Sunday, June 24, 2012

KUHUSU AMRI YA MAHAKAMA KWA MADAKTARI --- Dr ULIMBOKA ALONGA

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dkt. Steven Ulimboka, amesema hawajapata taarifa zozote kutoka Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, ya kuzuia mgomo wa Madaktari uliopo katika siku yake ya pili leo.

Dkt. Ulimboka amesema mgomo ulioanza jana haukihusishi Chama cha Madaktari nchini (MAT).

Alisema, wao taarifa za agizo la kusitisha mgomo kutoka Ofisi ya Mwanash wamezisikia katika vyombo vya habari hivyo hawajui kama zinawahusu wao au MAT, na kwamba itakuwa ni vigumu kutolea ufafanuzi jambo lisilowahusu.

Dkt. Ulimboka alisema kuwa kimsingi Serikali imekuwa ikipotosha dhana nzima ya mgomo huo kwani inaonyesha kuwa suala la posho ndilo linalogomewa na madaktari wakati si kweli.

“Watu wanadhani tunapigania posho zaidi, hapana tunapigania huduma bora kwa wagonjwa, kwa sababu sifa ya kwanza katika hospitali ya rufaa ni kuhakikisha yale yanayoshindikana katika hospitali nyingine yanawezekana katika hospitali za rufaa,” alisema.

Alitolea mfano kifaa cha kupimia cha CT- SCAN ambacho kina zaidi ya miezi saba hakifanyi kazi katika Hospitali ya Muhimbili huku ikiwalazimu baadhi ya wagonjwa wanaofika kutakiwa kufanya kipimo hicho katika hospitali nyingine.

“Wengine hawana uwezo huo, wale wanaobahatika kufika huku wanakuta kifaa hakifanyi kazi, huyu ni mgonjwa bado unamuongezea gharama nyingine, tukiyasema haya wanasema sisi hatuwajali wagonjwa,” alisema Dkt. Uliomboka.

Alisema madai mengine ni pamoja na miundombinu ya hospitali kwa kile alichoeleza haziwiani na idadi ya wagonjwa na kutolea mfano wodi ya watoto katika Hospitali ya Temeke kuwa mazingira ni magumu.

Alibainisha kuwa kitaaluma ni lazima wawahudumie wagonjwa wakiwa vitandani na inapotokea wagonjwa wakiwa chini inawawia vigumu kuwahudumia, na kwamba hayo ndiyo masuala waliyokuwa wanalalamikia.

“Kwanini hospitali zetu ziwe sehemu ya mateso kwa wagonjwa badala ya kuwa sehemu ya faraja? Tunaambiwa tuwaandikie dawa wagonjwa, wakienda dirishani hata Panadol hakuna, haya hawataki kuzungumzia, wameamua kupandisha posho ya maiti wakati hata katika madai yetu hatukuwa na dai hilo,” alisema.

Source: Gazeti la Tanzania Daima Jumapili

No comments: