HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA
KAMBI YA UPINZANI BUNGENI NDUGU KABWE ZUBERI ZITTO (MB), WIZARA YA FEDHA NA
UCHUMI, KUHUSU MAPENDEKEZO YA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALI KWA
MWAKA WA FEDHA 2012/2013
______________________
I. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya
Kambi ya Upinzani, ninatoa maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu Bajeti ya Nchi ya
mwaka wa fedha 2012/2013 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kifungu cha 99(7) toleo
la Mwaka 2007.
Mheshimiwa Spika, Natoa pongezi za dhati kabisa kwa
Ndugu William Augustao Mgimwa, Mbunge wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa kwa
kuteuliwa na Rais kuwa Waziri wa Fedha na Uchumi. Vile vile nawapongeza Ndugu
Saada Mkuya na Ndugu Janeth Mbene kwa kuteuliwa kwao kuwa Wabunge na baadaye
kuwa Manaibu Mawaziri katika Wizara hii nyeti sana. Ninawapa pole pia
maana Wizara ya Fedha sio Wizara lelemama. Kambi ya Upinzani itaendelea
kuisimamia Wizara hii kwa ukaribu sana kama ilivyofanya katika kipindi cha miaka
miwili iliyopita. Mtakapofanya vizuri tutawapongeza ili muongeze juhudi,
mtakapoharibu tutawawajibisha.
Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri kwamba Mwaka wa Fedha
uliopita ulikuwa mwaka mgumu sana kwa Watanzania. Ni mwaka ambao gharama za
maisha zilipanda kwa kasi kubwa sana na juhudi za Serikali kuwakwamua wananchi
na hasa wananchi wanyonge kutoka kwenye lindi la ufukara ziligonga mwamba.
Kambi ya Upinzani inawapa pole Watanzania kwani hili ndilo walilochagua. Muhimu
ni kuvumilia mpaka uchaguzi ujao na kufanya mabadiliko ya Serikali ili kuweka
Serikali itakayoongozwa na CHADEMA na itakayoweza kukabili changamoto za sasa
na za baadaye.
Mheshimiwa Spika, naomba tufanye
mapitio kidogo ya Bajeti inayomaliza muda wake.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kutoa
bajeti mbadala ya Kambi ya Upinzani ni vema kufanya tathmini ya utekelezaji wa
bajeti ya Serikali iliyopita ili kuona ni kwa namna gani Serikali inathamini
fedha za walipa kodi, na dhamira yake ya kuleta maendeleo ya kiuchumi katika
Taifa. Katika kufanya hivyo, tutapitia baadhi ya maeneo ambayo Kambi ya
Upinzani tunaona kuwa hayakutekelezwa katika bajeti iliyopita.
Kupunguza Makali ya Maisha
Mheshimiwa Spika, Katika Bajeti
ya mwaka 2011/12 Serikali ilitangaza nia yake ya kupunguza makali ya maisha.
Hatua mbali mbali zilichukuliwa ikiwamo kupunguza kodi na tozo kwenye mafuta ya
Dizeli na Petroli, kuanza kutekeleza mpango wa dharura wa umeme na kutoa fedha
za kununua chakula kwa Wakala wa Chakula. Serikali ilitumia shilingi bilioni
296 na dola za Marekani milioni 183 kwenye Umeme. Vilevile Serikali ilitumia
shilingi bilioni 27 kununua Mahindi na kusambaza kwenye masoko.
Mheshimiwa Spika, licha ya hatua hizo
zilizochukuliwa Mfumuko wa Bei uliongezeka maradufu kutoka wastani wa asilimia
6.3 mwaka 2010/11 mpaka wastani wa asilimia 17.8 mwaka 2011/12. Serikali
imefeli katika lengo lake la kupunguza makali ya maisha kwa wananchi. Sio tu
kwamba Serikali imeshindwa kudhibiti upandaji holela wa gharama za maisha bali
pia hatua za Serikali zimeongeza kasi ya kupanda kwa makali ya maisha.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani
Bungeni katika Hotuba yake mbadala ya mwaka 2011/12 iliitaka Serikali
kushughulikia msingi wa mfumuko wa Bei hapa nchini ambao ni uzalishaji
mdogo wa mazao ya chakula. Tumeelezwa na Waziri Kivuli wa Mipango na Uchumi
kwamba Chakula peke yake ni asilimia 48 ya kapu la bidhaa na huduma ambazo
mwanachi anatumia. Mfumuko wa Bei ya Chakula kinacholiwa nyumbani na kwenye
migahawa ilikuwa asilimia 25 mwezi Aprili 2012 (BoT monthly Economic Review,
May 2012). Vile vile mfumuko wa bei wa nishati inayotumika nyumbani na mafuta
ya Dizeli na Petroli ulifikia asilimia 25 pia mwezi Mei mwaka 2012. Ni dhahiri
kwamba iwapo tutadhibiti mfumuko wa bei ya chakula tutaweza kushusha mfumuko wa
bei kurudi kwenye tarakimu moja.
Mheshimiwa Spika, Serikali
inapendekeza hatua zilezile ilizofanya mwaka wa fedha unaokwisha kwa kutoa
vibali kwa Wafanyabiashara vya kuagiza Mchele na Sukari. Katika hotuba yake
Waziri wa Fedha anasema ‘….Serikali ilitoa vibali vya kuagiza sukari bila
kutoza ushuru wa forodha kiasi cha tani 200,000 ili kukabiliana na uhaba na
kupanda kwa bei ya Sukari…’(uk 9 ibara ya 15). Baada ya hatua hii bei ya
Sukari ilipanda kutoka tshs 1700 mpaka tshs 2800 kwenye maeneo mengi nchini.
Waziri wa Fedha katika hotuba yake anatoa suluhisho. Ninanukuu. ‘…hatua za
haraka ambazo Serikali itachukua ni pamoja na kutoa vibali vya uagizaji wa
Sukari na mchele kutoka nje….’! Serikali inachukua hatua zilezile kwa tatizo
lile lile ikitegemea matokeo tofauti.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani
Bungeni inarejea pendekezo lake la mwaka jana kwa Serikali kutoa vivutio kwa
wakulima wadogo kuzalisha chakula kwa wingi. Miongoni mwa vivutio hivyo ni:
- Kuwekeza kwenye barabara za vijijini ili
mazao yao yafike kwenye masoko na kupata bei nzuri,
- Kuwekeza kwenye Usambazaji wa Maji vijijini
ili kina mama wasitembee mwendo mrefu kutafuta maji na hivyo kutumia muda
mwingi kwenye uzalishaji,
- Kuwekeza kwenye Umeme vijijini ili
wafanyabiashara wa vijijini waongeze thamani ya mazao. Kwa mfano, kuuza
Unga badala ya Mahindi.
- Kuwekeza kwenye miundombinu ya Umwagiliaji
vijijini ili wakulima wazalishe muda wote wa mwaka.
- Kuwekeza kwenye Elimu vijijini na pia Afya
vijijini ili wananchi wetu wawe na Afya bora na waelimike katika mbinu za
uzalishaji bora.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani
inaamini kuwa, hakuna mbadala wa kudhibiti mfumuko wa bei zaidi ya kuongeza
uzalishaji wa chakula na kuwekeza kwa wananchi wetu. Serikali inafikiria
uzalishaji utaongezeka kwa kusaidia wakulima wakubwa ambao watageuza wananchi
wetu kuwa Manamba na vibarua ndani ya nchi yao. Tuwekeze kwa watu wetu vijijini
ili waongeze uzalishaji na kwa kufanya hivyo mfumuko wa Bei ya chakula utakuwa
historia. Hakuna mwarobaini wa kupanda kwa bei za vyakula isipokuwa Kilimo.
Mhesimiwa Spika, Tunatambua kuwa
hatua tunazotaka Serikali ifanye ni za muda wa kati. Kwa muda mfupi tunataka
Bodi ya Mazao mchanganyiko, Wakala wa Hifadhi ya Chakula na Bodi ya Sukari
zipewe fedha kuagiza Mchele na Sukari na pia kununua kutoka kwa wakulima na
kusagisha Mahindi. Wafanyabiashara waagizaji wa Chakula washindane na Taasisi
hizi za Umma badala ya kuwapa vibali ambavyo hutolewa kwa rushwa na hivyo
kuongeza bei za bidhaa hizo.
Kuwezesha Wananchi Kiuchumi na
Kuongeza Ajira.
Mheshimiwa Spika, Serikali imesema
kwamba ilichukua hatua mbalimbali kukabiliana na tatizo la Ajira kwa kuongeza
fursa za ajira. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuongeza mitaji
katika Benki ya Rasilimali, Benki ya Wanawake, Benki ya Posta na Twiga Bancorp.
Pia Serikali imetangaza kwamba imeajiri walimu, maafisa ugani na watumishi wa
Afya. Hatua kama hizi pia zimetangazwa kwa mwaka wa Fedha wa 2012/13 ambapo pia
Serikali imetangaza kuajiri watumishi 71,756.
Mheshimiwa Spika, Duniani kote
Serikali haizalishi ajira bali ajira huzalishwa na Uchumi mzima ambapo Serikali
ni sehemu tu ya Uchumi (Jobs are created by the economy). Takwimu
zinaonyesha kwamba kila mwaka Tanzania inaingiza kwenye soko la Ajira watu
takribani laki saba. Shughuli za Uchumi zikiongezeka ndio Ajira zinatengenezwa.
Serikali inafikiria nini kuhusu vijana takribani milioni nane walio shule za
Msingi hivi sasa, Vijana milioni 1.7 walio katika Shule za Sekondari hivi sasa,
Vijana 200,000 waliopo vyuo vya Ufundi na Wanachuo 180,000 walio katika Vyuo
vya Elimu ya Juu (takwimu kutoka kitabu cha hali ya uchumi, 2012 sura ya 19).
Serikali ambayo bado inategemea takwimu za Ajira za Mwaka 2006 inajitamba kwa
kuajiri watu 70,000.
Mheshimiwa Spika, Jukumu la
Serikali ni kujenga mazingira ya wananchi kupata ajira ama kwa kujiajiri au kwa
kuajiriwa na shughuli za uchumi. Lakini ukweli ni kwamba Serikali imeshindwa
kushughulikia tatizo la Ajira na hasa ajira kwa vijana. Tatizo la Ajira kwa
Vijana ni Bomu litakalokuja kutulipukia vibaya sana kama hatutakuwa makini
nalo. Hii ni nchi ya Vijana. Kutoshughulikia masuala yao ni kutoshughulikia
masuala ya nchi.
Mheshimiwa Spika, changamoto ya
ajira kwa vijana Bajeti mbadala imeiwekea mikakati mipana ya kiuchumi kwa
kuanzisha miradi mikubwa ya Umma itakayomeza vijana waliopo mtaani na kuanzisha
kwa makusudi na kwa kasi Vyuo vya Ufundi stadi na Vyuo vya Ufundi na Mafunzo
vingi. Kambi ya Upinzani Bungeni inapendekeza Uwekezaji wa Miundombinu Vijijini
kama njia ya kupunguza tatizo la ajira kwa vijana. Vilevile tunapendekeza
Miradi mikubwa ya kuongeza mazao ya Kilimo hasa Pamba, Korosho na Katani ili
kupanua Ajira. Kambi ya Upinzani pia inapendekeza kujenga VETA katika kila
Halmashauri ya Wilaya na Chuo cha Ufundi katika kila Mkoa ili kutoa ujuzi kwa
vijana ili waweze kukabili maisha yao. Badala ya Serikali kukopa kwa ajili ya
Matumizi ya kawaida, Serikali ikope kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi na vyuo vya
Ufundi na Mafunzo. Ni Lazima viongozi sio tu tuwe makini bali tuonekane kuwa
makini tunaposhughulikia suala la Ajira kwa Vijana.
Sera ya Mapato
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani
Bungeni ilitangaza vipaumbele katika sera ya Mapato ambavyo ni pamoja na
kukusanya Mapato ya Serikali mpaka zaidi ya asilimia 20 ya Pato la Taifa ili
kuwezesha kujitegemea kupata fedha za miradi ya maendeleo. Pia Kambi ya
Upinzani inakusudia kufanya marekebisho mbalimbali ya sheria za kodi ili
kulinda viwanda vya ndani vinavyotumia malighafi za kilimo na mifugo za hapa
nchini, kupanua wigo wa Mapato kwa kutunga sheria ya kulazimu kila Mtanzania
kujaza fomu za marejesho ya kodi na kurekebisha viwango vya kodi ya Mapato
(PAYE). Vile vile tunapendekeza kufanya marekebisho ya sheria za kodi kwenye
sekta za madini na mawasiliano ili kuongeza mapato ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa
Fedha 2011/12 Serikali ilichukua hatua mbalimbali katika masuala ya Kodi.
Katika Bajeti mbadala pia tulipendekeza hatua mbali mbali ambazo tuliona
zitaongeza mapato ya Serikali na hivyo kutuwezesha kuendeleza nchi yetu. Baadhi
ya hatua mbalimbali tulizopendekeza Serikali imetangaza kuzitekeleza.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani
katika Bajeti Mbadala ya mwaka 2011/12 ilipendekeza masuala yafutayo ili
kuongeza mapato ya Serikali.
- Hatua zifuatazo zilipendekezwa ili kuweza
kukabiliana na ukwepaji wa kodi unaofanywa na makampuni makubwa ya
kimataifa (Multinational Corporations) na hatimaye kulipunguzia taifa
mapato:
i.Kutunga sheria kwa kuimarisha zaidi
sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004 kwamba, mikopo ya makampuni kwenye
uwekezaji, kwa sababu za kikodi, isizidi asilimia 70 ya mtaji wote uliowekezwa
na hii ianze mara moja bila kujali mikataba iliyopo.
ii.Kutunga sheria kuhakikisha kwamba
riba kwenye mikopo kutoka Makampuni yanayohusiana (sister companies)
haitaondolewa kwenye kutoza kodi (not tax deductible).
iii.Kuhakikisha kwamba mauziano ya
Kampuni yoyote ambayo mali zake zipo Tanzania yanatozwa kodi ya asilimia 30%
kama ‘ongezeko la mtaji’ (‘capital gains’).
Mheshimiwa Spika, katika mapendezo
haya ni pendekezo moja tu ndilo limechukuliwa na Serikali katika Bajeti ya
mwaka 2012/13 nalo ni pendekezo la ‘capital gains tax’. Hata hivyo Pendekezo la
Serikali lina makosa makubwa sana ya kifundi. Waziri wa Fedha Mhe. Mgimwa
amesema, ninanukuu ‘Kuanzisha kodi itokanayo na uuzaji wa rasilimali ya
uwekezaji (capital gains tax) kwenye uuzaji wa HISA za kampuni mama ya nje ya
nchi’
Mheshimiwa Spika, Ukisoma pendekezo
letu kwa haraka utaona kama Serikali imelichukua lilivyo, lakini kwa jicho la
kiuchumi pendekezo la Serikali na lile la Kambi ya Upinzani ni mambo tofauti
sana. Pendekezo la Serikali linazungumzia HISA. Mamlaka ya Mapato Tanzania
haitakuwa na mamlaka (jurisdiction to tax) kutoza kodi kwa Kampuni mama (as a
source or even residence). Mamlaka ya Mapato Tanzania ina mamlaka na Mali
(assets) zilizopo Tanzania za Kampuni mama. Kwa mfano, wakati kampuni ya
Barrick inanunua mgodi wa Bulyanhulu haikuinunua Kampuni ya Kahama mining ltd
bali ilinunua hisa zote za Kampuni ya Sutton Resources. Vile vile, wakati Zain
inanunua Celtel, haikununua Celtel Tanzania ltd bali Celtel Africa BV ambayo
ilikuwa inamiliki Celtel Tanzania BV ambayo ilimiliki Celtel Tanzania ltd.
Hivyo hivyo ilikuwa kwa AirTel ilipoinunua Zain. Kukwepa mitego hii ya
Mashirika ya Kimataifa (MNCs) sheria itaje kwamba Kodi hii itozwe kwa Mali
zilizopo Tanzania na sio kwa HISA kama alivyopendekeza Waziri wa Fedha.
Hata hivyo Kambi ya Upinzani inatambua hatua hiyo ya Serikali kuchukua wazo hili
ili kuongeza Mapato ya nchi.
Misamaha ya Kodi
Mheshimiwa Spika, Katika Bajeti
ya mwaka 2011/12 Serikali iliahidi kupunguza misamaha ya Kodi mpaka kufikia
asilimia 1 ya Pato la Taifa. Ahadi hii haikutekelezwa na Serikali na badala
yake imerejea kuahidi tena. Waziri wa Fedha ameliambia Bunge katika hotuba
yake, nanukuu ‘kuendelea kufanya mapitio ya sharia mbalimbali zinazotoa
misamaha ya kodi kwa lengo la kudhibiti na kupunguza misamaha hiyo’ (uk.39).
Badala ya Serikali kutuambia hivi sasa misamaha ya kodi imefikia asilimia
ngapi, imeendelea kutoa ahadi isizoweza kutekeleza.
Mheshimiwa Spika, Katika
Taarifa ya Utafiti uliofanywa na Jopo la Taasisi za dini hapa nchini
waliyoiita ‘The One Billion Dollar Question’ imeonekana
kwamba Tanzania inapoteza takribani shilingi trilioni 1.7 kutokana na misamaha
ya kodi, ukwepaji wa kodi, utoroshaji wa mitaji nje na udanganyifu katika
biashara ya kimataifa. Fedha hizi ni zaidi ya jumla ya Bajeti za Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Nishati na Madini. Fedha hizi ni zaidi ya Mkopo ambao
Serikali itadhamini kwa TPDC ili kujenga Bomba la Gesi kutoka Mtwara mpaka Dar
es Salaam. Fedha hizi zinazopotea kutokana na misamaha ya kodi ni zaidi ya
gharama za Ujenzi wa Gati mpya katika Bandari ya Dar es Salaam. Kambi ya
Upinzani inawapongeza Viongozi wa Dini kwa kufanya kazi hii nyeti sana lakini
tunampongeza zaidi Mtafiti Mtanzania Dokta Prosper Ngowi kwa kushiriki katika
utafiti huu. Tunaishauri Serikali kusoma Taarifa hii na kutekeleza mapendekezo
yake ili kuongeza mapato ya Serikali. Lugha za kufanya mapitio kila mwaka
hazisaidii, wananchi wanataka kuona misamaha ya kodi imepungua mpaka kiwango
kinachostahili cha asilimia 1 ya Pato la Taifa.
Kurekebisha mfumo wa Kodi ya Mapato
Mheshimiwa Spika, Bajeti mbadala ya
mwaka 2011/12 ilipendekeza kuifanyia marekebisho sheria ya Kodi ya Mapato ya
mwaka 2004. Tunarejea pendekezo letu na kuongeza pia kwamba sehemu ya kodi ya
Mapato inayotoa fursa (grandfathering) kwa Kampuni za Madini kutumia sheria ya
kodi ya Mapato iliyofutwa ya mwaka 1973, ifutwe. Pendekezo letu lina lengo la
kutaka kuweka mfumo wa ‘straightline method of depreciation’ ya asilimia 20
badala ya sasa ambapo Kampuni za Madini hufanya ‘100% depreciation’ kwenye
Mitambo yao mwaka wa kwanza na hivyo kuchelewesha kulipa ‘Corporate Tax’.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeamua
kupandisha kiwango cha chini cha kipato ili kutoza kodi ya Mapato (PAYE) kutoka
tshs 135,000 mpaka tshs 170,000 bila kushusha kodi yenyewe. Hii haitamsaidia
mwananchi hata kidogo kwani bado kiwango cha kodi cha asilimia 14 kipo
juu sana. Vile vile kiwango cha chini cha pato litakalotozwa kodi kitawaathiri
wafanyakazi wa Serikali maana ndio ambao Serikali ina mamlaka ya kutangaza kima
cha chini cha Mshahara wao na kuwaacha wafanyakazi wa Sekta Binafsi ambao wengi
hulipwa kiwango kidogo sana cha mishahara. Kimsingi kutokana na tangazo lake,
Waziri wa Fedha ametangaza kima kipya cha chini cha mshahara kuwa kitakua tshs
170,000.
Mheshimiwa Spika, tunarejea kauli
yetu kwamba kupanda kwa gharama za maisha kumepunguza uwezo wa matumizi ya
wananchi walioajiriwa na kulipwa mishahara ambayo inakatwa kodi (PAYE).
Tunapendekeza kwamba PAYE ianzie asilimia 9 kutoka asilimia 14 na kiwango cha
chini cha kutoza kiwe tshs 150,000. Tunatambua kuwa kodi hii ni chanzo kikubwa
cha Mapato kwa Serikali ambapo kwa mwaka huu wa Fedha kinatarajiwa kuingiza
takribani shilingi bilioni 1,437 (asilimia 18 ya Mapato yote ya kodi
yanayokusanywa na TRA) kutoka Idara ya Kodi za Ndani (Wafanyakazi wa Serikali
tshs 115bn, Wafanyakazi wa Mashirika ya Umma tshs 47bn na Wafanyakazi wa Sekta
binafsi tshs 312bn) na Idara ya Walipa kodi wakubwa (Wafanyakazi wa Serikali
tshs 450bn, Wafanyakazi wa Mashirika ya Umma Tshs108bn na Wafanyakazi wa Sekta
Binafsi tshs 406bn). Hata hivyo wananchi wanapobakia na pesa za matumizi kodi
nyingine kama VAT na Ushuru wa Bidhaa huongezeka na hivyo kupunguza kiwango cha
Mapato ya Serikali ambayo yangepotea kutokana na uamuzi huu.
Mheshimiwa Spika, Hata hivyo bado
kuna haja ya kuangalia upya ‘tax brackets’ na kuzirahisisha kwa kuzipunguza
na kuongeza kiwango cha kodi ya Mapato kwa watu wenye kipato kikubwa zaidi.
Mheshimiwa Spika, ili kuongeza
mapato kutoka kwa watu wenye kipato kikubwa kambi ya Upinzani inapendekeza
mabadiliko katika viwango vya juu vya kodi ya Mapato ambapo tunapendekeza
kupandisha kiwango cha juu kabisa cha kukokotoa kodi ya mapato (PAYE) kiwe
shilingi milioni kumi na kodi iwe asilimia 42 kutoka asilimia 30 ya sasa.
Mheshimiwa Spika, Tunapendekeza
kwamba mtu yeyote anayepata mapato ya zaidi ya shilingi 10,000,000 alipe kodi
ya Mapato ya shilingi 500,000 kujumlisha na asilimia 42 ya tofauti ya shilingi
10,000,000 na shilingi 3,200,000 kama inavyoonekana kwenye jedwali hapa chini.
Lengo la mapendekezo haya ni kuwafanya watu wenye kipato kikubwa walipe kodi
zaidi kulingana na kipato wanachopata maana hivi sasa masikini wanalipa kodi
nyingi zaidi kuliko wenye nacho.
Kodi
(PAYE)
|
Mapendekezo ya mapato ya kutozwa
kodi kwa mwezi
|
Kiwango kipya cha Kodi
(PAYE)
|
|
Mapato yanayozidi shilingi
720,000
|
Sh. 112,500 ongeza
30% ya kiasi kinachozidi sh. 720,000
|
Mapato yanayozidi 720,000 lakini
hayazidi sh. 3,199,199
|
Sh.112,500 ongeza 30% ya ziada ya
sh. 720,000
|
Mapato yanayozidi sh. 3,200,000
lakini hayazidi sh.9,999,999
|
Sh.190,000 ongeza 38% ya ziada ya
3,200,000.
|
||
Mapato kuanzia sh. 10,000,000 na
kuendelea
|
Sh. 500,000 ongeza 42% ya mapato
yake.
|
Mheshimiwa Spika, Mapendekezo haya
hayatapunguza Mapato ya Serikali kwani wigo wa kodi utakuwa umeongezeka kwa
kuwagusa wafanyakazi katika sekta binafsi na pia kupata kodi zaidi kutoka kwa
watu wenye kipato kikubwa zaidi.
Mheshimiwa Spika, vile vile Kambi
ya Upinzani inaendelea kupendekeza kuwa mchakato uanze ili kila
Mtanzania mwenye umri wa miaka 18 na zaidi awe anajaza fomu za kodi (tax
returns) kila mwaka. Suala hili ni muhimu sana na litangazwe mwaka huu
ili tuwe na mwaka mzima wa kujitayarisha ili lianze Mwezi Julai mwaka 2013.
Mtanzania yeyote, awe na kipato au asiwe na kipato ajaze Tax Returns. Mfumo huu
utatoa takwimu muhimu sana kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania na utasaidia sana
hapo baadaye kupanua wigo wa Mapato. Tunapendekeza marekebisho katika Sheria ya
Kodi ya Mapato ili mfumo huu uwepo kisheria ndani ya mwaka mmoja kuanzia sasa.
Mheshimiwa Spika, Vile vile, Kambi
ya Upinzani inapendekeza kuanzishwa kwaReal Estate Regulatory Authority kama
tulivyofanya kwa mwaka uliopita na kwamba kila mwenye nyumba ya
kupangisha lazima atambuliwe na kulipa kodi inavyostahili. Lengo ni kuhakikisha
Sekta ya Nyumba inatoa mapato ya kutosha kwa Serikali na kuzuia mianya ya
ukwepaji kodi inayofanywa na wenye nyumba.
Presumptive Tax
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni
ilipendekeza mwaka 2011/12 kwamba ushauri wa Mradi wa kuboresha mfumo wa kodi
(Tax Modernisation Project) ambao ulishauri kwamba ipo haja ya kuainisha Kodi
ya VAT na Presumptive Tax, utekelezwe. Tunashauri kuwa kodi anayotozwa
mfanyabiashara ndogondogo kabla hajaanza kufanya biashara ifutwe kabisa. Uamuzi
huu utapunguza mapato ya Serikali (Shilingi bilioni 21.6 kwa mujibu wa Kitabu
cha Bajeti Vol. I) katika kipindi cha muda mfupi lakini itakuwa ni chanzo
kikubwa sana cha mapato katika kipindi cha muda mrefu.
Vyanzo vipya vya Mapato
Mheshimiwa Spika, Pamoja
na kupitia vyanzo vya mwaka jana na kulinganisha na mapendekezo ya Serikali,
Kambi ya Upinzani bado inapendekeza vyanzo vya ziada mwaka huu ili kuboresha
Mapato ya Serikali.
Kupanua wigo wa Skills Development
levy
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani
tunapenda kushukuru kuwa wazo letu la kutoza kodi ya skills development
levy tuliyopendekeza katika hotuba yetu ya mwaka uliopita lilifanyiwa
kazi na serikali lakini kwa mwaka ujao wa fedha tunaitaka serikali kuipitia
upya kodi kwa kuongeza wigo wa wachangiaji ili kuwa na fedha za kutosha kwa
ajili ya kugharamia elimu ya juu.
Mheshimiwa Spika, tunapendekeza
kiwango cha tozo ya kuendeleza stadi (skills development levy – SDL) kishuke
kutoka asilimia 6 ya sasa mpaka asilimia 4. Tunapendekeza kuwa Waajiri wote
walipe kodi hii ikiwemo Serikali na Mashirika ya Umma. Lengo ni kupunguza mzigo
kwa Waajiri na kuondoa ubaguzi kwani wanaofaidika na tozo hii (wanafunzi wa
elimu ya Juu) pia huajiriwa na Serikali na Mashirika ya Umma. Serikali ilipanga
kukusanya tshs 161bn kutoka katika tozo hii kwa mfumo wa sasa.
Mheshimiwa Spika, Marekebisho
ambayo Kambi ya Upinzani inayapendekeza yataongeza mapato ya Serikali mpaka
tshs 320bn.
Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha
katika tozo hii amesema Serikali ‘itapitia upya maudhui ya viwango vya tozo’
hii. Kambi ya Upinzani imetamka maudhui na viwango na tunaiomba Serikali
itekeleze pendekezo hili.
Mheshimiwa Spika, Tunapendekeza mgawanyo
wa tozo hii urekebishwe kwa kuongeza mapato yatakayokwenda kwenye Vyuo vya
Ufundi mchundo.
Mheshimiwa Spika, kama wanafunzi
wetu watasomeshwa na kodi hii basi tuangalie upya mfumo wa Mikopo ya wanafunzi
wa Elimu ya Juu. Fedha inayopatikana kwenye Kodi hii itumike kusomesha kwa
‘grant’ wanafunzi wanaofanya vizuri zaidi darasani na kuwapunguzia mzigo wa
mikopo. Vile vile tuangalie kama tunaweza kukopesha wanafunzi malazi na chakula
tu na kutoa bure ada na mafunzo kwa vitendo pamoja na vitabu.
Kulinda kazi za Wasanii
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani
mara kwa mara tumekuwa tukieleza jinsi wasanii wanavyoshindwa kunufaika na kazi
zao kutokana na kukosekana mfumo rasmi wa kiserikali unaozuia wizi wa kazi za
wasanii. Pamoja na serikali kukubali kuahidi kuwa na mfumo rasmi wa kuzuia wizi
wa kazi hizo, serikali haijaweka wazi mfumo rasmi utakaokuwa unatumika kuzuia
wizi huo na hatimaye wasanii kunufaika na kazi zao.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani
katika hotuba ya Wizara ya Habari Vijana na Michezo kwa mwaka uliopita
tulingumzia suala hili na tulishauri kwamba kuwe na utaratibu wa kuweka sticker maalumu
zinazotolewa na mamlaka za serikali kuonyesha uhalali wa muuzaji wa kazi za
wasanii. Serikali imetekeleza pendekezo letu. Hata hivyo tuna maoni tofauti
kuhusu namna ya kutekeleza pendekezo hili.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa
kumbukumbu zilizopo, serikali mwaka 2006 kupitia gazeti la Serikali Na. 18 la
tarehe 10 Mwezi wa Februari, ilianzisha utaratibu wa HAKIGRAM kama stiker
maalumu za kazi halali za wasanii zinazotolewa na COSOTA. Kambi ya Upinzani
tunapendekeza utaratibu huo uendelee na Mamlaka ya Mapato TRA ihusike kukusanya
mapato kwa ajili ya kazi hiyo na COSOTA wataratibu utoaji wa HAKIGRAM. Hii
itaenda sambasamba na kuzuia uchakachuaji wa HAKIGRAM hizo ili kutopoteza lengo
la kuweka mfumo huo. Stiker zisitolewe na TRA bali zitolewe na COSOTA na TRA
isimamie eneo la Mapato tu. Hii itasaidia kwani stiker hizi hazitatumika kupata
mapato peke yake bali pia kuweka kumbukumbu muhimu za kazi za wasanii.
Mapato kutoka Sekta ndogo ya
Mawasiliano ya Simu
Mheshimiwa Spika, serikali imekuja na
pendekezo la kuendelea na kutoza ushuru wa bidhaa kwenye masuala ya huduma ya
mawasiliano ya simu, jambo ambalo litamgusa mtumiaji wa huduma hiyo ambaye ni
mwananchi wa kawaida na hivyo kuongeza gharama za simu. Kambi ya Upinzani
inapinga kabisa kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye muda wa Maongezi (airtime)
kwenye simu za mkononi.
Mheshimiwa Spika, Hoja ya wananchi
hapa ni kwamba Kampuni za Simu za mkononi hazilipi kodi ya kutosha na hasa kodi
ya Makampuni (corporate tax). Waziri Mkuu alipokuwa anafunga Bunge la Bajeti
mwaka 2011 alitangaza Kampuni ambazo ni walipa kodi wakubwa katika kipindi cha
miaka 5 iliyopita. Katika orodha hiyo kulikuwa na Kampuni moja tu ya Simu za
Mkononi (Kampuni ya AirTel).
Mheshimiwa Spika, wakati wananchi
wanataka kodi zaidi kutoka Kampuni za simu, Serikali inapendekeza kuongeza kodi
kwa mwananchi anayetumia simu. Kampuni zilipe kodi ya Mapato na sio kukandamiza
wateja kwa ushuru wa bidhaa ilihali huduma zenyewe za simu hazina ubora.
Mheshimiwa Spika, vilevile wananchi
wanalalamika kwamba Kampuni za simu za Mkononi hajiweki wazi mapato yake yote
hali iliyopelekea Kamati ya Bunge ya POAC kuiagiza TCRA kufunga mtambo
utakaoweza kuijulisha TCRA mapato yote ambayo kampuni za Simu zinapata.
Serikali ya Ghana ilifanya hivi na kupandisha maradufu mapato yanayotokana na
sekta ndogo ya simu. Hivi sasa Ghana, nchi yenye watumiaji wa simu milioni 17
ukilinganisha na Tanzania yenye watumiaji 23 milioni, inakusanya asilimia 10 ya
Mapato ya Serikali kutoka kwenye kampuni za Simu peke yake. Iwapo Tanzania
ikifikia kiwango cha Ghana cha asilimia 10 ya Mapato ya ndani ya Serikali
kutoka kwenye kampuni za simu, Tanzania itaweza kukusanya zaidi ya Shilingi bilioni
860 kutoka kwenye sekta ndogo ya simu peke yake. Hata hivyo mazingira ya Ghana
na Tanzania ni tofauti na hivyo tunapendekeza kiwango kutokana na hali yetu.
Mheshimiwa Spika, Shirika la TCRA
kupitia zabuni nambari AE-020/2010-11/C/04 imetangaza ‘request for
expression of interest for design, development, installation and Management of
Telecommunication monitoring system under build, operate and transfer’ ili
kupata chombo cha kufuatilia Mapato ya Kampuni za Simu. Kwa mujibu wa ratiba
zilizotangazwa na TCRA chombo kitakuwa kimeanza kazi mwishoni mwaka huu wa
2012. Kwa dhati kabisa napenda kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa TCRA na watumishi
wote kwa kutekeleza maelekezo ya Kamati ya Bunge kwa haraka ili kuhakikisha
mapato kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kilichotushangaza
ni kwamba Waziri wa Fedha na Uchumi hakugusia kabisa suala hili muhimu sana kwa
mapato ya Serikali badala yake Serikali imekimbilia kukandamiza wanyonge
watumiaji wa Simu na kuyaacha Makampuni ya Simu yakilipa kiduchu kutoka kwenye
mapato yao.
Mheshimiwa Spika, uamuzi huu wa
kufuatilia mapato ya Kampuni za Simu na Marekebisho tunayopendekeza ya kujenga
uwezo zaidi wa TCRA kwa kuwa na Idara ya ‘Revenue Assurance’ na kurekebisha
sheria ya TCRA kwa kuweka wazi makujumu ya TRA ndani ya TCRA, utaiingizia
Serikali mapato ya takribani tshs 660bn.
Mheshimiwa Spika, katika eneo hili
la Sekta ya Mawasiliano ninaomba kurejea kuitaka Wizara ya Fedha itoe maelezo
hapa Bungeni namna ambavyo Hisa za serikali katika Kampuni ya MIC Tanzania ltd
inayomiliki Kampuni ya Tigo zilivyouzwa. Mheshimiwa Spika Serikali ilikuwa
inamiliki hisa asilimia 26 katika Kampuni hii. Kwa mujibu wa kumbukumbu
nilizoziona Hisa hizi zote ziliuzwa kwa thamani ya dola laki saba kwa mwana
hisa mwenza mnamo mwezi Februari mwaka 2004. Kampuni hii leo inapata mapato ya
Tshs bilioni 20 kwa mwezi, tuliuza hisa zetu asilimia 26 kwa dola laki saba!
Laki Saba dola! Kambi ya Upinzani inataka uchunguzi maalumu katika mauzo haya
na Taifa liambiwe nini kilitokea na hatua gani za kuchukua dhidi ya waliouza
mali hii ya Umma bila zabuni wala kuzingatia thamani ya fedha.
Kuzuia mauzo ya ngozi ghafi nje ya
nchi
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani
imeshangazwa na hatua ya serikali kuja na pendekezo la kuongeza ushuru kwenye
bidhaa ya ngozi ghafi inayosafirishwa nje kutoka asilimia 40 hadi 90 lengo
likiwa ni kuhamasisha usindikaji wa ngozi hiyo na kuiongezea thamani.
Mheshimiwa Spika, kwa nchi iliyo na
mianya mingi ya rushwa kama Tanzania hatua hii haitakuwa na tija kwa kuwa
wafanyabiashara wengi wa ngozi ghafi wamekuwa na tabia ya kupunguza takwimu za
kusafirisha ngozi ghafi na hivyo kupelekea serikali kukosa mapato mengi sana.
Serikali inafahamu kwamba hata ushuru wa mauzo nje wa asilimia 40 haukuweza
kutatua tatizo la viwanda vya ndani kukosa malighafi. Kambi ya Upinzani
haikubaliani na Pendekezo la Serikali kwani halitatatua tatizo la kukuza sekta
ndogo ya Ngozi nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani
tunaitaka serikali kuzuia kabisa kusafirisha ngozi ghafi kwenda nje na badala
yake kuwe na mpango wa kutumia ngozi ghafi hapa nchini na kuleta tija katika
uchumi wa taifa kwa kutengeneza ajira na kuongeza thamani ya mauzo nje.
Mheshimiwa Spika, hatua ya kuzuia
ngozi ghafi kusafirishwa kwenda nje kwa Tanzania itakuwa sio suala jipya kwa
sababu Ethiopia imezuia na kuwekeza katika kiwanda cha viatu, mikanda na bidhaa
za ngozi. Kutokana na Mpango wa Mendeleo ya Ethiopia (GTP – Growth and
Transformation Plan) sekta ya Ngozi itaingiza fedha za kigeni za thamani ya
dola za Kimarekani bilioni 4 kwa mwaka. Hii ni sawa na fedha za kigeni ambazo
Tanzania inapata kutoka kwenye Dhahabu na Utalii kwa pamoja. Ethiopia nchi
iliyokuwa inatembea na bakuli na kulia njaa leo inakuwa nchi ya kupigiwa mfano
na sisi Watanzania! Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda pia amepiga marufuku
kuuza ngozi ghafi nje. Hata nchi ya Pakistani ambayo ndio ngozi zetu zinakwenda
nayo imepiga marufuku mauzo ya ngozi ghafi nje. Serikali ipige marufuku Mauzo
ya ngozi ghafi nje ya Nchi ili kulinda viwanda vya ngozi nchini, kuoongeza
Ajira na kuongeza mapato ya Fedha za kigeni.
Kufuta Kodi ya Ongezeko la Thamani
(VAT) kwa bidhaa za Maziwa
Mheshimiwa Spika, sekta ndogo ya
Maziwa hapa nchini inahitaji kuwekewa maazingira ya kukua ili izalishe ajira na
mapato ya kodi kwa Serikali. Wakati Tanzania ndio nchi ya Afrika Mashariki
inayoongoza kwa kuwa na Ng’ombe wengi lakini inaongoza kwa kuagiza maziwa
kutoka nje yenye thamani ya dola za kimarekani 3.6m. Wakati Kenya imelinda soko
la Maziwa na Bidhaa za Maziwa kwa kuondoa (zero rating) kodi ya VAT kwenye
bidhaa za Maziwa, Waziri wa Fedha hajaonyesha kabisa juhudi zozote za kujengea
uwezo sekta ndogo ya Maziwa hapa nchini na hivyo kuweza kuondolewa kabisa
katika ushindani na kujikuta wafugaji wanakosa kabisa soko la kuuza maziwa yao
hapa nchini. Nchi za Rwanda na Uganda pia zimelinda Maziwa na Bidhaa za maziwa
kwa njia hii. Ni muhimu Serikali kuwianisha kodi hii na Nchi nyingine za Afrika
Mashariki.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani
inapendekeza kufanya marekebisho kwenye sharia ya Kodi ya Ongezeko la Thamani
kwa kufanya ‘zero rating’ kwenye Maziwa na Bidhaa za Maziwa zinazozalishwa hapa
nchini kwa kipindi cha miaka 5 ili kufikisha uzalishaji wa angalau lita 500,000
za maziwa kwa siku kutoka lita 123,000 za sasa na kuweza kutoa ajira kwa
watanzania zaidi ya elfu tatu.
Mheshimiwa Spika, hatua zote za
kuongeza mapato tulizopendekeza pamoja na hatua za Bajeti Mbadala iliyopita
ambazo tunarudia kuzipendekeza zitaongeza Mapato ya Serikali kwa takribani
shilingi bilioni 2,885 kama inavyoonyeshwa katika jedwali hapa chini.
NYONGEZA YA VYANZO
VYA MAPATO MBADALA 2012/2013
Makisio - Bilioni
|
|
Marekebisho ya kodi za misitu
ikiwemo Mkaa
|
130.8
|
Kupunguza misamaha ya kodi, kuzuia
ukwepaji kodi na udanganyifu wa Biashara ya Nje
|
742.74
|
Mauzo ya hisa za serikali
|
415.55
|
Marekebisho ya kodi Sekta ya
madini (kodi ya Mapato, Kodi ya CGT na ushuru mbalimbali) (25% ya Mauzo
ya Madini Nje)
|
578.36
|
Marekebisho ya Kodi na Usimamizi
bora wa Mapato Kampuni za Simu
|
502.26
|
Marekebisho ya Kodi ya SDL
|
243.52
|
Mapato ya wanyamapori
|
61.64
|
Kuondoa msamaha wa ushuru wa
mafuta- kampuni za madini
|
44.9
|
Usimamizi wa mapato ya utalii
|
51.75
|
Kuimarisha biashara katika EAC kwa
kuongeza mauzo
|
114.15
|
JUMLA
|
2,885.67
|
Mheshimiwa Spika, kama
nilivyosema hapo juu, vyanzo hivi vya mapato ni mjumuisho wa vyanzo ambavyo
katika hotuba zetu mbadala za nyuma tumekuwa tukipendekeza, ambapo tumevifanyia
marekebisho kulingana na hali halisi ya uchumi ulivyo kwa sasa, pamoja na
kupendekeza baadhi ya marekebisho ya sheria za kodi ili kuongeza mapato zaidi
kwa Serikali.
DENI LA TAIFA
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani
inasikitika kwa serikali kuendelea kutengeneza madeni kwa Taifa kwa kuendelea
kukopa zaidi kwa matumizi ya kawaida ya serikali. Wakati Serikali inasisitiza
kwamba Deni letu linastahmilika, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali
anaonyesha mashaka makubwa sana kutokana na kasi ya kukua kwa Deni la Taifa.
Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonyesha kuwa
Deni la Taifa linazidi kuongezeka kwa asilimia 38 kutoka shilingi trillion 10.5
mwaka 2009/2010 hadi shilingi trillion 14.4 mwaka 2010/2011. Kwa mujibu wa
Waziri wa Fedha Deni la Taifa limefikia shilingi trillion 20.3 mpaka ilipofika
mwezi Machi mwaka 2012. Ukisoma taarifa ya Mwezi wa Mei 2012 ya Benki Kuu ya
Tanzania, Deni la Taifa sasa limefikia shilingi trillion 22.
Mheshimiwa Spika, Suala hapa sio
ustahmilivu wa Deni kama inavyodai Serikali bali ni kwamba tunakopa kufanyia
nini? Bajeti ya Mwaka 2012/13 inayopendekezwa inaonyesha kwamba Serikali
itakusanya shilingi trilioni 8.7 kama makusanyo ya ndani na itatumia shilingi
trilioni 10.6 kama matumizi ya kawaida. Ni dhahiri kwamba sehemu ya mikopo
ambayo serikali inachukua sasa itakwenda kwenye matumizi ya kawaida. Hatutaki
mikopo kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya posho, kusafiri, magari nk. Tuchukue
mikopo kuwekeza kwenye miradi itakayokuza uchumi na kuzalisha kodi zaidi.
Bajeti inaonyesha kwamba Serikali itakopa shilingi takribani trillion 5 mwaka
2012/13. Serikali ikubali kutekeleza mapendekezo ya Kambi ya Upinzani ya
kuimarisha ukusanyaji wa kodi na kupanua wigo wa kodi katika maeneo muhimu kama
sekta ya madini na mawasiliano, kuzuia misamaha ya kodi, kutokomeza ukwepaji
kodi, na kuepuka matumizi mabaya ili kuepuka madeni yasiyo ya lazima.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani
inapenda kusisitiza kwamba Bunge lifanye ukaguzi maalumu kuhusu akaunti ya Deni
la Taifa ili kuweza kubaini ukweli kuhusu ustahmilivu wa Deni na mikopo ambayo
Serikali inachukua kama inakwenda kwenye Maendeleo na miradi ipi na kama miradi
hiyo ina tija. Vilevile tumependekeza kwamba Mikopo yote ambayo Serikali
inachukua iwe inapata idhini ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi au Bunge
litunge sharia ili kiwango cha juu cha kukopa ambacho Serikali haipaswi kuvuka.
Kuiacha Serikali inaendelea kukopa bila mpango ni kuliweka Taifa rehani na
kupeleka mzigo wa kulipa madeni haya kwa kizazi kijacho. Hatuwezi
kukubali Wazee wetu waishi maisha yao, waishi maisha yetu na pia wakope maisha
ya watoto wetu.
Mheshimiwa Spika, Ukiangali sura ya
Bajeti ya Serikali, inaonyesha kuwa Serikali itakopa fedha zenye masharti ya
kibiashara ndani na nje yenye thamani ya Tshs. Trilioni 2.89 kwa kipindi
hiki cha 2012/13. Athari ya mikopo ya kibiashara ya ndani ni kubwa
sana kwa watanzania, kwanza inawafanya wananchi hasa wajasiriamali wanaokopa
kushindana na Serikali yao, kwani mabenki yatashindwa kuwakopesha wafanyabiashara au
wakikopa watakopa kwa masharti magumu na hasa riba kuwa kubwa. Jambo hili
linapunguza uwezo wa wazalishaji kuongeza uzalishaji hasa viwandani kwa kukosa
mikopo ya uendeshaji. Kama tulivyoshauri hapo juu, Serikali ijiepushe na mikopo
ya masharti ya kibiashara kwa kuongeza makusanyo ya kodi.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani
imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya Serikali kuwa imepata Mshauri
Mwelekezi atakayeishauri katika kujiandaa kufanyiwa tathmini ya uwezo wa kukopa
na kulipa madeni. Serikali ilieleze Bunge ni lini na kwa namna gani
zabuni ya kumpata mshauri huyu ilitangazwa na kama Sheria ya Manunuzi
ilifuatwa.
Mwenendo wa Matumizi.
Mheshimiwa Spika, Serikali inapendekeza Bajeti ya TZS 15
trilioni(USD 8.75 Billion) katika mwaka 2012/13 kama ilivyowasilishwa na Waziri
wa Fedha na Uchumi wiki iliyopita. Uchambuzi wa vitabu vya Bajeti unaonesha kwamba
mafungu ya juu 5 yatakayoongoza kwa matumizi kwenye Bajeti hiyo ni Kama
ifuatavyo;
1. Huduma kwa Deni
la Taifa Tshs 2.7 trilioni (USD 1.69 Billion)
2. Wizara ya Ujenzi. Tshs 1 trilioni (USD 625 Million)
3. Wizara ya Ulinzi Tshs 920 bilioni (USD 575 Million)
4. Wizara ya Elimu Tshs 721 bilioni (USD 451 Million)
5. Wizara ya Nishati na Madini Tshs 641 bilioni (USD 400 Million)
Jumla TZS 5.982 Trilioni(USD 3.74 Billlion)
Chanzo: Vitabu vya Bajeti kwa Wabunge
2. Wizara ya Ujenzi. Tshs 1 trilioni (USD 625 Million)
3. Wizara ya Ulinzi Tshs 920 bilioni (USD 575 Million)
4. Wizara ya Elimu Tshs 721 bilioni (USD 451 Million)
5. Wizara ya Nishati na Madini Tshs 641 bilioni (USD 400 Million)
Jumla TZS 5.982 Trilioni(USD 3.74 Billlion)
Chanzo: Vitabu vya Bajeti kwa Wabunge
Mheshimiwa Spika, Jumla ya mafungu
haya ni sawa na asilimia 40% ya Bajeti yote, kwa hiyo asilimia 40% ya Bajeti
yote imepangwa kwa mafungu 5 tu na kati ya hayo Wizara ni nne tu za Ujenzi,
Elimu, Ulinzi na Nishati na Madini. Wizara ya Kilimo wala Afya hazimo kabisa
katika Wizara 5 zitakazopata fedha nyingi zaidi katika Bajeti. Fungu lenye
kiwango kikubwa zaidi ya Bajeti kuliko vyote ni fungu 22 ambalo ni malipo kwa
Deni la Taifa. Pia sehemu kubwa ya fedha zilizotengwa kwa Ujenzi na Nishati ni
madeni kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya miaka ya nyuma. Shilingi bilioni
40 ambazo zimetengwa kwa ajili ya Mradi wa Kiwira katika Wizara ya Nishati na
Madini ni kwa ajili ya kulipia Madeni ya Kampuni ya TanPower Resources ambayo
iliuziwa Mgodi wa Kiwira na kushindwa kuundeleza.
Mheshimiwa Spika, Madhara ya Deni la Taifa
yanaonekana hapa katika matuumizi ya Serikali ambapo tunapokuwa tunalipa madeni
tunachukuwa rasilimali fedha nyingi kutoka kwenye Miradi ya Maendeleo. Wakati
Bajeti ya Maendeleo ni shilingi trilioni 4.5, Bajeti ya kugharamia Deni la
Taifa ni shilingi trilioni 2.7 (sawa na nusu ya Bajeti nzima ya Maendeleo).
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya 2012/13 ni ya kulipa
madeni zaidi kuliko Bajeti ya kuchochea maendeleo ya Taifa letu. Bajeti hii pia
yaweza pia kuwa ni Bajeti ya kukopa zaidi maana jumla ya TZS 5.1
trilioni (USD 3.19 Billion) zitachukuliwa na Serikali kama
mikopo kutoka vyanzo mbalimbali. Mikopo ya kibiashara ambayo ni mikopo ghali
sana itachukuliwa kwa wingi zaidi kuliko mwaka wa fedha uliopita.
Mheshimiwa Spika, Mgawanyo wa
rasilimali za nchi kwenye sekta za kipaumbele (Miundombinu ya usafirishaji kama
reli, bandari, ndege viwanja vya ndege n.k), Barabara, nishati,kilimo na
mifugo, ili kuinua uchumi zimetengewa fedha kidogo sana kuweza kuleta tija
kulingana na malengo ya Mpango wa Maendeleo kama ulivyopitishwa na Bunge lako
tukufu. Bajeti iliyotengwa kwa ajili ya nishati imeshuka kwa kiwango cha shilingi
40 bilioni, pia kwa mwaka uliopita fedha zilizotengwa kwa ajili ya
miundombinu,reli na TEHAMA zilitengwa shilingi 2,781.4 bilioni kwa
2011/12 ikilinganishwa na shilingi 1,505.1 bilioni kwa mwaka
2010/2011,(hili lilikuwa ni ongezeko la asilimia 85). Kwa bajeti ya mwaka
huu inaonesha sekta zilezile za vipaumbele; bajeti iliyotengwa ni shilingi
1.394.5 bilion ambayo ni pungufu ya asilimia 49.86 kwa kulinganisha na mwaka
2011/2013.
Mheshimiwa Spika, wakati Waziri wa
Fedha analiambia Bunge kuwa ametenga shilingi bilioni 1,383 kwa ajili ya
Usafirishaji na Uchukuzi, Wizara ya Ujenzi imetengewa shilingi bilioni 1,000
kati ya hizo. Wizara ya Uchukuzi yenye Reli, Bandari, Viwanja vya Ndege na
Usafiri wa Maziwa ya Tanganyika, Nyasa na Viktoria imetengewa chini ya shilingi
bilioni 380. Serikali pia haijasema fedha ambazo zilitengwa na Bunge katika
Bajeti inayomaliza muda wake na kuzielekeza kwenye Wizara ya Miundombinu na
Wizara ya Uchukuzi zimetumikaje maana bado wakandarasi wanadai na fedha za Reli
hazikutoka zote kama ilivyopitishwa na Bunge.
Mheshimiwa Spika, wizara nyingi
hazikupata fedha za Maendeleo kama zilivyopitishwa na Bunge. Halmashauri za
Wilaya ndio zilipata hali mbaya zaidi katika kupata fedha za Maendeleo ambapo
kwa wastani ni asilimia 47 tu ya Bajeti ndio ilipelekwa katika Halmashauri za
Wilaya, Miji na Manispaa. Kutokana na hali hii Wabunge kama wawakilishi wa
wananchi walihoji Serikali kwenye Kamati zao na kupata majibu ambayo sio ya
kuridhisha hivyo kupelekea Wabunge kugomea baadhi ya Wizara.
Mheshimiwa Spika, Ushahidi wa hayo
ni baadhi ya Kamati za Kudumu za Bunge kukataa kukubali Makadirio ya
Mapato na Matumizi kwa baadhi ya Wizara zilizo chini ya Kamati hizo. Wizara
ambazo hazikupitishiwa /Kukubaliwa makadirio yake ni pamoja na;
- Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
- Wizara ya Uchukuzi, na (nilishangaa kumwona
Waziri wa Uchukuzi akiwaahidi wananchi pale Jangwani kwamba Reli
inakarabatiwa vya kutosha ilhali Kamati haijapitisha Makadirio ya Matumizi
ya Wizara yake kwa kuwa haikupewa fedha za kutosha)
- Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika
Mheshimiwa Spika, kabla Bunge lako
tukufu halijajadili Makadirio ya Matumizi ya mwaka unaokuja ni vema Serikali
itueleze kwanza fedha zilizotengwa mwaka uliopita na hazikufika hatima yake
nini?
Mheshimiwa Spika, uwiano wa
bajeti iliyotengwa kwa matumizi ya kawaida ambayo ni asilimia 70% wakati bajeti
ya maendeleo asilimia 30% haiwezeshi nchi kupiga hatua ya haraka ya Maendeleo.
Kama ilivyoonyeshwa na Waziri Kivuli Mipango na nitakavyohitimisha hotuba hii, Serikali
imetayarisha Bajeti hii bila kuzingatia masharti yaliyowekwa na Mpango wa
Maendeleo uliopitishwa na Bunge kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu ibara ya 63
(3)(c) kwa kutotenga asilimia 35 ya Mapato ya ndani ya Serikali kwenye Bajeti
ya Maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa
ikitenga fedha kidogo katika miradi ya maendeleo katika bajeti zake. Kwa mujibu
wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), matumizi ya
kawaida ya Serikali yanaongezeka huku matumizi katika shughuli za maendeleo
yanapungua mwaka hadi mwaka. Takwimu katika jedwali hapa chini
zinaonyesha
2009/2010
|
%
|
2010/2011
|
%
|
|
Fedha za matumizi ya kawaida (Sh)
|
6,251,629,581,428
|
73
|
7,587,424,923,903
|
77
|
Fedha za matumizi ya maendeleo (Sh)
|
2,299,010,652,135
|
27
|
2,223,684,150,465
|
23
|
Jumla
|
8,550,640,233,563
|
100
|
9,811,109,074,368
|
100
|
Chanzo: Ripoti ya CAG, uk. 21
Aidha, kwa miaka miwili iliyopita
yaani 2009/2010 na 2010/2011 kumekuwa hakuna uwiano wa fedha za Maendeleo kama
bajeti zilivyopitishwa na Bunge dhidi ya fedha zinazotolewa na hazina kwa ajili
ya maendeleo katika Wizara na Idara. Tazama jedwali;
Bajeti iliyoidhinishwa
|
Fedha halisi zilizotolewa
|
Tofauti (Sh)
|
%
|
|
2009/2010
|
2,825,431,400,000
|
2,299,010,652,135
|
526,420,747,865
|
19
|
2010/2011
|
3,750,684,569,000
|
2,223,684,150,465
|
1,527,000,418,535
|
41
|
Chanzo: Ripoti ya CAG, uk.22
Mheshimiwa Spika, Kutokana na
takwimu hizi, jumla ya Sh. 1,527,000,418,535 au asilimia 41 ya fedha
zilizoidhinishwa kwa maendeleo hazikutolewa katika mwaka wa fedha 2010/2011, na
kiasi cha Sh. 526,420,747,865 au asilimia 19 ya fedha zilizoidhinishwa
mwaka 2009/2010 hazikutolewa pia. Hii ina maana kuwa shughuli za maendeleo za
kiasi hicho cha fedha hazikutekelezwa kwa miaka husika.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya
Upinzani inatafsiri hali hiyo kama utovu mkubwa wa nidhamu ya matumizi ya fedha
za umma kwa upande wa Serikali, Vilivile inaonesha ni jinsi gani Serikali yetu
haithamini maendeleo ndio maana kila mwaka Serikali inazidisha matumizi yake na
kuhakikisha kuwa inayapata kwa wakati huku ikipunguza bajeti ya maendeleo na
kutotoa fedha zote kama zilivyoidhinishwa na mbaya zaidi hata zile zinazotolewa
hazitolewi kwa wakati muafaka. Hii inafanya kukaa hapa Dodoma na kupitisha
Bajeti kuwe hakuna maana maana Bajeti haitekelezwi kama ilivyopitishwa.
Mheshimiwa Spika, Kiasi
kinachotengwa kwa ajili ya maendeleo kimeshuka kutoka shilingi trilioni 4.9
katika mwaka wa fedha 2011/12 hadi kufikia kiasi cha shilingi trililioni
4.5 mwaka huu wa fedha 2012/13. Pamoja na serikali kushindwa kutekeleza
miradi ya maendeleo katika bajeti iliyopita, bado imeendelea kupunguza
bajeti ya maendeleo katika bajeti hii. Ni dhahiri serikali haizingatii
swala la maendeleo ya mwananchi, pia kutoona njia ya kuweka mkazo katika maendeleo
na kuendelea kupuuzia maazimio ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano.
Mheshimiwa Spika, katika Bajeti
mbadala, Kambi ya Upinzani imetenga asilimia 36.06 na kukidhi matakwa ya Mpango
wa Maendeleo ya Taifa kutoka katika mapato ya ndani kwa matumizi ya maendeleo
kama Mpango wa Maendeleo ya Taifa ulivyoelekeza.
Mheshimiwa Spika, Tuliamua kama
Taifa kwamba Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano ndio safina yetu ya kuelekea
nchi ya ahadi (middle income country). Mpango ukapitishwa na Bunge na kuwekwa
sahihi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Inasikitisha kuona kuwa
Serikali inatoboa kisiri siri safina hii wakati tupo kati kati ya maji!
Ninaamini wananchi wanawaona wanaotoboa safina yetu na watawatosa kabla
hawajazamisha Taifa zima kwa kushindwa kutekeleza Mpango unavyoelekeza.
Ubadhirifu wa fedha zinazotengwa
Mheshimiwa Spika, pamoja na fedha
za maendeleo kutolewa kidogo kulinganisha na bajeti inayopitishwa na Bunge,
bado kumekuwepo na matumizi yasiyo na tija na ubadhirifu mkubwa.
Mheshimiwa Spika, upotevu wa
fedha za umma umeendelea kuwa kikwazo
kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi. Uchambuzi wetu juu ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2010/2011 pekee, umebaini takribani jumla ya Bilioni 12.9 (12,968,168,985) za fedha za umma zimepotea kama ongezeko kutoka shilingi billion 11.9 (11,152,048,065) ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 14 ya upotevu wa fedha za Serikali kwa mwaka wa fedha 2009/2010,hii inaonyesha kuwa Serikali inaona ni jambo la kawaida kupoteza viwango hivi vya pesa za Serikali na kambi ya upinzani kuwasisistiza wananchi kuendelea kuitathmini Serikali yao sasa ili kuweza kufanya maamuzi sahihi dhidi ya Serikali yao.
kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi. Uchambuzi wetu juu ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2010/2011 pekee, umebaini takribani jumla ya Bilioni 12.9 (12,968,168,985) za fedha za umma zimepotea kama ongezeko kutoka shilingi billion 11.9 (11,152,048,065) ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 14 ya upotevu wa fedha za Serikali kwa mwaka wa fedha 2009/2010,hii inaonyesha kuwa Serikali inaona ni jambo la kawaida kupoteza viwango hivi vya pesa za Serikali na kambi ya upinzani kuwasisistiza wananchi kuendelea kuitathmini Serikali yao sasa ili kuweza kufanya maamuzi sahihi dhidi ya Serikali yao.
MAPENDEKEZO YA KAMBI YA UPINZANI
SERA YA MATUMIZI 2012/13 KWA BAJETI
MBADALA
Mheshimiwa Spika, lengo kuu la
Bajeti Mbadala ni kuhakikisha uchumi unakua katika maeneo ya vijijini kwa kati
ya asilimia 6 na 8 ili kuleta Maendeleo ya wananchi na kutokomeza umasikini.
Kwa njia hiyo ni dhahiri wananchi wapatao milioni 30 waishio vijijini
watanufaika na matumizi ya raslimali zao.
Vipaumbele vya bajeti ya Matumizi.
i.Kujenga Mazingira ya Ukuaji wa uchumi
vijijini (rural growth) kwa kuboresha miundombinu ya umeme, barabara, maji na
miundombinu ya Umwagiliaji. Tunapendekeza kutumia shilingi bilioni 600 kila
mwaka (bilioni 150 kwa kila sekta niliyotaja). Fedha hizi zitasimamiwa na
Mamlaka ya Maendeleo Vijijini (Rural Development Authority – to be established)
itakayokuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
ii.Kukarabati Reli ya Kati na matawi
yake ya Tanga/Arusha na Mpanda. Tutatenga tshs 443bn kwa RAHCO kwa ajili ya
Reli. Lengo ni kuhakikisha Reli ya Kati inafikia uwezo wa kusafirisha Tani 1.5m
kwa mwaka na hivyo kulipatia Taifa fedha za kigeni katika sekta ya usafirishaji
kupitia Bandari ya Dar es Salaam. Tunataka sekta ya usafirishaji iliingizie
Taifa fedha za kigeni mpaka dola za kimarekani 1.5 bilioni kutoka dola 0.5
bilioni za sasa.
iii.Kuboresha Elimu na Afya hasa kwa
Shule na Zahanati/Vituo vya Afya vya Vijijini kwa kutoa motisha kwa wafanyakazi
wa Sekta hizi walio kwenye Halmashauri za Wilaya. Tunapendekeza posho za
Mazingira ya Vijijini kwa Walimu, Madaktari na Manesi sawa na mara moja na nusu
ya Mishahara yao. Vile vile tutaongeza mishahara ya Walimu, Manesi na Madaktari
kwa asilimia 50, pamoja na kuboresha stahili zingine za kazi ili kuvutia
Watanzania wengi zaidi katika maeneo haya na kuboresha huduma zao kwa wananchi.
iv.Kuongeza Kima cha chini cha Mshahara
kwa Wafanyakazi wa Umma mpaka Tshs 315,000 kwa Mwezi
v.Kuanzisha Pensheni ya uzeeni kwa
Wazee wote nchini wenye umri wa zaidi ya miaka 60.
vi.Kujenga Uwezo wa Viwanda vya ndani
ili Kuuza nje bidhaa za kilimo na mifugo zilizoongezewa thamani. Tutazuia kuuza
nje Korosho ghafi na Ngozi ghafi kwa kuanzia. Lengo ni kufufua viwanda vyote
vya nguo na kuanzisha viwanda vipya kwa kutoa motisha kwa wawekezaji
watakaotumia malighafi za hapa nchini.
vii.Kupunguza mzigo wa matumizi ya magari
ya Serikali kwa kupiga mnada baadhi ya ‘mashangingi’ na kuweka mfumo wa
kukopesha Magari kwa watumishi wote wa Umma wanaostahili Magari kama
alivyofanya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania. Katika Taarifa yake kwa Kamati ya
Fedha na Uchumi, Waziri wa Fedha alitamka, ‘….kufanya mapitio ya stahili za
aina za magari kwa viongozi wa ngazi mbalimbali na kuandaa mwongozo wa
kugharamia ununuzi wa vyombo vya usafiri ili kupunguza matumizi ya magari,
mafuta na matengenezo ya magari…’ kama hatua za kubana matumizi. Hatua hii ya
kupunguza gharama za magari Waziri hakuisema kabisa katika hotuba yake Bungeni.
viii.Kuendelea kusisitiza kufutwa kwa
posho za vikao katika mfumo mzima wa malipo na stahili kwa watumishi wa Umma.
Katika Taarifa yake kwa Kamati ya Fedha, Waziri wa Fedha alitamka ‘…. Kufanya
mapitio ya posho na stahili zote kwa lengo la kuziwianisha….’ Suala hili nalo
Waziri hakulizungumza kabisa katika Hotuba yake Bungeni.
ix.Kuanzisha Chuo Kikuu cha Mtwara
(Mtwara University for Petroleum Studies) ili kuzalisha wataalamu wa kutosha wa
Sekta ya Mafuta na Gesi na kuliandaa Taifa kuwa na wasomi mahiri wa maeneo hayo
na hivyo kufaidika na Utajiri wa Mafuta na Gesi uliopo nchini kwetu.
Tunapendekeza shilingi bilioni 200 mwaka huu katika Bajeti ya Wizara ya Elimu
kwa ajiri ya Mradi huu.
x.Kutunga sheria mpya ya Mashirika ya
Umma (Public Corporations Act) ili kujengea uwezo Ofisi ya Msajili wa Hazina
ili kusimamia vyema Mashirika yote ya Umma ambayo Serikali inamiliki kwa zaidi
ya asilimia 100 na kutoa nguvu za kisheria kwa Shirika la CHC kuweza kusimamia
hisa za Serikali katika Kampuni na Mashirika ambayo Serikali inamiliki chini ya
asilimia 50.
xi.Kupunguza gharama za safari za nje
kwa kupunguza ukubwa wa misafara na madaraja ya kusafiria. Eneo hili la safari
za nje limekuwa likiigharimu Serikali fedha nyingi sana.
Mheshimiwa Spika, kufuatia hatua
mbali mbali za kikodi tulizozichukua Kambi ya Upinzani inapendekeza Bajeti ya
shilingi trilioni 15 ambazo zitapatikana kwa Mapato ya ndani ya shilingi
trilioni 11.9 na misaada na mikopo ya kibajeti ya shilingi trilioni 3.2 kama
ilivyopendekezwa na Serikali. Kambi ya Upinzani inapendekeza Serikali kutokukopa
kibiashara ili kudhibiti ukuaji wa Deni la Taifa.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani
Bungeni inapendekeza kwamba Serikali itatumia shilingi trilioni 9 katika
Matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 6 kama Matumizi ya Maendeleo. Katika
fedha za Maendeleo, asilimia 35 ya Mapato ya ndani yameelekezwa huko kama
ilivyoagizwa na Mpango wa Maendeleo ya Taifa ulioidhinishwa na Bunge kwa mujibu
wa Katiba.
SURA YA BAJETI
MBADALA YA MWAKA 2012/2013
MAPATO
|
SHILINGI MILIONI
|
||
A
|
Mapato ya ndani
|
11,889,078
|
|
i)mapato ya kodi (TRA)
|
|||
ii)Mapato yasiyo ya kodi
|
|||
B
|
Mapato ya Halmashauri
|
||
C
|
Mikopo na Misaada ya kibajeti (GBS)
|
842,487
|
|
D
|
Misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo nay a kisekta
|
2,314,231
|
|
i)Misaada
|
1,465,461
|
||
ii)Misaada na mikopo kisekta
|
415,137
|
||
iii)MCC(MCA-T)
|
433,634
|
||
Jumla ya Misaada na mikopo ya kibajeti
|
3,156,718
|
||
JUMLA YA MAPATO YOTE.
|
15,045,796
|
||
MATUMIZI
|
|||
E
|
Matumizi ya Kawaida
|
9,000,000
|
|
H
|
Matumizi ya Maendeleo
|
||
(i)Fedha za ndani
|
4,161,177
|
||
(ii)Fedha za Nje
|
1,884,619
|
||
Jumla ya matumizi ya maendeleo
|
6,045,796
|
||
JUMLA YA MATUMIZI YOTE.
|
15,045,796
|
Hitimisho
Fedha za Rada
Mheshimiwa Spika, Wakati Kamati za
Bunge zilipokaa kujadili taarifa ya Serikali kuhusu Mfumo wa Mapato na
Matumizi, Waziri wa Fedha na Uchumi alitoa Taarifa kuhusu Fedha za Rada
zilizorejeshwa, jumla ya shilingi 72.3 bilioni ambazo zilipokelewa tarehe 26
Machi, 2012. Kwa mshtuko wa Wabunge, Waziri aliiambia Kamati kuwa mchakato wa
manunuzi ya vitabu na madawati kwa kutumia fedha hizi ulikuwa umeanza chini ya
Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI. Fedha hizi hazijawahi kupitishwa na Bunge lako
tukufu. Kitendo cha Serikali kuzitumia kabla ya kupitishwa na Bunge ni kuvunja
sheria za Fedha kuhusiana na masuala ya Bajeti. Wakati Waziri akiwasilisha
Hotuba yake hakugusia kabisa suala la fedha zilizorejeshwa kutokana na Ununuzi
wa Rada!
Mheshimiwa Spika, Kambi ya
upinzani inataka maelezo ya Serikali juu ya Fedha hizi na utaratibu wa
kuzitumia. Kambi inataka kufahamu vigezo vilivyotumika kuteua mikoa ya Mwanza,
Morogoro na Dar es Salaam kutumia fedha hizi. Kambi pia inapenda kufahamu Deni
lililochukuliwa kununua Rada hii iliyoleta kashfa kubwa sana hapa nchini
limefikia kiasi gani kulilipa na tukililipa tutakuwa tumelipa kiasi gani kwa
ujumla.
Mheshimiwa Spika, Uumbaji wa bajeti
ya Serikali umekuwa ni ule ambao unapendelewa zaidi na wale wavivu wa kufikiri,
yaani mfumo rahisi, wataalamu wanauita Incremental Budgeting. Mfumo
huu hujikita zaidi katika kutizama ukuaji wa mapato na kugawa mapato hayo kwa
mtindo wa nyongeza ya asilimia Fulani toka katika bajeti iliyotangulia. Mfumo
huu huacha kuzingatia mambo mengi mtambuka. Mfano, tunaweza tizama sekta
mojawapo ya umeme ambapo tukifanya uumbaji wa bajeti kwa mfumo wa kiasi cha
nyongeza (incremental budget) kuna thamani halisi ambazo ukizitizama kwa bei
wazi ya soko tayari zimepaa sana ndani ya miezi kumi na miwili.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani
Bungeni, tukiwa ni serikali ambayo tunasubiri kukabidhiwa dola, tunapendekeza
kwamba ni vema tukaanza kutizama uwezekano wa matumizi ya Zero
Budgeting ambapo japo ni mfumo ambao unahitaji kazi ya ziada, lakini
una faida sana kwani hutizama mipango ya matumizi kulingana na wakati uliopo
huku ikifanya rejea ya wakati uliopita.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani
pia inapendekeza kwamba Bajeti za Mashirika ya Umma ziwe sehemu ya Bajeti Kuu
ya Nchi kwani kuna masuala mengi yanayotekelezwa na Mashirika haya na Wananchi
kupitia Bunge hawayajui. Ni vema katika mfumo mpya wa Bajeti tutakaokuwa nao
kufuatia mapendekezo ya Spika wa Bunge ambapo kutakuwa na Ofisi ya Bajeti ya
Bunge na Kamati ya Bunge ya Bajeti, Sheria ya Bajeti (Fiscal Responsibility
Act/Budget Act) izingatie suala la kuziweka kama viambatisho Bajeti za
Mashirika ya Umma katika Bajeti ya Nchi.
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya
Serikali ya mwaka huu kama ilivyowasilishwa na Waziri wa Fedha imewasahau
kabisa wananchi wa vijijini na haina mkakati wowote wa kuwakomboa watanzania
walio wengi wanaoishi huko. Mipango mingi ya kikodi katika sera ya Mapato ya
Serikali itasaidia wakazi wa mijini ambao ni asilimia 25 tu ya Watanzania wote.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani
inapenda kuweka msisitizo kwamba Tanzania bado ni nchi ya Wakulima maana robo
tatu ya Watanzania wanaishi vijijini ambapo hawajui hizi hadithi za Uchumi
kukua tunazoimba na kupewa sifa kila siku. Hawa ni watu milioni 30 ambao hawana
Maji, hawana Umeme, mazao yao hayafiki sokoni maana hawana barabara nzuri,
shule wanazosoma watoto wao hazina walimu maana wanakimbia mazingira magumu.
Hawa Watanzania wa chini milioni 30 (The Bottom 30M) tunaowawakilisha hawana
bima mazao yakiharibiwa na wala hawana pensheni wanapokuwa wamezeeka na
kupoteza nguvu za kufanya kazi. Hawa ‘The Bottom 30M’ bado wanaishi maisha
walioshi babu zetu. Hawa Watanzania milioni 30 tumewasahau. Tunajenga Mataifa
mawili ndani ya nchi moja, moja la mafukara (wanavijiji) na moja la wanaojiweza
(wamijini).
Mheshimiwa Spika, Kama tunataka
kujibu kitendawili cha kuwa na Uchumi unaokua kwa kasi lakini haupunguzi
umasikini inabidi kuelekeza nguvu zetu vijijini walipo Watanzania wengi. Kukuza
Uchumi wa Vijijini kwa kuwekeza kwenye misingi ya kujenga uchumi imara ndio
njia pekee ya kutokomeza ufukara wa Watanzania.
Mheshimiwa Spika, Bajeti Mbadala ya
Kambi ya Upinzani mwaka huu ni Bajeti ya Ukombozi wa mwananchi. Licha ya kwamba
tunahitaji ukuaji wa kasi zaidi wa uchumi. Changamoto sasa ni namna gani ukuaji
huu wa uchumi unawafikia wananchi milioni thelathini wa Vijijini na kuboresha
maisha yao.
Mheshimiwa Spika, KWA KUWA
Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano uliwasilishwa Bungeni na Serikali na kupata
pongezi nyingi sana kutoka kwa waheshimiwa wabunge lakini cha kushangaza
Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi imeshindwa kuutekeleza kwa vitendo mpango
huu wa Taifa. Mwaka wa kwanza Mpango haukuwekewa fedha kwa kuwa ulikuwa wa
Mpito. Mpango unahitaji angalau shilingi trillion Nane kila mwaka ili uweze
kutekelezwa. Mpango ulipata shilingi trillion moja tu mwaka 2011/12.
Mheshimiwa Spika, KWA KUWA Bunge
liliazimia namna ya kuhakikisha tunapata fedha za kuendeleza nchi yetu sisi
wenyewe, naomba kunukuu ukurasa wa 92 kifungu cha 4.3.1 katika Mpango wa
Maendeleo wa miaka mitano toleo la kiswahili kama ifuatavyo ‘kwa
kuelewa kuwa wakati wote kutakuwa na miradi ya uwekezaji nje ya mpango,
serikali, kuanzia sasa, itakuwa inatenga asilimia 35 ya makadirio ya
mapato yake ya ndani kwa ajili ya kugharamia bajeti ya maendeleo kila
mwaka’ mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika, KWA KUWA
katika makadirio ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2012/13 Serikali
imetenga asilimia sifuri ya Mapato ya ndani kwa ajili ya kugharamia Bajeti ya
Maendeleo. Serikali hii imeshindwa kusimamia ahadi zake yenyewe kama
inavyoonekana katika mpango wa maendeleo ya miaka mitano. Serikali hii ya CCM
imeshindwa kuheshimu Uamuzi uliopitishwa na Bunge kwa mujibu wa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Mheshimiwa Spika, KWA KUWA Kwa
mujibu wa ibara ya 63(3)(c ) madaraka ya Bunge ni pamoja na ‘Kujadili na
kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa
kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano, na kutunga sheria ya kusimamia
utekelezaji wa mpango huo”. Bunge liliidhinisha Mpango kwa mujibu wa
ibara tajwa ya Katiba.
Mheshimiwa Spika, KWA KUWA Bajeti
ya mwaka 2012/13 iliyowasilishwa Bungeni na Waziri wa Fedha na Uchumi
haikukidhi matakwa ya Mpango wa Maendeleo kama ambavyo ulipitishwa na Bunge,
HIVYO BASI,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
iiondoe (withdraw) Bungeni Bajeti iliyoileta ili ikatayarishwe upya ili ikidhi
matakwa (compliance) ya Mpango wa Maendeleo kama ulivyoidhinishwa na Bunge na
kusainiwa na Rais wa nchi.
Mheshimiwa Spika Naomba Kuwasilisha
………………………………………………….
Kabwe Zuberi Zitto,
Mb
Waziri wa Fedha na
Uchumi Kivuli
18.06.2012
SURA YA BAJETI YA SERIKALI KWA
MWAKA 2012/2013.
TOFAUTI KATI YA BAJETI YA SERIKALI NA
BAJETI MBADALA YA KAMBI RASMI YA UPINZANI
Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013
|
|
Kukuza uchumi vijijini.
|
Mwelekeo na malengo ya Serikali hauleweki, hatua zilizochukuliwa
ni koboresha uchumi wa mijini.
|
Njia mbadala zinazotekelezeka za kupunguza mfumuko wa bei.
|
Kuwa na njia zilezile zilizoshindwa mwaka wa fedha uliopita za
kupunguza mfumuko wa bei.
|
Kunufaika na mapato ya mitaji “Capital gains” kwa kutoza kodi
kwa mali za kampuni zilizopo nchini kwa mauzo yanayofanyika nje ya nchi na
hivyo kupanua wigo wa TRA kutoza kodi
|
Kutoza hisa kwa mauziano ya hisa pekee kwa mauziano
yanayofanyika nje. Hisa inapunguza wigo wa TRA kutoza kodi.
|
Kupanua wigo wa kodi ya tozo la ujuzi (SDL)kwa kuijumuisha
serikali na mashirika ya umma na kupunguza mzigo kwa sekta binafsi pekee.
|
Kupitia upya SDL bila kuonyesha namna itakavyofanyika.
|
Kupunguza misamaha ya kodi kutoka 3% ya sasa hadi 1% ya pato la
taifa.
|
Kurudia ahadi zilezile za mwaka jana za kupitia upya misamaha ya
kodi bila kuleta mrejesho wa kile walichokifanya.
|
Kuboresha kodi sekta ya madini ili kupelekea taifa kupata
nagalau 25% ya mazuo ya madini nje kama mapato ya serikali.
|
Kutokuwa na hatua yoyote ya kuongeza mapato ya Serikali kutoka
katika sekta ya madini.
|
Kulipa kima cha chini cha mshahara kuanzia shilingi 315,000.
|
Kulipa shilingi 170,000 kama kima cha chini.
|
Kulipa pensheni kwa wazee wote kuanzia miaka 60 na kuendelea
|
Kutokuwa na mfumo wa pensheni kwa wote.
|
Kushusha kiwango cha chini kodi ya mapato kwa wafanyakazi (PAYE)
kutoka 14% hadi 9% ili kumpunguzia mfanyakazi makali ya maisha na
kutoza kodi zaidi kwa watu wenye kipato kikubwa
|
Kubaki na kiwango kilekile cha chini cha kodi ya 14% na kubakiza
mfumo ule ule wa kodi ya Mapato unaomfanya Masikini alipe zaidi ya Tajiri.
|
Kuziba mianya kwa makampuni ya simu kukwepa kutokulipa
kodi ya mapato.
|
Kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye muda wa maongezi na hivyo
kumwongezea gharama mwananchi.
|
Kuondoa mikopo ya kibiashara ili kulipunguzia taifa mzigo wa
madeni
|
Kuendelea mikopo na hivyo kuongeza deni la taifa. mingi ya
kibiashara.
|
Kutenga asilimia 35 ya mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji
wa miradi ya maendeleo kama ilivyoelekezwa kwenye mpango wa maendeleo wa
miaka mitano.
|
Kutenga asilimia sifuri ya fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya
miradi ya maendeleo na hvyo kutokutekeleza mpango wa taifa .
|
Utegemezi wa Bajeti 21.3%
|
Utegemezi wa Bajeti 42.37%
|
JEDWALI LA ULINGANISHO WA ASILIMIA
KWA BAJTEI MBILI
‘Licha ya kwamba tunahitaji ukuaji wa
kasi zaidi wa uchumi. Changamoto sasa ni namna gani ukuaji huu wa uchumi
unawafikia wananchi milioni thelathini wa Vijijini na kuboresha maisha yao.’ Zitto Kabwe, Waziri Kivuli wa Fedha, Tanzania.
No comments:
Post a Comment