Tuesday, June 19, 2012

kKAMA DENI LENYEWE NDIO HILI BASI IPO KAZI NZITO...

Chenge, alisema kutokana na taarifa iliyowasilishwa mbele ya kamati hiyo na Waziri wa Fedha, deni la taifa hadi kufikia Machi mwaka huu limefikia Sh trilioni 20.2 kutoka Sh trilioni 17.5 Machi 2011.

Alisema deni hilo ni sawa na ongezeko la asilimia 15.4 na kwamba kati ya deni hilo, deni la nje ni Sh trilioni 15.3 na deni la ndani ni Sh trilioni 4.9.

“Kutokana na umuhimu wa kodi kwa taifa letu, kwa muda mrefu kumekuwa na tabia kwa wawekezaji, hasa wa nje kupewa misamaha ya kodi bila sababu za msingi.

“Zao la pamba ni muhimu sana, kwani linatoa ajira kwa wakulima wadogo wapatao 500,000 na kuwezesha maisha ya Watanzania, kwa hiyo ni wakati mwafaka kwa Serikali kutangaza bei ya pamba.

“Kwa hali hii, ninaweka wazi msimamo wangu ni lazima Serikali itambue bila Sh 1,000 ya kununua kilo ya pamba hakuna pamba na hili Serikali ilitambue,” alisema Chenge.

Wakichangia bajeti hiyo baada ya Kamati ya Fedha na Uchumi, Mbunge wa Sumve, Richard Ndasa (CCM), alivirushia kombora vyombo vya usalama kwa kushindwa kufanya kazi inavyopaswa.

Alisema kuwa, kuathirika kwa mapato ya Serikali kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa malipo hewa katika wizara na idara za serikali, hali inayowafanya wananchi kukata tamaa kwa viongozi wao.

Pia alipinga hatua ya Serikali kutaka kupandisha kodi kwa waendesha pikipiki, huku akionya kwamba hali hiyo itawafanya wananchi kuichukia Serikali yao.

“Kila eneo hivi sasa kumekuwa na malalamiko juu ya vitendo vya rushwa na Serikali inajua, tena kwa kuanzia na wizara ambazo ni vinara wa malipo hewa, zikiwamo TAMISEMI, Wizara ya Fedha na Wizara ya Kilimo.

“Pamoja na uwepo wa mambo hayo, Serikali katika bajeti yake haijasema namna ilivyoshughulikia tatizo hili.

“Kwa mfano hii TAKUKURU imelala mithili ya sanamu lililotegwa katika jaruba la mpunga, watu wanaiba lakini wao wamelala, na si hao tu, hata Usalama wa Taifa. Hivyo kutokana na umuhimu wa bajeti hii tunaviomba vyombo hivi vifanye kazi yake kwa mujibu wa sheria,” alisema Ndasa.

Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohammed (CUF), alisema kitendo cha Serikali kuwakumbatia wawekezaji kinaweza kuhatarisha usalama wa taifa.

“Kuna wawekezaji ambao huwa wanakuja nchini wakiwa na shida huku wakiweka mikono nyuma lakini baada ya kuingia mikataba na Serikali huanza manyanyaso dhidi ya wazawa, hili katu hatuwezi kulivulimia.

“Kwa kupitia bajeti hii na kama tunahitaji kumkomboa mkulima wa pamba, ni wakati mwafaka wa kuwathamini Watanzania kwa kuhakikisha Serikali inaweka mazingira mazuri ya soko.

“Kila kona wananchi wanalia na pamba yao, lakini Serikali haitoi bei dira katika zao hili, sasa kama wanahitaji kuuza kwa Sh 1,000 waruhusiwe na si kuwanyanyasa wakulima,” alisema Hamad Rashid.

Source: http://www.wavuti.com/index.html#ixzz1yDx9ihom

No comments: