Tuesday, June 19, 2012


MAONI YA KAMATI YA KUDUMU YA BARAZA LA WAWAKILISHI YA WENYEVITI WA KAMATI ZA KUDUMU ZA BARAZA KUHUSU MAPITIO YA HALI YA UCHUMI NA MPANGO WA MAENDELEO (2011/2012) NA BAJETI YA SERIKALI KWA   MWAKA 2012/2013 

Mhe Spika, Kwanza sote hatuna budi kumshukuru M/Mungu kwa kutujaalia kukutana tena katika kuwatumikia wananchi wetu waliotuchagua tukiwa wazima kabisa na wenye afya njema. Pili, nikushukuru na wewe mwenyewe Spika wetu mpendwa kwa kunipa nafasi ya mwanzo kuwasilisha ripoti yetu ya kamati ya Wenyeviti wa kamati za Baraza lako tukufu la Wawakilishi hapa Zanzibar. 
Ili kuichangia Hotuba ya Bajet ya SMZ iliyowasilishwa na kipenzi chetu Waziri wa Nchi Fedha na Uchumi na Maendeleo Zanzibar, Tatu, niwashukuru Wajumbe wote wa Baraza hili la Wawakilishi kwa kutupa dhamana ya kuwa wenyeviti wa kamati na leo tunawasilisha ripoti hii kwa niaba yao wote, 
Nne, nawashukuru wananchi wote Zanzibar kwa kutuamini na kutupa dhamana ya kuwatumikia ndani ya chombo hiki ili kulinda maslahi yao hapa Zanzibar. Pia tunawashukuru wafanyakazi wote wa Baraza lako la Wawakilishi hapa Zanzibar kwa kwa msaada na huduma wanazotupatia wakati wote tunapohitajia tunaomba waendelee na moyo huo huo, Mwisho, shukurani kubwa zaidi kwa waandishi wote wa Habari ,wa TV,Magazeti, Radio, Wapigapicha na wengine wote kwa kutuwezesha kufikisha habari zetu kwa wananchi wote tunawashukuru sana kwa hilo.

Mhe Spika, kamati yangu ilipitia Bajeti ya SMZ na iltoa maoni mbali mbali kwa Serikali ili kuiboresha na leo pia tutaongezea michango zaidikama itakavyofuata muda huu. Aidha naomba niwashukuru kwa dhati Wajumbe wote wa Kamati yetu kwa michangoyao ya kina waliyoitoa wakati Kamati yetu ilipokuwa inaijadili hoja hii. Napenda niwataje Waheshimiwa Wajumbe haokama ifuatavyo:-

1.      Mhe. Hamza Hassan Juma                   - Mwenyekiti

2.      Mhe. Ali Abdalla Ali                            - Mjumbe

3.      Mhe. Asha Bakar Makame                   - Mjumbe

4.      Mhe. Amina Idd Mabrouk                   – Mjumbe

5.      Mhe. Makame Mshimba Mbarouk       – Mjumbe

6.      Mhe. Omar Ali Shehe                         - Mjumbe

7.      Mhe. Salmin Awadh Salmin                 – Mjumbe

8.      Ndg. Nasra Awadh Salmin                  – Katibu

9.      Ndg. Ramadhan Kh. Masoud               – Katibu

Mhe Spika, tunaungana na kauli ya Mhe Waziri, kwa Serikali kutimiza matakwa ya katiba (Kif. 105) kwa kuwasilisha Bajeti kuu ya SMZ huu ndio utekelezaji wa utawala bora,kama MKUZA Klasta ya tatu inavyoeleza suala la Utawala Bora, kwani sote tunatakiwa kufuata katiba. Kwa hiyo pia tunaitaka Serikali kutekeleza (kif.61 (2) cha katiba kinachotaka kuteuliwa kwa Wakuu wa Mikoa na kabla ya kuanza kazi zao ni lazima wale kiapo cha kuitii katiba inayoiongoza nchi, kwa kua leo tunapitisha matumizi ya Serikali na wao wakiwamo katika Utumishi wa Umma basi ni vyema Katiba itekelezwe kama inavyo taka vinginevyo hata wananchi wetu hawataitii Katiba na Sheria tunazozitunga sisi wenyewe, kwani hakuna aliye juu ya Sheria.

Mhe Spika, kamati yangu inampongezasana Mhe Rais wa Zanzibar, Dkt. Mohammed Ali Shein kwa kuendelea kutuongoza kwa amani na utulivu hapa nchini. Pia tunampongeza Waziri wa Nchi (OR) Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo kwa kuwa muelewa na msikivu kwa hoja zetu nyingi hasa tunapoishauri Serikali zaidi katika mianya ya ukwepaji kodi na uvujaji wa mapato ya Serikali na matunda yake tumeanza kuyaona ingawa kwa kasi ndogo kwani taasisi za kodi zimevuka malengo waliojiwekea lakini bado kuna baadhi ya maeneo yanahitaji kuwekewa mkazo ili kuziba kabisa uvujaji wa mapato ya Serikali. Lakini pia bado kuna maeneo machache Serikali yetu haikusanyi mapatokama Katiba ya Jamhuri ya Muungano inavyosema. Mapato ambayo yangelisaidia katika uchumi wetu.

Mhe Spika, leo kwa mshangao mkubwa tumekuja hapa kuidhinisha ukusanyaji na kuruhusu matumizi ya pesa nyingine za Umma, kwa shughuli za uendeshaji na maendeleo ya wananchi wakati baadhi ya wasimamizi wa pesa hizi tayari kupitia ripoti za kamati ulizoziunda wewe mwenyewe zimegundua usimamizi mbovu na uvujaji wa mapato wakiwa wao ndio wasimamizi wakuu katika sehemu zao, na taarifa zao tumekuletea wewe Mhe Spika, na tayari umeziwasilisha Serikalini zikiwa na ushahidi kamili hadi leo hatujapokea taarifa yeyote na wala hatujaona hatua zozote zilizochukuliwa na Serikali, sasa nakuuliza wewe Mhe Spika, je zile taarifa tulizokuletea wewe hukuziamini? Au Serikali haikuziamini? Na kwa kua kanuni zetu hapa Barazani zinatukataza kusema uongo je kuna maelezo yeyote tuliyoletewa kutoka Serikalini kuwa tumelidanganya Baraza? Mhe Spika, sisi Wajumbe wako kwa mujibu wa katiba yaZanzibar ya mwaka 1984 kif. Cha 4  Baraza la Wawakilishi limepewa dhamana ya kuisimamia Serikali, kuihoji na kuielekeza lakini sasa inaonyesha ni kinyume chake kuwa sasa Serikali ndio inalisimia Baraza la Wawakilishi na wanaweza kufanya lolote kwa kuamini kuwa hatuna uwezo wa kufanya chochote, hii inawapa Watendaji wa Serikali jeuri na kibri kwani hawajali chochote na wanaweza kufanya lolote dhidi ya Baraza kwani Serikali itawalinda.

Mhe Spika, mimi nasikitika sana kuwa ulimega sehemu ya fedha ulizotengewa na Serikali katika bajeti yako na kuwalipa wajumbe wako ili wakachunguze uzembe na ubadhirifu unaofanyika ndani ya taasisi za Serikali na wamegundua mambo mengi tena kwa ushahidi wa vielelezo vya maandishi na kinasa sauti ili kulinda uadilifu na fedha walizotumia wajumbe hao na kodi ya wananchi, na leo tuko hapa tena tunaendelea  kutumia kodi za wavujajasho hao hao wananchi wa Zanzibar lakini mawazo, fikra na maamuzi tunayoyafikia hadi sasa hatujaona dalili ya uwajibikaji kwa wahusika.


Mhe Spika, tunaombasana Serikali yetu kuifuata katiba na Sheria tulizozitunga sisi wenyewe na sote tulikula kiapo kwa kukamata msahafu, naombasana Mhe Spika, tuwajibike kwa pamoja, tuache muhali, kuoneana haya kila mmoja awajibike kwa nafasi yake kwa uadilifu vinginevyo tutaendelea kutambaa badala ya kutembea.

Mhe Spika, hii ndio Bajeti ya Serikali tunaidhinisha tena matumizi kwa baadhi ya watendaji ambao hatuna imani nao kuendelea kusimamia taasisi walizoshindwa kuzisimamia, aidha kwa kukiuka maadili ya dhamana waliopewa, au ubadhirifu katika taasisi zao, tunaiomba Serikali kuchukua hatua za dharura kuhusu suala hili ili na sisi tuamini kuwa kweli sote nia yetu kuijenga nchi yetu na sio kuwalinda watu. Vinginevyo itakuwa ni sawa na kutia maji kwenye pakacha.

Mhe Spika, kwa kua kuna baadhi ya matumizi hasa ya Maendeleo na mengine ya kawaida tayari kunabaadhi ya wizara aidha wametumia kinyume na walivyotuahidi, na baadhi yao pia tumegundua wamekusanya pesa za umma na kuzitia mifukoni mwao sasa na leo bado tena Serikali inataka tuenedelee kuwaamini watu wao hao wakakusanye nyingine na kama kawaida yao wakazitafune tena, ah! Nadhani hata wananchi wetu watakosa imani na sisi, sasa Mhe Spika, naomba utumie busara zako kuilekeza Serikali ipasavyo ili tutekeleze matakwa ya katiba yaZanzibar kuhusu ubadhirifu wamali za Umma na nini kifanyike kabla ya kuipitisha Bajet hii.

Mhe Spika, Serikali yetu inaongozwa na CCM  na chama Chetu kinapiga vita kwa nguvu zote ubadhirifu wa aina yeyote au ufujaji wa pesa za Umma, pamoja na Rushwa, sasa siamini kama kuna mtu yeyote atakaekwenda kinyume na matakwa hayo ya Chama chetu ambacho ndicho kinachoongoza Nchi kwa sasa.

Mhe Spika, kamati yangu pia inaungana na Serikali kuwapa pole wananchi wetu wote waliopatwa na janga la kuzama kwa meli ya MV SPICE ISLANDER iliyozama siku ya Tarehe 10/06/2012 kwa uzembe uliosababishwa na tamaa na kutowajibika kwa viongozi wakuu wa Wizara ya Miundombinu katika kusimamia majukumu yao kwa kujua kuwa chochote kitakachotokea wao hawatoathirika kwa lolote (BUSSINESS AS USUAL) Mhe Spika, kamati yangu inasiskitika kwa wajumbe wako walipozuiwa na Serikali kuzungumzia tukio lile hapa Barazani baada ya kuzama kwa Meli ile eti kwa kwa sababu kumeundwa tume, wakati kanuni zetu hapa Barazani hazituzuii kuzungumzia jambo lolote isipokuwa suala hilo liweko Mahakamani, haya ndio baadhi ya yale niliyoyazungumza mwanzo kuwa Serikali ndio inayolisimamia Baraza la Wawakilishi badala ya Baraza kuisimimia Serikali, kama kawaida na kwa hivi sasa wakati tume hiyo  ilipomaliza kazi yake haraka suala hilo likapelekwa Mahakamani kwa hiyo hivi sasa pia kwa mara nyingine tena hatuwezi kulijadili tena kwa kua liko Mahakamani, lakini tukitaka tusitake wananchi wetu wengi wameathirika kutokana na tukio lile,wengi wao wamebaki Mayatima, Wajane, Wagonjwa, na wengine kupoteza Mali zao na hakuna njia ya kuwarejeshea mali zao kwa fidia ya aina yeyote, ingawa waliohusika wanaendelea kupiga tai, wao na familia zao, lakini kwa taarifa tulizozipata ambazo Serikali haikututhibitishia kuwa Tajiri mwenye Meli yeye tayari alikwishakulipwa na Bima na nnadhani hivi sasa anatafuta Meli nyengine, Mhe Spika, hii inatupa fundisho sisi wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Kuleta Mswada wa  Sheria zitakazowalinda wananchi wetu wakati zinapotokea ajali ili na wao waweze kupata fidia kisheria sio ilivyo hivi sasa kufikiriwa tena kama kipo hicho cha kufikiriwa. Kwani sisi hapa wametuleta wao na tunapaswa kutunga Sheria za kulinda maslahi yao na ni vyema kuwalipa fadhila zao.

Mhe Spika, Pato la taifa kweli tunakubali limekuwa kwa mwaka unaomalizika na kipato cha mwananchi kimekuwa, na kama ilvyoelezwa na waziri, hasa kutokana na kupanda kwa bei ya karafuu na kuongezeka kwa watalii kumesaidia sekta ya huduma kuimarika kwani utalii unatija kwa njia tofauti huongeza kipato na ajira kwa wananchi, Lakini pamoja na kipato cha mwananchi kukua hakiendani na kasi ya mfumko wa bei za bidhaa kuanzia chakula na vifaa vya ujenzi n.k, Mhe Spika, pamoja na bei ya karafuu kupanda lakini sio watu wote wanayo mikarafuu, kwani ukiangalia hata hiyo mikarafuu iko zaidi katika baadhi ya mikoa tu ya Zanzibar wazanzibari mazingira yao ya kiuchumi yanatofautiana sana. Kuhusu kuongezeka watalii hapa tunapata fundisho sote wazanzibari kulinda amani iliyopo kwani zikianza vurugu hapa nchini kwetu basi hao watalii hawatokuja kupunguza mapato yetu.

Mhe Spika, kukua kwa pato la taifa pia kunatokana na kuongezeka Miradi ya Uwekezaji ikwemo ujenzi wa Barabara, Viwanja vya ndege, Ujenzi wa Maskuli, Mahoteli, Viwanda n.k, lakini bado haturidhiki na kasi ndogo ya ujenzi  wa miundombinu hasa barabara, hatuelewi tatizo nini kwani miradi yote kabla ya ujenzi hufanyiwa Upembuzi Yakinifu na zinapototolewa Tender kila kitu kinajieleza, kitu cha kushangaza kuna barabara tena za kilomita chache zimeanzwa kujengwa tangu mwaka 2008 hadi leo bado hazijakamilika, na zilitolewa ahadi zingelimalizika kabla ya uchaguzi mkuu uliopita hasa barabara zinazosimamiwa na Kampuni ya MECCO, na hivi sasa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar, unajengwa, unasimama, nao hatujui utamaliza lini kwani tunaelewa mradi wowote ukisimama kuna mambo mengi yatatokea, ikiwemo upotevu wa vifaa, kuongezeka bei za vifaa vya ujenzi toauti na bei iliyopangwa mwanzo n.k.

Mhe Spika, mfumko wa bei wa 14.7 mwaka unaomalizika unatishia amani ya uhai wa wananchi wetu, tumeshuhudia bidhaa za chakula kupanda ingawa Waziri ametupa moyo kuwa kwa mwaka huu mfumko wa bei utashuka lakini mimi sikubaliani nae sana kwani tayari katika Bajeti yake ametangaza kuongeza kodi katika bidhaa ya Mafuta baada ya bajeti, kwa hiyo ni dhahiri na bei ya usafirishaji itaongezeka, na bei za bidhaa zitapanda, lakini isitoshe kinachotutia hofu zaidi  ni kuendelea kwa mvutano unaoendelea baina ya Marekani na Iran kuhusu uzalishaji wa Nuklia na tishio la kuwekewa vikwazo Iran kuhusu kuuza Mafuta yake inatishia kupanda kwa mara nyengine bei ya Mafuta Duniani na kusababisha bidhaa nyingi kupanda bei ambapo liko nje ya uwezo wetu, Mhe Spika, Jingine ni kupanda kwa bei ya Umeme imeongeza ugumu wa maisha ya wananchi wetu wakiwemo wafanyakazi wa serikali na wanachi wengine kwani umeme kwa hivi sasa ni jambo la lazima kwa maisha yetu na kutokana na Serikali yetu kuwa na uhaba wa vianzio vya mapato imeshindwa kufidia gharama hiyo kwani vitu kama hivi vya maisha ya kila siku Serikali inabidi iangalie namna ya kuwapa wanachi unafuu ili kuweza kukabiliana na kasi ya maisha. Lakini hapa Serikali naomba iangalie upya ongezeko hilo kama kweli linasababishwa na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji au kufidai wizi na ubadhirifu usio na kificho unaofanywa na watendaji wachache wa Shirika la Umeme wasioitakia mema nchi yetu kwa maslahi yao binafsi,

Mhe Spika, kwa kua sisi Wajumbe wako kama kawaida yetu tukiona wizi tunasema katika Shirika la Umeme kuna wizi tumeugundua na wakati huo huo wamechukua hatua ya kupandisha bei ya Umeme kwa wananchi sasa sisi tunaamini wamechukua hatua hiyo ili kuziba pengo la pesa walizoziiba wao sio wananchi, kwa hiyo tunaitaka Serikali kusitisha mara moja ongezeko hilo la bei ya Umeme ili kwanza kupitisha uchunguzi wa kitaalam atafutwe mtaalam nje ya Shirika afanye tathmini ya kujua je ongezeko hilo la bei ya Umeme ni sahihi au ni moja katika njia za kuziba pengo hilo, pili kwa kua wajumbe wako tumegundua kuwa kuna baadhi ya wafanya biashara wakubwa hapa Nchini wanakwepa au hawalipi Umeme na wanadaiwa pesa nyingi je! kuna utaratibu gani wa kulipa pesa hizo kuanzia siku waliyoungiwa Umeme huo? Kwani imani yetu wao ndio wanaosababisha kuongezeka kwa bei ya Umeme sisi tunasema hii sio haki kua ubadhirifu ufanywe na watu wengine na adhabu ya kulipa wapewe watu wengine. Huko nje wananchi wetu wote wanapiga kelele kupandishwa bei ya Umeme, wakati huku sisi tumekuja hapa na tunapitisha Bajeti ili wakaendelee kuiibia Nchi na hakuna hatua inayochukuliwa na Serikali kwani wameshazoea kufanya hivyo, lakini Kwa hili Mhe Spika, sisi tunakuahidi hatutokuwa rahisi kulikubali hata kidogo kwani mchezo wao ndio mauti yetu Serikali iwe makini katika hilo naomba watuelewe.

Mhe Spika, miongoni mwa mambo yaliyosababisha mfumko wa bei ni kushuka kwa thamani ya T/shs kwa USD na kwa kuzingatia chombo kinachodhibiti mfumko wa bei ni chombo kimoja yaani Benki Kuu ya Tanzania (B.O.T) inayosimamia Serikali mbili zenye chumi tofauti lakini zinazotoza kodi za aina moja bila ya kuangalia vianzio vya mapato ya nchi na rasilimali zilizopo katika nchi hizo na uhuru au vikwazo vya kuzitumia rasilimali hizo,  na ushahidi kama nilivyosema kwenye bajeti ya mwaka uliopita kuwa chombo hicho kilitoa msaada wa fedha taslim kwa makampuni karibu 90 ya T/Bara kutokana na mtikisiko wa kiuchumi Duniani ili makampuni hayo yasitetereke wakati hakuna hata kampuni moja ya Zanzibar iliyopata hata senti moja, eti kwa kisingizio kuwa Zanzibar hakuna kampuni iliyoathirika kwa mtikisiko huo, kwa hiyo Mhe Spika, naomba sana chombo hichi kiangalie sana uchumi wa Zanzibar na maisha ya watu wake, kwani kutokana idadi ya watu hata soko kwa wafanya biashara walioko Zanzibar ni dogo kutokana na idadi ya wake  kuwa ni kidogo kulinganisha na walioko T/Bara, sasa kwa hiyo hata mauzo kwa mfanyabiashara alioko T/Bara yatakuwa ni makubwa kulinganisha na ailyeko Zanzibar, kwa tathmini ya utaalam wa Kikwamtipura, hata ukichukulia muuza maandazi aliyeko T/Bara atakuwa na uwezo wa kuuza maandazi kwa wateja wengi kulinganisha na yule wa Zanzibar kutokana na idadi wa wateja walioko hapa, sasa leo hebu tujiulize inakuwaje kodi kwa nchi zetu hizi ziwe sawa? Mfano mwengine ni hata kwa mkulima aliyeko Zanzibar uwezo na ardhi ailiyonayo na ndogo kulinganisha na aliyeko T/Bara kwa hiyo hata mavuno atakayoyapata yatakuwa tofauti kubwa kwa hiyo mkulima aliyeko T/Bara anaweza kujikomboa na umasikini kwa asilimia 80 lakini mkulima aliyeko Zanzibar uwezekano wa kujikomboa na umasiskini asilimia 20 tu, Mhe Spika kwa  vigezo hivi hakuna haja ya kumtafuta mshauri muelekezi kutoka Ulaya kwani huyu wa Kwamtipura anatosha kabisa.


Mhe Spika, haya nimeyasema ili kuwafahamisha wale wanaopanga Mipango ya Maendeleo kwa Jamhuri ya Muungano waTanzania kujua hali ya maishayao tofautisana baina ya ZNZ na T/Bara, kwani hata ukianagalia bei ya bidhaa zote muhimu kwa maisha yetu ya kila siku hasa chakulaZanzibar bei iko juu. Kwani bidhaa nyingi sisi tunaagizia kutoka T/bara, kwa hesabu za haraka haraka mtumishi wa Serikali wa Zanzibar  anaepokea kima cha chini ambao ndio wengi, anapokea Mshahara kiasi laki moja na nusu inamaana kwa siku atumie elfu tano, kuanzia Chakula, mavazi, matibabu, makaazi, Umeme, Maji, Usafiri, kusomesha watoto, n,k  ukiangalia na sisi ndani ya Baraza hili tutapitisha Sheria ya marekebisho ya kodi mbalimbali ni vyema tukaangalia na ugumu wa maisha kwa wananchi wetu. Sasa hiyo nimeelezea kwa mfanyakazi wa Serikali tu lakini  wananchi wetu wa Zanzibar na wengi wao wanaishi katika Majimbo yetu likiwemo Jimbo langu la Kwamtipura ambao hawana kazi za uhakika za kupata hata hiyo laki moja na nusu kwa mwezi je maisha yao yatakuwa hali gani ,kwa hiyo tunaiomba Serikali yetu kutafuta namna yeyote ili kuweza kuzitumia Rasilimali zilizoko Nchini kwetu ili ziwanufaishe wananchi wetu, kwa kuwapa unafuu wa maisha yao.

Mhe Spika, Sekta ya fedha ni kweli imeimarika lakini hebu tujiulize ni asilimia ngapi ya wananchi wetu wanaitumia na kufaidika na sekta hiyo? Kwa haraka utaona zaidi ni wafanyabiashara tena wachache ndio wanaofaidika nayo ikiacha wengi wasiofaidika moja kwa moja. Wafanya biashara wadogo wengi wao hawafaidiki na mikopo kutokana kukosa dhamana, na hao ndio walio wengi na ndio maana wengi huwa hawaoni umuhimu wa kuweka fedha zao benki. Ingawa wafanyakazi wa Serikali na Mashirika labda wao ndio hufaidika na mikopo ya Benki na wamesaidia sana Mabenki hapa nchini kutengeneza faida kubwa lakini mabenki hayo bado yameshindwa kuwapunguzia riba kubwa inayowatoza kwani wao ni wateja wenye Guarantee ya waajiri wao hakuna njia ya kukimbia kulipa deni kwa hiyo kama Mwaka uliopita tunakuomba Waziri ukae na Watendaji wakuu wa mabenki kuwapa kilio cha wafanyakazi wetu hawa ili kuwapunguzia riba na wao kwakua wanaweka pesa kwao pia ni sehemu ya wabia wao.

Mhe Spika, Pia tunaitaka Serikali kuyashawishi Mashirika ya kujenga Nyumba za kuwakodisha na kuwauzia wananchi pamoja na mabenki ya kutoa mikopo ya ujenzi wa nyumba ili kuwawezesha wananchi wetu kupata makaazi yaliyo bora. Kwani tumeona kwa sasa kwa wenzetu wa T/bara tayari Shuirika la Nyumba wameanza kujenga Nyumba za Makazi ili kuwauzia au kuwakopesha watumishi wa Serikali ya Jamhuri ya MuunganoTanzania. Pia Mabenki nayo yameanza kutoa mikopo kwa watumishi hao ili waweze kuzinunua kwa fedha taslimu au kwa mkopo nyumba hizo.

Mhe Spika, kwa lengo la kuongeza mapato, Waziri ameeleza kuwa Serikali imekusudia kurekebisha kodi ya Lease ya Ardhi, ili kuendana na thamani ya soko la Ardhi ilivyo hivi sasa lakini kamati yangu haijaridhishwa na utaratibu wa utozwaji wa kodi za Lease kwa Ardhi za Serikali kwani kuna ubabaishaji mkubwa uliofanywa na Wizara ya Ardhi kwanza kufuta ovyo Lease zilizotolewa na Serikali na baadhi yao kulipishwa kodi ndogo ikilinganishwa na ile iliyokuwa ikitolewa hapo mwanzo Mhe Spika,tunaushahidi wa baadhi ya risiti za kodi zilizokuwa zikilipwa mwanzo ambazo baadhi yao zikilpwa kwa Dola 11,000 na kupewa mtu mwengine ambae ametakiwa na Wizara kulipia Dola 3,000 ,  kuna tofauti karibu  Dola 8,000 karibu T/shs 12,Mil kwa lease moja tu na hizi ziko nyingi tutakuletea Mhe Spika, tena hiyo ni Lease moja tu sasa angalia Mhe Spika, huu kama si  ufisadi ni kitu ganikweli tutamuamini mtu gani Serikalini hivi sasa?  Tatizo hili la watu kupokonywa ardhi na kupewa watu wengine ambao hulipa kwa bei ya chini limeenea katika maeneo mengi ya nchi yetu. Hivyo, lease ya Ardhi hizo lazima zifutwe mara moja na Ardhi hizo zirudishwe Serikalini mara moja, ili ziwanufaishe wananchi. Kila siku Serikali inawaongezea kodi wananchi wakati pesa za kodi za rasilimali ya nchi zipo zinaachiwa na kuliwa na watu wachache tena wenye Dhamana kubwa Serikalini huku wanakamuliwa walala hoi yaani wananchi wetu.

Mhe Spika, wakati umefika sasa rasilimali tulizojaaliwa na M/mungu  kwanza tuzitumie hizo na kama hazitoshi kutuendesha nchi yetu na kama hazitoshi ndio tuwakamue wananchi wetu, leo Wazee wetu wanaoishi Majumba ya Waezee Sebleni tunajisifu tunawalipa shs 40,000/=  kwa mwezi wakati pesa za kuwalipa vizuri tunazo lakini tunashindwa kujipangia matumizi sahihi kwa tamaa ya watu wachache.

Mhe Spika, vianzio vya mapato, tumeona mapato kwa mwaka uliopita yameongezeka  kutoka Shs 109.6 Bil hadi 120.4 Bil.mimi sijaridhikasana na kima hicho kwani ninazo taarifa kuwa kuna baadhi ya watendaji wa ZRB wanashirikiana na wafanya biashara na wawekezaji wachache kuiibia na kuikosesha mapato Serikali. Suala hili nikishalithibitisha nitakuja kuliripoti Barazani ili kulifanyia kazi hivi, sasa ni mapema mno kwani kanuni zako zinatutaka jambo tunaloliwasilisha hapa ni lazima liwe na uhakika na nikikamilisha ushahidi basi sitasita kujakukuomba kulifanyia kazikama tunavyoendelea kufanya hivi sasa kwa maslahi ya wananchi wetu.

Mhe Spika, kwa upande wa TRA-Zanzibar kamati yangu inawataka watendaji kujitahidi kudhibiti uvujaji wa mapato kwani pia hatujaridhika na utendaji wao kwani pia ninazo taarifa kuwa kuna baadhi ya watendaji kutoka Mamlaka ya Mapato hasa Bandarini kuwa wanashirikiana na Baadhi ya Wafanyabiashara wakubwa wanaoleta bidhaa hapa Zanzibar kukwepa kodi na kuibia Serikali na kuikosesha  mapato, na Mhe Spika, kwa mtindo huu uliokuwepo kwa Serikali yetu kushindwa kuwachukulia hatua za kuwawajibisha wabadhirifu wanaogundulika kuiibia Serikali,  mchezo huu utaendelea kila kukicha hasa ukizingatia hofu tulionayo sisi wajumbe wako Wawakilishi wa wananchi kutokujiamini katika kutekeleza majukumu yetu kwani tumeshindwa kujua kuwa sisi ndio tunaopaswa kuiwajibisha Serikali kutokana na uzembe na wizi unaofanywa kwa mali na rasilimali za umma.

Mhe Spika, kamati yangu pia haikuridhika na kitendo kilichofanywa na Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA) – Tanzania Barakwa kushindwa kutuletea fedha zetu karibu Bilioni 18 kwa mwaka unaomalizika, pesa ambazo sisi tuliziidhinisha zikusanywe kutokana na kodi ya huduma wanazozipata watumishi wa Jamhuri ya Muungano wanaofanyakazi zao hapa Zanzibar. Pesa hizo zingeliweza kutatua kero mbali mbali kwa wananchi wa Zanzibar. Mhe Spika, suala hili sio dogo kwani kwa kiasi kikubwa limerejesha nyuma jitihada za Serikali yetu kuwaondolea wananchi wake shida za maisha. Shs 18 Bilioni ni karibu bajeti ya wizara zaidi ya tatu, kama tungelizipata tungeliweza kujenga miundombinu mingi, mfano ni mwaka uliopita waziri wa Afya alihitaji Bilioni moja tu ili ajenge ICU hadi leo sijuikama ameweza. Pia kutokana tatizo la Serikali yetu kwa hivi sasa kutokuwa na Meli ya uhakika ya kuwasafirisha wananchi wetu, kati ya Unguja naPemba, fedha hizo zingeliweza kuisaidia Serikali japo kulipa nusu ya gharama ili kununulia Meli ya uhakika ili wananchi kuweza kupata huduma ya usafiri wa uhakika. Aidha, fedhaa hizo zingeliweza kutatua tatizo la ukosefu wa madawati kwa kununua madawati ya kutosha kwa ajili ya skuli zetu. Pia, fedhaa hizo zingeliweza kuchangia ujenzi wa barabara zetu za ndani karibu zote, hata kumalizia skuli zetu tulizozianzisha majimboni, na nyengine zingeliweza kuchimba visima ili kuondoa tatizo la maji majimboni mwetu, kwa mifano hiyo michache kila mtu ameona ni kiasi gani zimerejesha nyuma Maendeleo ya Jamii yetu. Lakini vile vile  fedha hizi pia zingeliweza kuboresha makaazi ya wazee wetu wasiojiwejiweza pale Sebleni, na haya ndio mambo yanayopigiwa kelele na wananchi wetu kila siku.

Mhe Spika, nnamuuliza Mhe Waziri Gawio tulilolipata kutoka B.O.T la T/sh 7.8 Bilioni ndio Serikali mmesharidhika nalo? Kwani Mimi nnavyojua kuna madai ya Zanzibar kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu kupatiwa 11.5% ya Gawio kutokana na hisa zetu kwenye uundwaji wa B.OT. Hesabu za haraka kwa asilimia 11.5% tunayoidai tungeliweza kupata  Gawio si chini ya T/sh 15 Bilioni kwa mwaka huu ambapo tumezikosa karibu T/sh 7 Bilioni lakini kutokana na kimya kirefu na kwa kua na sisi tumeridhika na kupokea tunachopewa kutokana na unyonge wetu inaonyesha tumeridhika wakati hicho kitu sio sahihi hasa katika nchi zilizoungana kwa hiari kwa maslahi ya kiuchumi na kijamii lakini hadi leo tuna miaka karibu 48, suala hili halijapatiwa ufumbuzi, nadhani tungelikuwa tunadai kwa mataifa ya kigeni tungelikuwa tumeshajua moja, mambo kama haya ndio yanayowafanya wazanzibari kupiga kelele kudai haki zao ndani ya Muungano.

Mhe Spika, tunaipongeza Serikali yetu kutokana na mapato ya nchi kuongezeka imeweza kutenga karibu  T/shs 8 Bilioni kwa ajili ya Mfuko wa Elimu ya juu, ambapo ni asilimia 200% ya Bajeti ya mwaka uliopita hii imetokana na kilio chetu mwaka uliopita kwa vijana wetu wengi kukosa Mikopo wa kuendelea na masomo yao ya Elimu ya juu, ndio maana tunakusifu Waziri wetu mpendwa kuwa msikikivu kwa kutekeleza ushauri tunao utoa, lakini pamoja na pongezi hizo kamati yangu inaitaka wizara ya Elimu Zanzibar kuzitafuta pesa za wananchi zilizopotea karibu T/sh 8 Bilioni wanazodai eti wamepewa wanafunzi wasiowajua (Wanafunzi Hewa)  kamati yangu yangu inaagiza pesa hizo zirudishwe Serikalini mara moja kabla ya Bajeti ya Wizara ya Elimu kwasilishwa hapa Barazani au tupatiwe maelezo ya kina vinginevyo Mhe Spika, itabidi askari wako shupavu, wajumbe wa Baraza lako tukufu la Wawakilishi (Watch Dog) uwaagize wakazisake na nnaamini watazigundua ziliko.

Mhe Spika, eneo jingine tuliloligundua tunaweza kuongeza mapato kwenye Bajeti yetu ni kupitia katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Nyongeza ya kwanza orodha ya Mambo ya Muungano orodha ya 18 Elimu ya juu ni jambo la Muungano kwa hiyo kama tunavyopata Gawio kwenye mambo mengine japo hiyo ya muda 4.5% kwa Bajeti ya mwaka huu unaoishia mwezi huu kuna Gawio letu kiasi cha T/sh  15 Bilioni ambapo ni 4.5% ya T/sh 350 Bilioni zilizopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo hili pia ni miongoni mwa kero za Muungano. Tunataka Serikali yetu kuidai kwa Bajeti ya mwaka ujao kwa kupatiwa asilimia yetu ili tujipangie wenyewe matumizi yetu ya Elimu ya juu kwani tumepata taarifa kuwa kuna baadhi ya wanafunzi waliopo nje ya nchi wanataka kurejeshwa nchini kutokana kukosa ada za masomoyao.

Mhe Spika, eneo jingine ambalo tunaloweza kuisaidia Serikali yetu kuongeza mapato yetu ni kupitia Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa TZ  nyongeza ya kwanza orodha ya 15 Mafuta na Gesi asilia katika mapato yanayoendelea kuvunwa na Wizara ya Nishati na Madini ya Tanzania Bara ambayo sio Wizara ya Muungano ambapo inaendelea kuvuna mapato ya Gesi kwa zaidi yamwaka wa tisa hivi sasa lakini Zanzibar hatuna kinacholetwa kwetu au labda Serikali ituambie je mwaka huu unaokwisha  tumepata T/shs ngapi? zitokanazo na mapato ya gesi inayovunwa huko Bara? Lakini sio hivyo tu hivi sasa kwa kua imegundulika Gesi nyingi zaidi katika eneo la Mtwara na tunayo taarifa ya kuwa kuna makampuni mawili STAR ONE na BRITISH GAS Tayari yamepewa kazi hiyo na kuna zaidi ya Blocks sita ambazo yatapewa makampuni kwa ajili ya uzalishaji wa gesi na kila kampuni kabla ya kupewa kazi hiyo watatakiwa kulipa ada ya kilemba, hayo yote ni mapato ya Muungano, lakini sisi tukiwa wasimamizi wa maslahi ya wananchi inapaswa tuiulize Serikalini Je! kunani? Tunaamini kama Serikali itafuatilia kwa dhati, kuna mapato tutaweza kuyapata ili kuongeza uwezo wetu katika Bajeti yetu, bila ya hivyo tutakuwa tunawadanganya wananchi wetu tunapowambia suala la GESI na Mafuta ni la Muungano, wakati Serikali yetu haipati kitu na wananchi wake hawafaidiki na mapato hayo.

Mhe Spika, tunaipongeza Serikali kwa kupiga marufuku uuzwaji wa mafuta huko Baharini kwa njia ya meli kwa meli kwani kuna mapato mengi ya Serikali yalikuwa yakipotea tunaamini sasa mapato hayo sasa yataongeza mapato ya Serikali yetu. Lakini katika eneo hili tunaitaka Serikali kukaa na waletaji wa mafuta ili kulizungumzia suala la uletaji mafuta hapa nchini na ikiwa kuna Kampuni yeyote itakayokuwa na uwezo wa kuleta mafuta moja kwa moja hapa nchini waruhusiwe kwani T/Bara wao wameamua kuagiza mafuta kwa pamoja na kuyauza kwa makampuni mengine kwa hiyo kuna uwezekano wa makampuni yanayoleta mafuta Zanzibar kutozwa ushuru mara mbili.

Mhe Spika, kwa upande wa utekelezaji wa Program ya Mkuza 11 kwa upande wa huduma za jamii kamati yangu imeridhika na mkakati wa SMZ wa miaka mitatu kwa kuamua kutumia pesa za ndani kwa ajili ya ununuzi wa Madawa hasa kwa kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato kwani kutokana na hali za wananchi wetu uwezo wa kununua Dawa unakuwa mdogo, lakini kuna taarifa ya kuwa hivi sasa kuna baadhi ya wafamasia huziiba Dawa kutoka Serikalini na kuziuza Madukani kwa watu binafsi ,tunawambia Ole wao tabia hiyo waiache mara moja, vinginevyo adhabu kali inawasubiri pindipo tukija kuwanasa. Kwa hiyo Kamati yangu inashauri Serikali kurudisha ule utaratibu wa zamani kwa Serikali kutengenezesha Madawa na kuyaandika SMZ hili litaweza kukomesha wizi huo.

Mhe Spika,  kamati yangu bado hairidhiki na utekelezaji wa mashirikiano na sekta binafsi PPP kwani bado kuna kazi nyingi ambazo Serikali ingeliweza kushirikiana na Sekta binafsi, PPP kwa mfano suala la kuuweka mji wetu safi basi ni bora Mabaraza ya miji kuzitoa kazi hizo kwa Makampuni binafsi ili kuongeza wigo wa ajira binafsi, na tayari tumewashauri Mabaraza ya miji ili kulitekeleza hilo ili mabaraza wabakie na kazi chache ambazo watazimudu kwa wepesi,  Mhe Spika, kamati yangu imegundua miradi mingi hasa ya ujenzi imekuwa ikipewa Makampuni yanayotoka nje ya ZNZ na kuzikosesha kazi Kampuni za ndani  kwani wao ndio walipakodi wakubwa kwani hata usajili wao uko hapa ZNZ Kampuni ambazo nyingi huwatumia vijana wa hapa Nchini, na kuongeza ajira kwani kwa Nchi za wenzetu kodi ya wananchi hupewa kipaumbele Makampuni ya ndani ili kuyajenga uwezo, kwani kama hivi sasa tunazo taarifa kuwa hata Madeski pia hutengenezwa na Makampuni kutoka nje ya Zanzibar ambapo Makampuni ya ndani hukoseshwa kazi hizo, sasa je! hawa wananchi wetu watapewa kazi Nchi gani?.

Mhe Spika, hali ya ajira kwa vijana wetu ni mbaya sana hivi sasa vijana wetu wengi hawana ajira kwa hiyo nnatofautiana na taarifa aliotusomea Waziri, kwenye kitabu chake cha Bajeti. Alisema kuwa kati ya vijana watano eti ni mmoja tu ndie hana ajira,Mhe Waziri, takwimu hiyo haikufanyiwa utafiti wa kutosha, kwani vijana wengi hasa wa kike ambao ndio wapo wengi wakishamaliza Skuli tu hubaki nyumbani bila ya ajira, na kwa mfano kuna wengine wameshasomea ualimu ngazi ya Cheti na Diploma hawajaajiriwa hadi leo mbali waliofeli Kidato cha Pili na mbali walioacha masomo yao njiani kutokana na sababu mbali mbali.

Tunaelewa kuwa ajira sio ile ya kuajiriwa Serikalini tu bali shughuli yoyote inayompatia kipato cha halali mwananchi pia ni ajira, lakini ukweli vijana wengi hawana ajira na wanakuwa mzigo mkubwa kwa familia zao, Kwa hiyo tunatoa wito kwa Wizara zote kuweka kipaumbele kwa kuwapa kazi Makampuni ya ndani kwani hata akiba zao karibu zote wanaziweka katika Mabenki yaliopo hapa  hapa Nchini, kwa nchi za wenzetu hasa china tumegundua kampuni nyingi zinazopewa kazi na Serikali aidha ni Kampuni za Serikali au Makampuni ya ndani ili kuongeza mzunguko wa pesa na ajira Nchini kwao. Kwani wanaamini kutoa kazi kwa Makampuni ya nje basi hata pesa zao hazibakii Nchini na kuwekeza nje,  na kuna mfano mzuri hata kwa jirani zetu T/bara hivi sasa Serikali imewahamasisha Makampuni kushirikiana kwa Makampuni zaidi ya moja na kupewa miradi mikubwa kwa pamoja mfano ujenzi wa Barabara na Madaraja ili kuunganisha nguvu ya mtaji na ubora . ili kuijenga sekta binafsi iweze kutoa ajira kwa wananchi wetu.

Mhe Spika, tunatoa pongezi kwa Serikali yetu kwa kuendelea kutoa mikopo kupitia mfuko wa A, K na J.K lakini bado haujakidhi haja ya kuwawezesha kwani pesa hizo ni kidogo sana kwa hiyo wananchi wengi wamezisubiri kwa muda mrefu hadi leo wengi hawajapata, hapa tunaishauri Serikali yetu kuanzisha Benki ya Maendeleo ya vijana tunaamini hilo ndio suluhisho la kusaida Maendeleo kwa vijana hapa nchini kwetu. Pia tunapongeza jitihada zinazofanywa na Waziri wa Kazi na Uwezeshaji wa Wananchi kwa kuwatafutia misaada mbali mbali ya fedha na ajira vijana na kinamama wetu ,lakini bado ana kazi kubwa kwani melengo yake ni makubwa lakini uwezo uliopo ni mdogo.

Mhe Spika, kupitia wizara ya Kazi na uwezeshaji wananchi kiuchumi, tunataka kuanzia mwaka huu Waziri wakati wa Bajet yake ajekutuhakikishia kuwa vijana wetu wote wanaofanya kazi kwenye Mahoteli ya kitalii pamoja na walinzi kwenye minara ya Zantel kuhakikisha wanapatiwa mikataba ya ajira vinginevyo tutaikataa Bajet ya wizara kwani tunasikitika kuwa Makampuni na waekezaji wao wanakuja kutengeza faida kwetu lakini wanawatumia vijana wetu kuwafanyia kazi bila ya kuwapa mikataba ambapo hupelekea kuwafukuza kazi kama kuku kwani hakuna mkataba unaowalinda Muajiri na Muajiriwa, kwa mfano hivi sasa kuna walinzi wa Kampuni ya Zantel wameshatumikia karibu miaka mitano Wanaka kuwaachisha kazi na kwa kua hawana mikataba inonyesha wataondoka patupu bila haki zao za kustaafishwa kazi, hivi sasa wamekuwa kama manamba, tu sio waajiriwa. Na suala hili ndilo linalosababisha vijana wetu kila siku kuwa na hali ngumu ya maisha kwani hawana kinga ya hatma yao.

Mhe Spika, tunaishukuru Serikali yetu kwa kuweka utaratibu mzuri wa kutoa pesa taslim kwa  wawakilishi kwa kuondolea kero ndogondogo majimboni mwao kwani kwa muda mrefu tulikuwa tunawaangalia Wabunge wanavyotumia pesa zao sisi tukiwa hatuna uhakika wa kuzipata naamini wawakilishi wote watafanya matumizi vizuri kwa kufuata sheria na kurejesha matumizi ili kila mwaka kupatiwa nyingine, lakini tunaomba Serikali kuangalia mfumo wa wenzetu Kenya jinsi walivyoweka utaratibu wa utoaji na usimamizi wa fedha hizo ambapo hivi sasa kuna miradi mingi imejengwa na wananchi kupitia pesa hizo. Kwani majimboni tuna matatizo mengi lakini uwezo wa kuyatatua ni mdogo sana, kwa hiyo kwa mfumko wa bei kwa vifaa vya ujenzi shs 10 Mil. Sijui tatatatua jambo gani na tuache jambo gani, lakini pia tunaishukuru Serikali yetu kwa kuanzia kima hicho na tunaamini kila tukizitumia vizuri basi Serikali itatupatia zaidi.

Mhe Spika,  kwa aujumla Bajet ya mwaka huu imejaribu kujikita zaidi kwa maendeleo ya wananchi zaidi kwani karibu 341.1 sawa  53% ya mapato yanaelekezwa kwenye maendeleo na 307.8 sawa na 47% kwa matumizi ya kawaida kamati yangu imeridhika na mgawanyo huo maalum wa fedha lakini tatizo letu liko pale pale baadhi ya tunokwenda kuwakabidhi kuzisimamia si waaminifu sasa ni vigumu kuendelea kuwaamini kuwapa nyingine wakafanye watakavyo. Hichi kitu hakiwezekani hata kidogo.

Kamati yangu imeridhika na jinsi ya mgao livyofanywa kutokana na fedha iliyopo karibu 2 Bil kwa maeneo maalum ikwemo utunzaji na uhifadhi Mazingira, Walemavu, Madawati, Madawa lakini kamati yangu inatoa angalizo kuwa utekelezaji wa matumizi hayo tutaufuatilia kwa karibu ili watu wachache wasije kujificha kwenye chaka hilo kwa matumizi yao binafsi.

Mhe Spika, kamati yangu inaipongeza Serikali kwa kutenga pesa kwa ajili ya kupanda Mikarafuu zaidi na kuitoa kwa wakuli wa zao hilo lakini pia kwa kuimarisha kilimo hasa cha Mpunga kwa kununulia mbegu , Mbolea na Pembejeo za Kilimo lakini bado hatutakubali kuruhusu kuidhinisha pesa nyingine mpaka tujue pesa tulizotoa mwaka uliopita zimetumika vipi, kwani tunazo taarifa kuwa kuna baadhi ya watendaji waliopewa pesa hizo kwa ajili ya kunulia Mbolea na pembejeo za kilimo hawakuzifikisha kwa wahusika na Serikali inaju lakini kama kawaida yao Serikali hadi leo iko kimya hakuna hatua tulioisikia iliyochukuliwa kwa wahusika hadi leo wanapiga tai maofisini mwao. Sasa nakuuliza Mhe Spika kwa hali hii tutapona kweli na hayo Maendeleo ndio yatapatikana au tunaimba tu? Mhe Spika, sasa wakati umefika kila mtu aliejikubalisha kuwatumikia wananchi awalibike kwaupande wake, na hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa haraka.

Mhe Spika, Serikali imetuomba ruhusa ya kuwaruhusu kuuxwa kwa majengo Machakavu ya Serikali, suala hili kamati yangu haikubaliani nalo kwa sasa mpaka tupate jawabu kutoka Serikalini ya hatua tuliyoitaka Serikali kuyarudisha Serikalini majengo tuliyataja kwenye ripoti ya kamati teule ambayo yaliuzwa kinyume cha Sheria na watu wachache kujinufaisha na kwa taarifa yako .

Mhe Spika, tumegundua kuwa pia kuna majengo mengine na mali nyingine za Serikali zimeuzwa kwa bei ya kutupwa wakati kuna agizo la Serikali kuzuia mali za Serikali zisiuzwe na majengo hayo pia kwanza yarudishwe Serikalini na hapo ndiopo tukubaliane utaratibu wa kuyauza majengho mengine, Mhe Spika, Serikali tushakukubalieni  mambo mengi lakini kutokana baadhi yenu kutiokuwa waaminifu kwa sasa hatukubali vitu kuirahisi, kwa hili Serikali itusikilize na sisi. Na hapo baadae tutapanga utaratibu mzuri wa uuzaji ambao hautaleta harufu ya Rushwa.

Mhe Spika, tunaipongeza Serikali yetu ya awamu ya Saba kwa kuanzisha utaratibu wa kuyafufua majengo ya zamani yaliokuwa yakitumiwa na Serikali kama vile viwanda huko Maruhubi kwa ajili ya kujenga majengo ya Serikali, ambapo baadhi yao si muda mrefu yataanza kutumika Hongera D.k Shein kwa  uono wako wa mbali kwa kua Serikali yetu inamipango mjngi ya Maendeleo tunaamini na mengine tutayaendeleza kwa maslahi ya umma.

Mhe Spika, kwa kumalizia  kamati yangu inaamini kama tutakuwa makini kuusimamia uchumi wetu hasa kwa kuimarisha ukusanyaji kodi kuacha kudokoa  tunachokipata na kuendelea kudai mapato yetu yaliyomo ndani ya muungano kwa sasa bila ya kuambiwa tusubiri Katiba mpya kama tunavyoambiwa hivi sasa tunaamini mapato yataongezeka sana kwa kipindi kifupi sana, lakini isitoshe kwa maandalizi ya siku za baadae, matayarisho ya uchimbaji wa Mafuta na Gesi lakini pia kuendelea kudai kwa ZNZ kuwa ni Eneo Maalum Tengefu La Kiuchumi ili kuvutia uwekezaji hasa wa viwanda na Bandari huru na kutafuta ufadhili kwa ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri tunaamini tukiweza kufanya hayo basi ZNZ itakuwa miongoni mwa Nchi zitakazobadilika kwa maendeleo kwa haraka sana. Tunamuomba M/Mungu atujaalie tufikie hatua hiyo kwa haraka sana, Mhe Spika, mwisho kabisa napenda kuwashukuru wananchi wangu wote wajimbo la Kwamtipura kwa kuendelea kunipa moyo na imani ya kuwatumikia na ninawaahidi nitajitahidi kuwatumikia kwa uwezo wangu wote, pia naishukukuru familia yangu Mama yangu Ndugu zangu, hasa wake zangu woote kwa kunivumilia na kunipa moyo wakati wote ninapowataka ushauri wao,

Mhe Spika, kwa mara nyingine nakushukuru wewe kwa kuniruhusu kusimama mbele ya Baraza lako tukufu kuwasilisha ripoti hii ya Kamati ya Wenyeviti wako wa Baraza pia nawashukuru Waheshimiwa wote pamoja na wananchi kwa kunisikiliza, Ahsantenisana.

Mhe Hamza Hassan Juma

…………………………….

Mwenyekiti wa Kamati ya Wenyeviti  wa
Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi, Zanzibar

No comments: