi 100,000 pamoja na kuwasilisha wadhamini wawili wenye vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, ambao kila mmoja atasaini bondi ya kiwango kama hicho cha fedha.
Upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, upande wa mashitaka uliiomba mahakama hiyo kuiarisha na kuipangia tarehe nyengine kwa ajili ya kutajwa, ili kupata muda zaidi wa kukamilisha upelelezi huo, ambapo hakimu Fatma aliiahirisha hadi Julai 2 mwaka huu kwa kutajwa.
CHANZO :- zanzibarnews blog

No comments: